Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukutana na Mwindaji Anayenyemelea Ghafla

Kukutana na Mwindaji Anayenyemelea Ghafla

Kukutana na Mwindaji Anayenyemelea Ghafla

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

“TAZAMA! Pale uwanjani,” nilinong’oneza kwa furaha. Mimi na mke wangu tulikuwa tukisafiri kwa mashua katika Mto mkubwa wa Nechako, katikati ya British Columbia, tukifurahia mandhari na sauti nzuri za mwituni. Ghafla, mnyama fulani alitokea amrukie sungura asiye na tahadhari. Mara, sungura alitoweka. Mwindaji huyo alipotuona, alisimama kwa muda mfupi. Alitutazama kwa hasira na kunguruma kana kwamba alitaka kusema: ‘Asanteni kwa kuninyang’anya kiamsha kinywa changu,’ naye akatoweka kwenye giza kichakani. Mke wangu aliniuliza: “Ni mnyama gani huyo? “Simba-mangu,” nilijibu. Wakati huohuo tukasikia mngurumo mwingine wenye kuogopesha, sasa ulikuwa mkubwa zaidi na wa muda mrefu. Ilikuwa asubuhi na mapema.

Haonekani Mara Nyingi

Hilo halikuwa tukio la kawaida. Wakati mmoja simba-mangu waliishi kotekote katika misitu na milima ya sehemu ya Kaskazini ya Dunia, lakini leo wanapatikana tu katika maeneo machache ya mbali. Simba-mangu fulani wameonekana katika maeneo ya mbali sana ya milimani ya Ulaya na Asia kwenye milima ya Hispania upande wa kusini. Hata hivyo, simba-mangu wengi wanapatikana Siberia na katika misitu mikubwa ya Kanada na Alaska. Kitabu kimoja kuhusu paka wa mwitu kinasema: “Ili waishi vizuri simba-mangu wanahitaji aina mbili za misitu: misitu yenye miti iliyosongamana iliyojipinda na kukomaa ili wawe na makao na mahali pa kuzalia, na uwanja wenye nyasi na miti michanga ambapo wanaweza kuwinda sungura.”

Simba-mangu wengine waliokomaa wana ukubwa kama wa paka sita wakubwa wa nyumbani na kimo chao kinafikia mapajani mwa mtu mzima. Simba-mangu wa kiume wa Amerika Kaskazini ana uzito wa kati ya kilogramu 10 na 15, na wa kike kilogramu 5 hadi 10. Ukubwa wake ni nusu ya simba-mangu wa Ulaya. Baadhi yao wanaweza kuwa na urefu wa meta moja.

Baadhi ya mambo yanayomtambulisha simba-mangu ni manyoya yaliyo katika shavu lake ambayo humtofautisha na paka wengine. Uso wake ni mpana na mfupi kuliko wa paka wengine, nao humfanya aonekane kama ana haya na ni mpole. Katika majira ya baridi kali manyoya ya simba-mangu wa Amerika Kaskazini huwa mengi na yenye urefu wa sentimeta 10 na kwa kawaida ni yenye rangi ya kijivu-nyangavu na madoa ya kijivu-meusi usoni. Simba-mangu wa Ulaya na Asia huwa na rangi ya kahawia-nyangavu na madoa ya kahawia-nyeusi. Pia, wanatambuliwa kwa mkia wao mfupi mnene wenye ncha nyeusi, na huo ni wenye urefu wa sentimeta kumi. Masikio yake makubwa yana umbo la pembe tatu na manyoya meusi nchani. Manyoya hayo humsaidia kutambua upande ambao sauti ya windo lake hutoka.

Mwindaji huyo hupenda kuwinda peke yake na hufaulu kushika windo lake kwa sababu ya kulenga kwa usahihi na kujificha. Kwa sababu ya nyayo zake pana na laini zenye kucha zinazoweza kukunjwa anaweza kukimbia juu ya theluji. Miguu yake mirefu na yenye nguvu ya nyuma humwezesha simba-mangu kutimua na kuruka meta mbili hadi tatu. Pia anaweza kugeuka akiwa hewani anapofukuza windo. Hata hivyo, yeye hufukuza windo lake kwa muda mfupi tu. Simba-mangu anapokosa kumkamata mnyama anayemfukuza baada ya kuruka mara tano, yeye hukata tamaa. Hivyo, itambidi mara nyingi kufukuza sungura watatu hadi kumi ili akamate mmoja. Asipofaulu hatakula. Anapokamata windo, simba-mangu hutumia utaya wake wenye nguvu—ulio na meno 28, na 4 ni marefu na yenye ncha kali—kumwuma shingoni.

Kwa kawaida yeye huwinda kabla tu ya mapambazuko na baada tu ya machweo. Kama paka wengine, simba-mangu anaweza kuona kukiwa na mwangaza kidogo. Ana uwezo wa kuona katika giza, ambao ni mwangaza kidogo sana ya ule anaohitaji binadamu. Paka huyo ana utando katika jicho lake ambao hurudisha nuru kwenye sehemu ya jicho inayopokea nuru na kufanya jicho lake kung’aa kama marumaru gizani. Kitabu kimoja kuhusu paka wa mwituni kinasema: ‘Simba-mangu huona windo lake akiwa mbali sana. Inasemekana kwamba anaweza kumuona panya akiwa umbali wa meta 75, na sungura akiwa umbali wa meta 300.’

Huko Kanada simba-mangu anapenda sana kula sungura aina ya snowshoe, naye hushika wastani wa sungura wawili kila siku tatu. Simba-mangu aliyelishwa vizuri anaweza kuishi kwa miaka 15. Akiwa mwindaji anayeweza kubadilika kulingana na hali, yeye pia hula panya, panya wa majini, kwale wa Ulaya, bata, panya-buku, na kindi. Pia kuna taarifa zinazoonyesha kwamba simba-mangu anaweza kumuua mbawala, kwa hiyo anajulikana kuwa mwindaji mkali sana.

Kumfahamu na Kumhifadhi Simba-Mangu

Anapokuwa tayari kujamiiana, simba-mangu wa kike hutoa harufu fulani na hulia. Baada ya kujamiiana, yeye huzaa watoto wanne hivi wakati mmoja, chakula kinapopatikana kwa wingi nyakati nyingine anaweza kuzaa watoto saba. Jambo la kupendeza ni kwamba wakati ambapo chakula si kingi, simba-mangu huzaa watoto wachache.

Si rahisi kuwaona simba-mangu kwa sababu wao huepuka maeneo yaliyo na watu. Jitihada za kuhifadhi simba-mangu zimefanya waongezeke katika maeneo mengi ya British Columbia. Pia, huenda mbinu za siku hizi za kukata miti zimesaidia kuwahifadhi kwa sababu nyasi humea katika nafasi ndogondogo zinazoachwa katika msitu ambapo sungura wanaweza kula. Kadiri sungura wanavyoongezeka ndivyo simba-mangu huongezeka.

Kiumbe huyu mwenye kuvutia ni muhimu katika mazingira. Kama wawindaji wengine, yeye hutegemea windo lake. Kama kitabu kimoja kuhusu mazingira kilivyosema, ‘yeye pia hutegemea nyasi na matawi ambayo windo lake hula. Yeye hutegemea vilevile vijidudu walio katika udongo wa msitu ambao hutumiwa na mimea ambayo huliwa na wanyama ambao yeye hula.’ Kwa hakika, utata wa maumbile hutufunza umuhimu wa kuishi kupatana na mazingira yetu na kuyahifadhi kwa ajili ya viumbe kama simba-mangu.