Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ushindi wa Nyanya!

Ushindi wa Nyanya!

Ushindi wa Nyanya!

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hispania

KARNE nyingi zilizopita mmea usiopendeza wa nyanya ulimea katika eneo la Andes huko Amerika Kusini. Matunda yake yalikuwa matamu sana, lakini Wahindi wenyeji hawakuupanda. Kwa njia fulani, mmea huo wa pekee ulipelekwa Mexico, ambako Waazteki waliuita xitomatl. Neno tomatl lilitumiwa kwa ajili ya matunda kadhaa yaliyofanana na nyanya, hasa matunda yenye umajimaji mwingi. Punde si punde, Waazteki wakaanza kutumia mchuzi wa nyanya katika mapishi yao, na hatimaye mmea wa nyanya ukaanza kujulikana ulimwenguni pote.

Wahispania waliokuwa watekaji walipenda mchuzi wa nyanya pia. Mnamo mwaka wa 1590, kasisi mmoja Myeswiti aliyeishi Mexico kwa miaka mingi alisifu nyanya sana na kusema kwamba tunda hilo lilikuwa lenye lishe bora na lenye maji mengi ambayo yanafanya mchuzi uwe na ladha tamu. Wahispania waliokuwa Mexico walituma mbegu za nyanya huko Hispania na katika makoloni yao huko Karibea na Ufilipino. Hata hivyo, licha ya jitihada hizo zote, ilichukua zaidi ya karne tatu kabla ya nyanya kuanza kutumiwa kwa mapishi ulimwenguni pote.

Kushinda Maoni Yasiyofaa

Kama kawaida, ni vigumu sana watu waanze kupenda chakula ambacho hawajawahi kula. Licha ya sifa yake huko Mexico, tunda la nyanya lilichukiwa sana huko Ulaya. Tatizo lilianza wakati wataalamu wa mimea huko Ulaya walipoorodhesha nyanya katika jamii ya Solanaceae, jamii moja na mbeladona wenye sumu. Isitoshe, majani yake yalitoa harufu kali, na yalikuwa na sumu. Na zaidi ya hilo, waganga wa miti-shamba walidai kwamba tunda la nyanya lilikuwa na nguvu za kuamsha tamaa ya ngono. Watu wengine huamini kwamba hiyo ndiyo sababu Wafaransa waliliita pomme d’amour, yaani, “tofaa la mapenzi.”

Maoni yasiyofaa kuhusu nyanya yalienea pia hadi Amerika Kaskazini. Mwishoni mwa miaka ya 1820, mkulima mmoja Mmarekani kutoka Massachusetts alisema hivi: “[Manyanya] yalionekana kuwa yenye kuchukiza sana hivi kwamba nilifikiri ningeyala tu nikiwa na njaa kali sana.” Si yeye tu aliyeyatilia shaka. Mwanamume mmoja kutoka Pennsylvania aliyaita “takataka chungu,” naye mkulima mmoja Mwingereza alifafanua mnyanya kuwa “tofaa la dhahabu linalonuka.”

Jambo la kupendeza ni kwamba Waitaliano, ambao katika karne ya 16 waliliita nyanya pomodoro, yaani tofaa la dhahabu, walikuwa na maoni yanayofaa. * Kufikia mwanzoni mwa karne ya 17, manyanya yalikuwa yameanza kuliwa nchini Italia ambako yalisitawi vizuri kwa sababu ya hali nzuri yenye joto. Hata hivyo, kwa karibu karne mbili hivi, wakulima huko kaskazini mwa Ulaya waliendelea kutilia shaka nyanya, na hivyo walizipanda kwa ajili ya kurembesha au kwa matibabu.

Kutopendwa Hadi Kupendwa Zaidi

Mara tu watu walipoanza kula manyanya, mashaka yoyote waliyokuwa nayo hapo awali yalitoweka na ukuzaji wa nyanya ukaanza kusitawi. Kufikia miaka ya 1870, kwa kutumia njia ya usafiri ya reli, manyanya kutoka California yaliuzwa huko New York. Miaka michache kabla ya wakati huo, mahali pa kwanza pa kutengenezea na kuuza piza palifunguliwa huko Naples, Italia, hivyo kukawa na uhitaji mkubwa wa nyanya. Katika karne ya 20, mbali na kutumiwa katika piza inayopendwa sana, maji ya nyanya, mchuzi wake, na rojo yake imependwa sana hivi kwamba sasa nyanya ni tunda linalopendwa zaidi duniani. (Ona sanduku.) Zaidi ya kuwafanikisha wafanyabiashara, tunda la nyanya limependwa sana na wakulima wa mabustani toka majangwa ya Mashariki ya Kati hata kufikia sehemu kame za Bahari ya Kaskazini.

Kutoka Jangwani Hadi Kwenye Maeneo ya Mafuta

Vyombo vya mafuta vilivyomo katikati ya Bahari ya Kaskazini huenda visiwe mahali panapofaa kupanda matunda na mboga, lakini mmea wa nyanya hauhitaji uangalifu mwingi. Mbegu zake zaweza kusitawi bila udongo zikitiwa ndani ya mfuko wa plastiki ulio na virutubishi vyote vinavyohitajiwa na maji ya kutosha. Hilo lilisababisha kusitawi kwa nyanya katika eneo hilo la wachimba-mafuta ambao hupenda kuona mboga na matunda yakisitawi miongoni mwa mabomba ya mafuta na mashine zisizo na uhai na vilevile kufurahia matunda yaliyopandwa nyumbani ili kuboresha vyakula vyao.

