Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dubu-Jike Hulala Fofofo Wakati wa Majira ya Baridi Kali

Dubu-Jike Hulala Fofofo Wakati wa Majira ya Baridi Kali

Dubu-Jike Hulala Fofofo Wakati wa Majira ya Baridi Kali

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

NDEGE wanaohama huashiria kwa wakati ufaao kukaribia kwa majira ya kupukutika kwa majani upande wa Kaskazini. Ili kuepuka baridi kali, makundi maridadi ya kwezi na korongo wanaopaa angani kwa mpangilio huelekea upande wa kusini. Wakati huohuo, dubu wa Ulaya (European brown bear) anakabili tatizo hilohilo—Atakula nini majani yatakaponyauka, na ardhi itakapoganda na kufunikwa kabisa kwa theluji? Ni rahisi kwa ndege kutoroka hatari hiyo, lakini dubu huyo hawezi kukimbia kupitia msituni na jangwani na kuhamia maeneo yenye joto.

Yeye hujiokoa kwa njia nzuri sana. Dubu huyo hula chakula kingi wakati wa majira ya joto kisha hulala usingizi hadi majira ya baridi yanapokwisha. Lakini hilo si jambo rahisi hata kidogo. Hebu wazia jinsi afya yako inavyoweza kudhoofika ukikosa kula au kunywa kwa muda wa miezi sita. Hebu tuchunguze hatua mbalimbali zenye kustaajabisha za usingizi wa dubu-jike wakati wa majira ya baridi kali.

Hufanya Kazi Nyingi Majira ya Joto

Ni lazima dubu-jike ahifadhi mafuta mengi mwilini mwake mapema ili aishi bila chakula kwa miezi kadhaa. Kwa hiyo, hana wasiwasi kuhusu umbo la mwili wake. Lengo lake kuu ni kuhifadhi mafuta mengi mwilini mwake, naye huhifadhi mafuta yenye unene wa sentimeta nane katika sehemu fulani mwilini. Yeye hula kitu chochote ingawa anapenda sana beri zenye sukari nyingi. Yeye hula mizizi, wanyama wadogo, samaki, na chungu. Hatimaye, uzito wake huongezeka kutoka kilogramu 130 hadi kilogramu 160, na thuluthi moja ya uzito huo ni mafuta (wakati huo, dubu-dume anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 300 hivi). Kabla ya kwenda katika makao yake ili kulala fofofo, yeye huacha kula kisha huenda haja kubwa. Hali, hakojoi wala kwenda haja kubwa kwa muda wa miezi sita.

Dubu anaweza kulala pangoni, katika kichuguu kilichoachwa, au katika tundu lililo kwenye mizizi ya miti, maadamu mahali penyewe ni patulivu—kwa sababu hakuna anayependa kusumbuliwa akiwa usingizini. Dubu hukusanya matawi ya msonobari, kuvumwani, majani, na vifaa vingine laini na kuvitia pangoni ili liwe lenye kustarehesha. Dubu huyo mkubwa anatoshea barabara pangoni. Majira ya baridi kali yanapoanza, pango litafunikwa kabisa kwa theluji, lakini kutabaki shimo dogo tu ambalo haliwezi kuonekana kwa urahisi.

Kipindi cha Usingizi

Wanyama fulani wadogo kama vile nungunungu, popo, na panya-miti, hulala kabisa kana kwamba ni wafu katika majira ya baridi kali, miili yao huwa baridi kama mazingira. Hata hivyo, joto la mwili wa dubu hupungua kwa karibu nyuzi Selsiasi 5 tu, na hivyo hawalali usingizi mzito sana. “Dubu hapotezi kabisa fahamu wakati huo. Hunyanyua kichwa chake na kujipindua kila siku,” aeleza Profesa Raimo Hissa, ambaye amefanya uchunguzi kwa miaka mingi kwenye Chuo Kikuu cha Oulu, Finland, kuhusu usingizi wa dubu wakati wa majira ya baridi kali. Lakini si rahisi kumwona dubu akitoka pangoni wakati majira ya baridi kali yanapoendelea.

Dubu anapolala wakati wa majira ya baridi kali, utendaji wa mwili wake hupungua kabisa. Mapigo ya moyo wake hayazidi kumi kwa dakika moja, na utengenezaji wa kemikali mwilini hupungua. Dubu-jike anapolala fofofo, mafuta yaliyo mwilini mwake huanza kutumika wakati huo muhimu sana. Mafuta hayo huyeyushwa na kutokeza joto na maji yanayohitajiwa mwilini. Uyeyushaji huo wa mafuta unatokeza kiasi fulani cha taka licha ya kwamba utendaji wa mwili umepungua. Ataondoaje taka hizo mwilini bila kuchafua pango lake? Mwili wa dubu unazichuja taka hizo badala ya kuziondoa.

Profesa Hissa aeleza: “Kemikali za nitrojeni zilizo kwenye taka hufyonzwa tena kutoka kwenye mafigo na kibofu kisha husafirishwa kupitia damu hadi tumboni, ambamo bakteria hubadili mkojo kuwa amonia.” Jambo la kustaajabisha hata zaidi ni kwamba amonia hiyo inarudishwa kwenye ini, ambako inatumiwa kufanyiza asidi-amino mpya, msingi wa protini. Kwa hiyo mwili wa dubu hupata lishe kwa kubadili taka kuwa protini muda wote anapolala usingizi pangoni!

Hapo zamani, watu walizoea kuwinda dubu mapangoni. Bila shaka, ilikuwa rahisi kumwinda dubu anayesinzia. Kwanza, watu wanaoteleza kwenye theluji walitafuta pango lenye dubu na kulizingira. Halafu walimwamsha dubu na kumuua. Siku hizi ni marufuku kuwawinda dubu wakati wa majira ya baridi kali barani Ulaya kwa sababu kufanya hivyo kunaonwa kuwa ukatili.

