Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kipindi Kibaya Sana kwa Wafungwa Huko Australia

Kipindi Kibaya Sana kwa Wafungwa Huko Australia

Kipindi Kibaya Sana kwa Wafungwa Huko Australia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

JOHN HILL: Alihukumiwa kwa kuiba kitambaa cha kitani chenye thamani ya peni sita akapelekwa uhamishoni huko Australia kwa miaka saba.

ELIZABETH BASON: Alihukumiwa kwa kuiba kitambaa cha pamba chenye urefu wa meta 6.4. Ijapokuwa alihukumiwa kunyongwa, hukumu yake ilibadilishwa akapelekwa uhamishoni kwa miaka saba.

JAMES BARTLETT: Alipatikana na hatia ya kuiba kilogramu 450 za nyuzi. Alipelekwa uhamishoni huko Australia kwa miaka saba.

GEORGE BARSBY: Alipatikana na hatia ya kumshambulia William Williams na kumwibia kibeti cha hariri, saa ya dhahabu, na sarafu sita za dhahabu (zenye thamani ya pauni sita hivi za Uingereza). Alihukumiwa kunyongwa, lakini hukumu hiyo ilibadilishwa akapelekwa kuishi uhamishoni hadi kifo.

HIYO ni mifano minne tu ya watu waliohukumiwa huko Uingereza na kupelekwa uhamishoni huko Australia mwishoni mwa karne ya 18. Watu wapatao 160,000 walihukumiwa kwa njia iyo hiyo katika kile kipindi kibaya sana kwa wafungwa. Kwa kawaida, wanawake walihukumiwa kifungo cha miaka 7 hadi 14 hata wakiwa na watoto wao.

Bill Beatty anasema hivi katika kitabu chake Early AustraliaWith Shame Remembered: ‘Watu wengi waliodaiwa kuwa wahalifu huko Australia walikuwa wavulana na wasichana ambao hawakuwa wamefikia umri wa miaka 13.’ Beatty asema kwamba mmojawapo wa wafungwa hao alikuwa mvulana wa miaka saba. Mvulana huyo alipelekwa uhamishoni huko Australia “hadi kifo.”

Hata hivyo, wafungwa wengine hawakuumia sana. Maisha ya wafungwa fulani hata yalikuwa mazuri zaidi baada ya kupelekwa uhamishoni. Matukio mengi katika kipindi hicho yalitofautiana; kipindi hicho kilikuwa cha ukatili na huruma, cha kifo na tumaini. Na mambo yote hayo yalianzia Uingereza.

Kipindi cha Wafungwa Chaanza

Katika karne ya 18, mabadiliko ya kijamii yalitukia huko Uingereza nayo yaliongeza uhalifu ambao mara nyingi ulisababishwa na ufukara. Ili kumaliza uhalifu, wenye mamlaka walitunga sheria kali na adhabu kali. Mapema katika karne ya 19, makosa 200 hivi yalikuwa na hukumu ya kifo. Msafiri mmoja alisema hivi: “Unaweza kuhukumiwa kifo kwa kuiba kitu kidogo sana.” Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 11 alinyongwa kwa sababu ya kuiba kitambaa cha mkono.

Hata hivyo, mwanzoni mwa karne ya 18, sheria fulani ilitungwa ili mara nyingi wahalifu wapelekwe kwenye makoloni ya Uingereza huko Amerika Kaskazini badala ya kuhukumiwa kifo. Hivyo, muda si muda, wafungwa wapatao 1,000 walikuwa wakihamishwa kwa meli kila mwaka. Mwanzoni, walipelekwa hasa huko Virginia na Maryland. Lakini zoea hilo lilikoma wakati makoloni hayo yalipopata uhuru kutoka kwa Uingereza katika mwaka wa 1776. Baadaye, wafungwa walipelekwa kwenye magereza mabaya ndani ya meli zilizokuwa kwenye mto Thames huko London. Kwa wazi, magereza hayo yalikuwa madogo sana. Basi, ni hatua gani ambayo ingechukuliwa?

Nahodha James Cook, aliyekuwa mvumbuzi, alisuluhisha tatizo hilo alipofanya eneo la New Holland—ambalo sasa linaitwa Australia—liwe mali ya Uingereza. Punde baadaye, mnamo mwaka wa 1786, pwani ya mashariki ya Australia iliteuliwa iwe mahala pa kuadhibia wafungwa. Mwaka uliofuata, safari iliyoitwa “Msafara wa Kwanza” ilianza huko Uingereza ili kuanzisha koloni la New South Wales. * Safari nyingine zilifuata, na punde baadaye vijiji kadhaa vya wafungwa vikaanzishwa huko Australia, kutia ndani kijiji kimoja kwenye Kisiwa cha Norfolk, umbali wa kilometa 1,500 kaskazini-mashariki ya Sydney.