Yakitunzwa vizuri, manyanya yaweza kusitawi jangwani. Kule Misri, Wabedui wa Jabaliyyah waliotawanyika miongoni mwa milima ya Sinai, wamelima mabustani yenye mitaro yanayopata maji kutoka kwenye vijito, visima na wakati mwingine mvua inayonyesha mara moja-moja. Mabustani yao yaliyonyunyiziwa maji kwa uangalifu huzaa manyanya makubwa-makubwa ambayo hukaushwa kwenye jua ili kuhifadhiwa kwa ajili ya majira ya baridi kali.

Hata hivyo kupandwa kwa nyanya karibu ulimwenguni pote, hakutegemei tu uwezo wake wa kumea katika aina mbalimbali za udongo wala tabia ya nchi. Mimea ya nyanya hujichavusha yenyewe, hivyo aina mbalimbali za nyanya zaweza kuzalishwa kulingana na mapendezi mbalimbali. Sasa wakulima wanaweza kuchagua miongoni mwa karibu aina 4,000 zilizopo. Manyanya madogo mekundu yaliyo na maji mengi huongeza rangi na ladha kwa saladi, na yale matamu yenye umbo la yai mara nyingi hutiwa makoponi. Nayo yale manyanya makubwa yenye nyama nyingi, yanayotumiwa sana katika mapishi ya Wahispania, ni bora kwa kachumbari na katika mapishi.

Hata hivyo, tunda la nyanya lilikuja kupendwa kwa sababu ya ladha yake iwezayo kuongeza utamu katika piza, kufanya kachumbari ivutie, kuongeza utamu kwenye mchuzi, au kuboresha maji matamu. Ijapokuwa halikuthibitika kuwa “tofaa la mapenzi,” sasa tunda la nyanya linapendwa ulimwenguni pote.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Inadhaniwa kwamba manyanya yalipewa jina hilo kwa sababu aina za kwanza za nyanya zilizopandwa na Waitaliano zilikuwa na rangi ya manjano.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

Gazpacho—Ladha Yenye Kuburudisha ya Nyanya

Ungependa kuonja mchuzi baridi wenye kuburudisha wakati wa joto jingi? Katika eneo la Andalusia huko Hispania, mchuzi wa gazpacho hutumiwa karibu kila siku pamoja na mlo mkuu. Ni rahisi kuutengeneza, kwani unahitaji viungo vinavyopatikana kwa urahisi, nao utaipatia familia yako hamu ya kula. Yafuatayo ni maelezo ya jinsi Wahispania wanavyotengeneza mchuzi wa gazpacho wa watu watano.

Viungo

gramu 600 za manyanya mabivu

gramu 350 za matango

gramu 250 za pilipili hoho nyekundu

vipande viwili vya mkate uliokaushwa (gramu 60)

mililita 30 za siki

mililita 30 za mafuta ya zeituni

chumvi

kidole kimoja cha kitunguu saumu

kiasi kidogo cha jira

Matayarisho Osha na uondoe mbegu za pilipili hoho, ondoa ngozi ya matango, na ya nyanya. Kisha katakata viungo hivyo vipande-vipande. Vitie ndani ya bakuli lenye lita moja ya maji (yanayotosha kuzifunika kabisa), tia ndani mkate, kitunguu saumu, vikolezo, siki, na mafuta. Acha mchuzi huo usiku kucha, kisha siku ifuatayo usage mchanganyiko huo na kuuchuja. Ikihitajika, unaweza kuongeza vikolezo. Itie supu ya gazpacho kwenye friji hadi wakati wa mlo. Gazpacho yaweza kupakuliwa pamoja na manyanya yaliyokatwa-katwa vipande vidogo-vidogo, matango, na pilipili hoho.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Ukweli Kuhusu Nyanya

Sasa nyanya huzalishwa sana ulimwenguni. Kila mwaka, karibu tani milioni 100 huvunwa. Idadi hiyo ni zaidi ya mavuno ya matunda mengine makuu ulimwenguni (kama vile matofaa, ndizi, zabibu, na machungwa).

Ijapokuwa mara nyingi nyanya huitwa mboga, kulingana na elimu ya mimea nyanya ni tunda. Hiyo ni kwa sababu sehemu yenye mbegu ndiyo huliwa (kwa kawaida sehemu za mboga zinazoliwa ni shina, majani, na mizizi).

Kulingana na kitabu cha The Guinness Book of Records, tunda kubwa zaidi la nyanya kuwahi kurekodiwa lilipandwa huko Oklahoma, Marekani, nalo lilikuwa na uzito wa kilogramu 3.5.

Kuvuta sigara karibu na mimea ya nyanya au kabla ya kuishika kwaweza kudhuru mimea hiyo. Sigara ina virusi ambavyo huathiri mmea wa nyanya.

Mbali na kuwa na vitamini A na C, tunda la nyanya lina rangi ya asili inayoitwa lycopene ambayo huzuia kuharibiwa kwa chembe kwa sababu ya oksijeni nyingi. Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kwamba chakula kilicho na manyanya mengi huenda kikapunguza hatari ya kupata kansa.