Maisha Mapya

Dubu-dume hupumzika na kujipindua-pindua kwa urahisi majira yote ya baridi kali, lakini dubu-jike huwa na shughuli nyingine. Dubu hujamiiana mapema wakati wa kiangazi, lakini mayai yaliyotungishwa mimba tumboni mwa dubu-jike huanza kukua anapolala usingizi wakati wa majira ya baridi kali. Kisha, viini-tete hujipandikiza kwenye tumbo la uzazi na kuanza kukua. Baada ya miezi miwili tu, joto la mwili wa dubu-jike huongezeka kidogo mnamo mwezi wa Desemba au Januari, kisha anazaa watoto wawili au watatu. Joto la mwili wake hushuka kidogo baada ya kuzaa, lakini si kufikia kiwango kilichokuwapo kabla ya kuzaa. Dubu-dume hayupo wakati watoto wanapozaliwa, lakini hata kama angekuwapo, hangestaajabishwa na tukio hilo. Huenda dubu huyo mkubwa asiweze kuwatambua watoto wake walio dhaifu mno, wenye uzito usiozidi gramu 350.

Dubu-jike huwanyonyesha watoto wake wachanga maziwa yenye lishe sana, na hilo humfanya awe dhaifu zaidi. Watoto wake hukua haraka sana, na kufikia wakati wa majira ya kuchipua, watoto hao wenye manyoya huwa na uzito wa kilogramu 5 hivi. Wao hucheza-cheza pangoni.

Majira ya Kuchipua

Mwezi wa Machi umeanza. Majira ya baridi kali yamekwisha, theluji inayeyuka, na ndege wanarudi kutoka upande wa kusini. Mwishoni mwa mwezi, dubu-madume hutoka polepole mapangoni. Hata hivyo, dubu-majike hupumzika mapangoni kwa majuma mengine kadhaa; huenda ni kwa sababu wamedhoofika baada ya kuwatunza watoto.

Baada ya kipindi hicho kirefu cha usingizi, dubu-jike huwa amekonda mno tofauti na vile alivyokuwa mkubwa wakati wa majira ya kupukutika kwa majani. Mafuta yaliyokuwa yamejaa mwilini mwake yamekwisha. Lakini ana afya nzuri kabisa—hana vidonda vya malazi, misuli yake si mikakamavu, wala hana ugonjwa wa mifupa. Anatoka pangoni na punde si punde anakunya shonde la mavi magumu. Kwa kawaida, dubu huanza kula baada ya majuma mawili au matatu hivi, kwa kuwa mwili hurudia hali yake ya kawaida baada ya muda fulani. Wakati huo dubu huhisi njaa kali ajabu. Hata hivyo, wakati huo ndipo tu mimea imeanza kuchipuka kwa hivyo hakuna chakula cha kutosha mwituni. Wakati huo, dubu hula mabuu na mbawakawa, hutafuna mizoga, na huenda hata akawinda mbawala.

Kwa kawaida, dubu-jike ndiye anayewatunza na kuwazoeza watoto wake, anaowapenda mno ajabu. Mithali moja ya kale yasema: “Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake, kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.” (Mithali 17:12) Yaani, hakuna mtu angependa kukutana na dubu huyo au mtu mpumbavu. Hissa asema, “Dubu-jike huwatunza mno watoto wake. Dubu-dume anapokaribia, dubu-jike huwapandisha watoto wake mara moja mtini, kwa sababu dubu-dume anaweza kuwadhuru ajapokuwa baba yao.”

Dubu-jike huandamana na watoto wake pangoni majira yafuatayo ya baridi kali. Mwaka unaofuata, watoto hao waliokomaa watahitaji kutafuta mapango mengine, kwani utakuwa wakati wa dubu-jike kuzaa watoto wengine.

Wanasayansi wamejifunza mengi kuhusu usingizi wenye kustaajabisha wa dubu wakati wa majira ya baridi kali, lakini kuna mambo mengi ambayo bado hatujui. Kwa nini dubu hushikwa na usingizi mzito na kukosa hamu ya kula kabla majira ya baridi kali hayajaanza? Mbona hapati ugonjwa wa mifupa? Si rahisi kujua tabia zote za dubu, lakini hilo halitushangazi kwa sababu kila mtu ana haki ya kuficha siri zake!

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

Utafiti Kuhusu Usingizi wa Dubu Wakati wa Majira ya Baridi Kali

Idara ya Elimu ya Wanyama katika Chuo Kikuu cha Oulu imefanya utafiti kwa miaka kadhaa kuhusu hali ya miili ya wanyama kujipatanisha na majira ya baridi kali. Dubu wa Ulaya alianza kuchunguzwa mwaka wa 1988, na kwa ujumla, dubu 20 wamechunguzwa tangu wakati huo. Pango maalumu la utafiti lilitayarishwa katika bustani ya wanyama chuoni humo. Kompyuta, utafiti wa maabara, na kamera ya video zimetumiwa kupima halijoto ya miili yao, ujenzi na uvunjaji wa kemikali mwilini, utendaji, na pia mabadiliko ya damu na ya kemikali yanayotukia mwilini mwa dubu, wanapolala usingizi wakati wa majira ya baridi kali. Chuo hicho kimeshirikiana na vyuo vikuu katika nchi nyingine hata nchi za mbali sana kama Japan. Watafiti hao wanatumaini kwamba matokeo ya utafiti huo yataandaa habari ambazo huenda hata zikawasaidia kutatua matatizo ya utendaji wa miili ya wanadamu.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Pango la dubu-jike

[Picha katika ukurasa wa 18]

Beri zenye sukari nyingi