Magumu Baharini

Wafungwa waliokuwa katika safari za kwanza kuelekea vijiji vya wafungwa walikabili magumu mengi sana, kwani walijazwa kupita kiasi katika sehemu za chini za meli zenye unyevu na uvundo. Mamia ya wafungwa walikufa njiani na wengine walikufa mara tu walipofika. Watu wengi walikufa kutokana na ugonjwa wa kiseyeye. Hata hivyo, baada ya muda madaktari waliagizwa kusafiri na wafungwa katika meli hizo, hasa katika zile zilizokuwa na wanawake. Hivyo, idadi ya vifo ikapungua sana. Hatimaye, meli zilizokwenda kasi zilipunguza muda wa safari hiyo toka miezi saba hivi hadi miezi minne, na jambo hilo pia likapunguza sana idadi ya vifo vya abiria.

Hatari nyingine ilikuwa kuzama kwa meli. Meli ya wafungwa iliyoitwa Amphitrite ilikumbwa na upepo mkali karibu na pwani ya Ufaransa, siku tano baada ya kuondoka Uingereza. Meli hiyo ilipigwa sana na upepo huo kwa siku mbili. Kisha, mnamo Agosti 31, 1883, meli hiyo ikazama saa kumi na moja jioni, umbali wa kilometa moja tu kutoka ufukoni.

Watu walikatazwa kutoa msaada, na mashua za kuokolea hazikufunguliwa. Kwa nini? Eti kwa sababu wafungwa—wanawake na watoto 120—wangetoroka! Kwa hiyo, baada ya muda wa saa tatu zenye kuogopesha, meli hiyo iliyovunjika-vunjika ikazama na kumwaga abiria baharini. Wengi wa mabaharia na wale wanawake na watoto 120 walikufa. Katika siku chache zilizofuata, mawimbi yalisukuma miili 82 hadi ufukoni. Kati ya miili hiyo, kulikuwa na mwili wa mwanamke mmoja aliyemshika mtoto wake kwa nguvu sana hata baada ya kufa.

Nyakati Nyingine Ilikuwa Afadhali Kufa

Gavana wa New South Wales, Bwana Thomas Brisbane, alitangaza kwamba wafungwa wabaya zaidi wa New South Wales na Tasmania walipaswa kupelekwa kwenye Kisiwa cha Norfolk. Alisema hivi: “Mhalifu anayepelekwa huko asitazamie kamwe kutoka huko.” Bwana Ralph Darling, aliyekuwa gavana baadaye, aliazimia kufanya kisiwa hicho kuwa “mahala pa adhabu [kali sana], ila kifo.” Kisiwa cha Norfolk kikawa mahala pa adhabu kali sana, hasa wakati John Price, ambaye alitoka katika ukoo wa kikabaila, alipokuwa gavana.

Inasemekana kwamba Price “alijua kwa usahihi kabisa jinsi akili ya mhalifu inavyofanya kazi, na jambo hilo, pamoja na jinsi alivyotekeleza Sheria bila huruma, lilimfanya aweze kuwadhibiti sana [wafungwa hao].” Price aliwaadhibu watu walioimba, wale waliotembea polepole, au wale walioshindwa kusukuma mikokoteni yenye mawe kwa kuwahukumia viboko 50 au kifungo cha siku kumi katika jela yenye wafungwa wengine 13, huku kukiwa na nafasi ya kusimama tu.

Wafungwa wengi waliona ni afadhali kufa. Kasisi mmoja aliandika hivi kuhusu uasi wa wafungwa 31, ambao 13 kati yao waliuawa na 18 walisamehewa adhabu ya kifo: “Ni ukweli mtupu kwamba kila mtu aliyesamehewa adhabu ya kifo alilia kwa uchungu, na kwamba kila mtu aliyesikia akiadhibiwa kifo alipiga magoti, bila kutoa machozi, na kumshukuru Mungu.” Kasisi huyo aliongeza hivi: “Pingu zilipofunguliwa na adhabu ya kifo kusomwa, watu hao walipiga magoti na kukubali jambo hilo kuwa mapenzi ya Mungu. Kisha, [watu hao waliohukumiwa] walisukumwa na hisia zao kubusu miguu ya mfishaji wao.”

