Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vijana Wanaosinzia—Je, Hilo Ni Jambo la Kuhangaisha?

Vijana Wanaosinzia—Je, Hilo Ni Jambo la Kuhangaisha?

Vijana Wanaosinzia—Je, Hilo Ni Jambo la Kuhangaisha?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

GAZETI la Globe and Mail la Kanada linasema kwamba kutolala hupunguza uwezo wa kufikiri na uwezo wa kukumbuka mambo, na wanafunzi wanaobalehe ndio wanaoweza kuathiriwa zaidi. “Kutolala kwaweza kuwafanya watoto na vijana wanaobalehe wawe na tabia zisizofaa, kukasirika haraka na kuwa machachari mno.” Wanasayansi walifanya utafiti kuhusu mazoea ya kulala ya wanafunzi wa sekondari wapatao 2,200 na wakagundua kwamba karibu asilimia 47 kati yao hawakulala kwa muda wa saa nane kama inavyopendekezwa.

Gazeti la Globe linasema kwamba ijapokuwa mara nyingi mtindo wa maisha wa vijana huwafanya wasilale vya kutosha, ‘huenda ikawa wengine wao pia wana magonjwa ambayo hayajatambuliwa. Asilimia 4 ya watoto walio kati ya umri wa miaka 4 na 18 huacha kupumua kwa muda mfupi wakati wanapolala.’ Wakati watoto hao wanapolala, kijia cha hewa kilichoko nyuma ya koo hujifunga kabisa au kwa kadiri, na hivyo kuzuia oksijeni isipite. Kwa hiyo, ubongo haupumziki vya kutosha, na ndiyo sababu watoto hao huamka wakiwa wamechoka au wakiwa wamekasirika.

Dalili zinazoonyesha kwamba huenda ikawa mtoto ana tatizo la kulala zinatia ndani kukoroma kwa sauti kubwa au kwa kutoa sauti kama ya filimbi wakati anapolala, kuumwa na kichwa mara kwa mara asubuhi, kusahau mambo na kutoweza kukaza fikira, na vilevile kusinzia-sinzia sana mchana. Wazazi wanahimizwa wasikilize mara kwa mara wakati watoto wao wanapolala fofofo. Dakt. Robert Brouillette, mtaalamu wa matatizo ya kulala ya watoto kwenye Hospitali ya Watoto ya Montreal, anasema kwamba mtoto mwenye tatizo hilo anaweza kuacha kupumua anapolala, hata wakati kifua chake kinapokuwa kikisonga juu na chini. “Mtoto huanza kupumua tena wakati anapoamka kabisa au anapoamka kidogo [na] kuvuta pumzi mara chache kabla ya kulala tena.” Jambo hilo linaweza kutokea mara nyingi sana kila usiku, na kumfanya mtoto aamke akiwa amechoka.

Shirika la Marekani la Matatizo ya Kulala linapendekeza kwamba mtu alale katika chumba chenye giza ambacho hakina joto wala vitu vya kukengeusha akili kama vile televisheni au kompyuta. Pia, kuwa na saa hususa za kulala na kuamka kutawasaidia watoto na vijana kulala vya kutosha. Watu fulani ambao huacha kupumua kwa muda mfupi wakati wanapolala hutumia mashine ya kusukuma hewa ambayo hupuliza hewa polepole kupitia puani na mdomoni ili kufungua sehemu ya nyuma ya koo. Daktari mmoja wa watoto alisema hivi: “Kulala ni muhimu kuliko chakula tunachokula. Ni muhimu kuliko kufanya mazoezi. Kulala huongoza homoni zetu, hisia zetu na mfumo wetu wa kinga.”