Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kasuku Wamo Hatarini

Kasuku Wamo Hatarini

Kasuku Wamo Hatarini

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Uingereza

Dakt. Timothy Wright wa Chuo Kikuu cha Maryland, Marekani, anasema kwamba kasuku ni “kati ya ndege walio katika hatari kubwa zaidi ya kutoweka duniani.” Kwa kusikitisha, manyoya yao yenye rangi nyangavu na uwezo wao wa kustaajabisha wa kuiga sauti ya wanadamu huwafanya wawe katika hatari ya kutoweka.

Daktari mmoja Mgiriki wa karne ya tano K.W.K. ndiye anayejulikana kuwa aliandika habari ya kwanza kabisa kumhusu kasuku mmoja aliyefugwa. Alistaajabu wakati ndege huyo alipoanza kusema maneno ya Kigiriki na vilevile maneno kadhaa ya lugha moja ya India, nchi ambayo kasuku huyo alitoka.

Leo, watu huvutiwa na uwezo wa kasuku wa kuiga maneno na ndiyo sababu wengi hupenda kuwafuga. Jambo hilo pia limefanya biashara haramu ya kuuza kasuku isitawi sana. Uchunguzi mbalimbali uliofanywa kwa muda wa miaka 20 iliyopita umeonyesha kwamba wawindaji-haramu wameharibu asilimia 30 ya viota vya aina 21 za kasuku ambazo zinapatikana katika nchi 14. Pia, wameharibu asilimia 70 ya viota vya aina 4 za kasuku. Bei ya ndege hao imepanda sana kwa sababu makao yao ya asili yameharibiwa na hawaongezeki kwa wingi kwa sababu wao hutaga mayai mara moja kwa mwaka. Kasuku wasiopatikana kwa urahisi huuzwa bei ghali zaidi.

Ripoti zinaonyesha kwamba aina fulani za ndege hao zimo katika hatari kubwa ya kutoweka kwa kuwa idadi yao imepungua sana. Inakadiriwa kwamba huko Brazili, kasuku aina ya Lear’s macaw hawazidi 200. Idadi ya kasuku wa Puerto Riko imepungua hata zaidi, kwani idadi yao msituni haizidi 50. Inadhaniwa kwamba kasuku aina ya Spix’s macaw ametoweka kabisa. Kuhifadhiwa kwa ndege huyo kunategemea mbinu ya kufuga na kuzalisha.

Maadamu ndege hao wenye kupendeza sana wangalipo, wataendelea kuonyesha kwamba kuna Muumba, ambaye pasipo shaka anafurahia sura yao yenye kuvutia na uwezo wao wa kustaajabisha. Je, wanadamu wenye pupa watawamaliza kasuku kabisa? Tutaona. Kwa sasa, kasuku wangali hatarini.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Kasuku wa Puerto Riko

“Spix’s macaw”

“Lear’s macaw”

[Hisani]

Kasuku wa Puerto Riko: U.S. Geological Survey/Photo by James W. Wiley; Kasuku aina ya Lear’s macaw: © Kjell B. Sandved/Visuals Unlimited; Kasuku aina ya Spix’s macaw: Progenies of and courtesy of Birds International, Inc.