Kwa kuwa makasisi hawangeweza kuadhibiwa, ni wao peke yao waliothubutu kushutumu ukatili huo. Kasisi mmoja aliandika hivi: ‘Siwezi kufafanua kikamili ukatili ambao [Price] anawatendea wafungwa hao. Ni jambo linalochukiza, na anafanya hivyo bila kuadhibiwa.’

Matumaini Kidogo

Nahodha Alexander Maconochie alipowasili, mnyanyaso ulipungua kwa kadiri fulani katika Kisiwa cha Norfolk katika mwaka wa 1840. Alibuni mfumo wa kuwapa wafungwa maksi. Kupitia mfumo huo, wafungwa walipewa thawabu walipofanya maendeleo na hiyo iliwawezesha kuachiliwa huru baada ya kupata kiasi fulani cha maksi. Maconochie aliandika hivi: ‘Naamini kwamba mfungwa anaweza kubadilika, iwapo mbinu zinazofaa zinatumiwa. Sikuzote, akili ya mwanadamu inaweza kurekebishwa maadamu inatumiwa kwa njia inayofaa badala ya kudhoofishwa kwa ukatili au kwa kufungiwa ndani ya gereza lenye hali mbaya.’

Mabadiliko ambayo Maconochie alileta yalitokeza mafanikio hivi kwamba baadaye mbinu zake zikatumiwa huko Uingereza, Ireland, na Marekani. Hata hivyo, ijapokuwa Maconochie aliwezesha wafungwa kutendewa vizuri, aliwaudhi watu fulani mashuhuri ambao alichukia mbinu zao za kushughulika na wafungwa. Kwa hiyo, aliondoshwa mamlakani. Alipoondoka, matendo ya kikatili yalianza tena kwenye Kisiwa cha Norfolk. Lakini hayakuendelea kwa muda mrefu. Katika mwaka wa 1854, baada ya makasisi kulalamika sana, kisiwa hicho kiliacha kutumiwa kama mahala pa wafungwa, na wafungwa wakahamishwa hadi mji wa Port Arthur huko Tasmania.

Watu waliogopa sana mji wa Port Arthur, hasa katika miaka hiyo. Hata hivyo, wafungwa waliokuwa huko hawakutendewa kwa ukatili kama ilivyokuwa kwenye Kisiwa cha Norfolk. Kwa mfano, tangu mwaka wa 1840, kwa ujumla wafungwa waliokuwa huko Port Arthur hawakuwa wakichapwa mijeledi.

Katika kitabu kinachoitwa Port Arthur—1830-1877, Ian Brand anaandika kwamba George Arthur, yule gavana mkali wa Tasmania, alitaka koloni hiyo “ijulikane kwa adhabu kali.” Kwa upande mwingine, Arthur alitaka kila mfungwa ajue “thawabu za tabia njema na adhabu za kufanya mabaya.” Kwa hiyo, aliwagawa wafungwa hao katika vikundi saba, kuanzia wale waliopewa kifungo cha nje kwa sababu ya tabia njema hadi wale waliohukumiwa kufanya kazi ngumu wakiwa wamefungwa pingu.

Uhamisho Ukawa Baraka kwa Wengi

Beatty anaandika hivi: ‘Mara nyingi wafungwa walikuwa na matumaini ya kufanikiwa katika vijiji vya wafungwa kuliko ilivyokuwa katika nchi yao kwa sababu walipata fursa za kufanikiwa maishani huko. Hata hivyo, wale wafungwa waliokuwa huko Port Arthur, Kisiwa cha Norfolk na kwingineko wakati kulipokuwa na uonevu mwingi huko ndio hawakuweza kufanikiwa.’

Kwelikweli, wafungwa waliosamehewa makosa yao kabla ya kumaliza kifungo chao, na pia wale waliomaliza kifungo chao, waligundua kwamba wao na familia zao wangeweza kufanikiwa maishani. Kwa hiyo, ni wachache tu waliorudi Uingereza baada ya kuachiliwa.

Gavana Lachlan Macquarie, mtetezi wa wafungwa walioachiliwa, alisema hivi: “Mtu anapowekwa huru, matendo yake ya zamani hayapasi kukumbukwa au kutumiwa kumzuia; acheni afanye lolote analotaka kwa uhuru kwa sababu amefanya matendo mema kwa muda mrefu na amethibitisha kwamba anastahili.”

Macquarie alitenda kulingana na maneno yake kwa kuwapa wafungwa walioachiliwa mashamba. Kisha aliwaagiza wafungwa wawasaidie wale walioachiliwa katika mashamba yao na kufanya kazi mbalimbali nyumbani.

