Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuna Jani Katika Utando wa Buibui!

Kuna Jani Katika Utando wa Buibui!

Kuna Jani Katika Utando wa Buibui!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

JE, UNAONA jani hili kavu lililokunjwa sana? Jani hilo limening’inia katika utando wa buibui. Unapolitazama kwa mara ya kwanza, utafikiri lilipeperushwa na upepo hadi hapo. Lakini kuna jambo la kipekee kuhusu jani hilo.

Kile unachoona ni makao ya kipekee ya buibui anayekunja majani—kiumbe wa ajabu sana. Yeye ndiye buibui mmoja tu anayejulikana kwa kukunja jani na kulitumia kujitengenezea makao. Yeye hutumia hariri kufunika sehemu ya ndani ya jani hilo kama tu anavyoitumia kutengenezea utando. Lakini je, jani hilo hupeperushwa tu kwa ghafula hadi kwenye utando huo? Huenda ikaonekana kuwa hivyo. Lakini uchunguzi wa karibu unaonyesha kwamba ubuni fulani unahusika. Buibui huyo huchagua jani moja kwa makini, labda kutoka kwenye majani yaliyoanguka chini ya mti. Baada ya kulikunja na kulizungusha, buibui hulifunga kwa nyuzi za hariri ili lisikunjuke.

Hata hivyo, si lazima buibui huyo atumie jani kutengeneza makao. Katika maeneo yaliyo nje kidogo ya jiji, wao hutumia magazeti ya zamani, kipande cha karatasi ngumu, au tiketi zilizotupwa. Kwa kushangaza, huenda hata wakachagua kutumia koa la konokono. Kwa mfano, buibui mmoja alibeba koa lililozidi uzito wake mara sita, kisha akaishi ndani ya koa hilo!

Hebu tuone kama buibui yuko katika jani lake sasa. Tunalitikisa jani kidogo. Ndiye huyo! Umemwona? Buibui mdogo, mwenye rangi maridadi anatoka nje ya jani na kuteremka chini kupitia kamba yake ya hariri. Usiogope! Tu salama. Buibui huyo si hatari, ingawa anaweza kukuuma kidole ukimshika vibaya.

Wakati wa mchana, buibui huyo hupumzika ndani ya jani lake. Lakini usiku, wakati wadudu wengi wanapotembea-tembea, utamwona amengojea mlangoni mwa jani lake. Akiwa hapo, yeye huwekelea mguu wake kwenye uzi mmoja wa hariri unaotoka ndani ya jani hadi katikati ya utando. Mdudu yeyote akigonga utando huo, buibui atasikia na kumrukia mara moja, amlemaze, na kisha amle.

Mjenzi huyo mdogo mwenye ustadi ni mmojawapo wa viumbe wengi wa kuvutia katika msitu wa Australia.