Baada ya muda, watu wengi wenye bidii walioachiliwa kutoka gerezani walitajirika, wakaheshimiwa, na wengine wakawa mashuhuri. Kwa mfano, Samuel Lightfoot, alisaidia sana kuanzisha hospitali za kwanza huko Sydney na Hobart. William Redfern akawa daktari anayeheshimiwa, na Francis Greenway alichora ramani za majengo mbalimbali huko Sydney na kwingineko.

Hatimaye mnamo mwaka wa 1868, baada ya miaka 80, wafungwa waliacha kupelekwa uhamishoni huko Australia. Leo, kuna jamii mbalimbali za watu huko Australia na hakuna dalili nyingi za kilichotukia katika miaka hiyo ya zamani. Sasa yale magofu ya vile vijiji vya wafungwa ni vivutio tu vya watalii. Hata hivyo, bado kuna mambo mazuri ambayo yamesalia kutoka katika kile kipindi cha wafungwa: madaraja, majengo ya kale, na hata makanisa—yaliyojengwa na wafungwa. Mengine yangali katika hali nzuri na yanatumiwa hadi leo hii.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kwa mazungumzo kuhusu vijiji vya wafungwa huko Botany Bay, tafadhali ona gazeti la Amkeni! la Februari 8, 2001, ukurasa wa 20.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

SIMULIZI LA MTU ALIYEZALIWA KATIKA UKOO WA WAFUNGWA

Mtu mmoja ambaye babu zake wa kale walikuwa wafungwa asimulia jinsi babu yake mmoja wa kale alivyoenda huko Australia. Anaeleza hivi:

“Alipokuwa na umri wa miaka 19, mmoja wa babu zangu wa kale alihukumiwa . . . kwa kuiba kibeti. Aliondoka Uingereza mnamo Desemba 12, 1834, akiwa kwenye meli iliyoitwa George III ambayo ilikuwa na abiria 308—wakiwemo wafungwa 220. Kufikia wakati ambapo meli hiyo ilifika karibu na pwani ya Tasmania mnamo Aprili 12, 1835, wafungwa 50 walikuwa wanaugua kiseyeye. Mke wa askari, watoto 3, na watu wengine 12 walikuwa wamekufa. Watoto wawili walizaliwa wakati wa safari hiyo ndefu.

“Baada ya kusafiri kwa majuma sita, meli hiyo ilishika moto. Lakini wafungwa wawili wajasiri waliondosha hatari hiyo kwa kuzuia mapipa mawili yenye baruti kutoshika moto. Hata hivyo, vitu vingi viliungua, na hiyo ikasababisha upungufu wa chakula na mahitaji mengine ya safari hiyo. Ili kufika haraka bandarini, nahodha aliamua kupita njia ya mkato kwenye Mlango-Bahari wa D’Entrecasteaux, kwenye ukingo wa kusini wa Tasmania. Saa 3:30 usiku, meli hiyo iligonga mwamba pasipo kutazamia, kilometa tano tu kutoka ufukoni na kuzama. Leo mwamba huo unaitwa Mwamba wa Mfalme George. Wengi wa wale watu 133 waliokufa maji walikuwa wafungwa waliokuwa wamefungiwa katika sehemu za chini za meli. Ni wafungwa 81 tu kati ya wale wafungwa 220 waliookoka. Babu yangu alikuwa mmoja wao. Mnamo mwaka wa 1843, alioa mwanamke ambaye aliachiliwa kutoka gerezani, na miaka miwili baadaye alisamehewa makosa yake. Alikufa mwaka wa 1895.”

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

BW. THOMAS BRISBANE

GAVANA LACHLAN MACQUARIE

Meli ya wafungwa ya Uingereza iliyoitwa “Amphitrite”

[Hisani]

Wafungwa: By Courtesy of National Library of Australia; F. Schenck’s Portrait of Sir Thomas Brisbane: Rex Nan Kivell Collection, NK 1154. By permission of the National Library of Australia; Macquarie: Mitchell Library, State Library of New South Wales; ship: La Trobe Picture Collection, State Library of Victoria

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Gereza la wafungwa la Port Arthur

[Hisani]

Minyororo na gereza: La Trobe Picture Collection, State Library of Victoria

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mnara huu wa taa kwenye Bandari ya Sydney unafanana na mnara uliochorwa na Francis Greenway, ambaye hapo awali alikuwa mfungwa

[Picha katika ukurasa wa 15]

Pwani ya Kisiwa cha Norfolk ambayo haiwezi kupitika

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kambi ya kale ya jeshi kwenye Kisiwa cha Norfolk