Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Misitu ya Mvua Je, Tunaweza Kuitumia Bila Kuiharibu?

Misitu ya Mvua Je, Tunaweza Kuitumia Bila Kuiharibu?

Misitu ya Mvua Je, Tunaweza Kuitumia Bila Kuiharibu?

WEWE unafikiri kwamba wakataji-miti wana haki ya kuharibu misitu yote ya mvua ulimwenguni? Yaelekea utajibu, la! Hata hivyo, wataalamu fulani wa viumbe na mazingira huenda wakasisitiza kwamba wengi wanaosema la, tayari wamesema ndiyo—kwa mfano, kwa kununua vyombo vya mbao vilivyotengenezwa kwa mbao maridadi na zinazopendwa sana zinazotoka kwenye misitu ya asili ya mvua badala ya misitu inayopandwa na watu.

Mara nyingi kukata miti huonwa kuwa sawa na kuharibu misitu. Na bila shaka, ukataji wa miti huharibu misitu mingi. Hata hivyo, inadaiwa kwamba miti imekatwa kwenye misitu fulani bila kuiharibu. Je, kweli misitu ya mvua na wanyama-pori wataokoka miti ikiendelea kukatwa? Hebu kwanza tuchunguze jinsi ukataji-miti unavyoharibu misitu.

Jinsi Ukataji-Miti Unavyoweza Kuharibu Msitu na Kuwaangamiza Wanyama-Pori

Fikiria kisa hiki: Matingatinga yanaanza kuchimba barabara ndani ya msitu. Punde si punde wakataji-miti wanaanza kufanya kazi kwa misumeno ya minyororo. Kampuni ya kukata miti ina kibali cha muda mfupi cha kupasua mbao, kwa hiyo wafanyakazi wameagizwa wabebe kila mti wenye thamani. Miti hiyo yenye thamani inapoanguka, inaharibu miti mingine iliyo karibu ambayo imeunganishwa na mimea inayotambaa. Kisha, matingatinga makubwa yanapenya vichaka ili kukokota magogo, na yanakanyaga-kanyaga udongo huo mwembamba na kuufanya ukose rutuba.

Kwa kawaida wafanyakazi wa kampuni hiyo wanakula nyama nyingi kuliko wanakijiji. Wanawinda wanyama wengi msituni; mara nyingi hata zaidi ya wanaohitaji. Barabara zinazoachwa na wakataji-miti hufika sehemu ambazo hazingefikika hapo awali. Sasa wawindaji wanaweza kuingia humo kwa magari wakiwa na bunduki ili kumaliza wanyama waliobaki. Wategaji hunasa wanyama wadogo na ndege kwa ajili ya biashara yenye faida kubwa ya wanyama-vipenzi. Wahamaji na maelfu ya watu wasio na makao huja wakitafuta nafasi ya kujiruzuku kwenye maeneo hayo mapya. Njia yao ya kilimo ya kukata na kuchoma misitu humaliza miti inayobaki, na hivyo mvua kubwa huja na kusomba udongo mwembamba wa juu.

Ni kana kwamba msitu umekufa. Uharibifu ulianza miti ilipoanza kukatwa. Lakini je, ni lazima kukata miti kuharibu misitu ya mvua?

Kukata Miti Bila Kuharibu Mazingira

Katika miaka ya karibuni watu wamependezwa kujua mbinu ya kukata miti bila kuharibu mazingira na kutunza misitu kwa njia inayofaa. Lengo ni kukata miti katika njia ambayo itapunguza uharibifu wa misitu na wanyama-pori. Pole kwa pole msitu husitawi tena, na hivyo miti inaweza kukatwa miaka kadhaa baadaye. Kwa sababu ya mkazo kutoka kwa wahifadhi wa misitu, wafanyabiashara fulani sasa hutangaza kwamba mbao zao zinatoka kwenye misitu ambayo imethibitishwa kuwa misitu inayotunzwa ifaavyo. Na tuchunguze utaratibu wa kukata miti bila kuharibu mazingira.

Mtaalamu wa misitu na kikundi cha wasaidizi wanaingia msituni. Kikundi hicho ni baadhi ya vikundi kadhaa ambavyo vitakaa msituni kwa muda wa miezi sita hivi, vikihesabu miti. Kampuni ya kukata miti ina kibali cha muda mrefu, kwa hiyo wafanyakazi wana wakati wa kuchunguza miti ili wahifadhi msitu kwa matumizi ya baadaye.

Mtunzaji wa misitu huandika jina la jamii na nambari ya utambulisho kwenye kila mti. Hapana shaka kwamba ana ujuzi mwingi kwa sababu kuna mamia ya jamii za miti. Hata hivyo, hatua ifuatayo yahitaji tekinolojia ya kisasa.

Akitumia mashine ndogo inayowasiliana na kifaa cha kupokea habari kutoka kwa setilaiti, mtunzaji wa misitu anarekodi ukubwa wa mti, jamii yake, na nambari yake ya utambulisho. Kisha anapohifadhi habari hizo kwenye mashine hiyo, habari zote kuhusu mti huo kutia ndani mahali hususa ulipo, zinawasilishwa kwenye kompyuta iliyo katika jiji kubwa mbali sana.

Baadaye msimamizi wa misitu anatumia kompyuta yake kuchapisha ramani yenye habari kamili kuhusu kila mti wenye thamani msituni. Anachagua miti hususa inayoweza kukatwa kulingana na sheria zilizowekwa. Kuhusu jamii nyingi za miti, inaruhusiwa kukata asilimia 50 tu ya miti yenye kipenyo hususa kilichoonyeshwa kwenye kibali. Miti ya kale na yenye afya zaidi yapaswa kuachwa ili izae mbegu.

Lakini, unawezaje kukata miti bila kuharibu msitu? Mwandishi wa Amkeni! alimwuliza swali hilo Roberto, mtunzaji wa misitu aliyetajwa katika makala iliyotangulia. Alieleza hivi: “Ili kufanya hivyo unahitaji ramani. Tukiwa na ramani ya miti, tunaweza kupanga jinsi ya kukata miti ili tusiharibu sana msitu. Hata tunaweza kupanga upande ambao miti itaanguka tunapoikata ili tusiharibu miti mingine iliyo karibu.

“Pia tunaweza kupanga kuondoa magogo kwa kuyanyanyua kwa kreni, badala ya kutumia matingatinga kwenda kuchukua kila mti mahali ulipo. Kabla ya kukata mti, wakataji hukata mimea inayotambaa kutoka mti huo hadi miti mingine iliyo karibu ili isiharibiwe. Tunakata miti kwa mzunguko, kila mwaka tunachora ramani na kukata miti katika sehemu fulani na hivyo angalau miaka 20 inapita kabla ya kurudi kwenye sehemu hizo. Katika misitu mingine tunarudi baada ya miaka 30.”

Hata hivyo, Roberto ameajiriwa na kampuni ya kukata miti. Kwa hiyo mwandishi wa Amkeni! alimwuliza hivi: “Wakataji-miti wanajitahidi kwa kadiri gani kulinda wanyama-pori?”

Kulinda Wanyama

“Msitu hauwezi kusitawi bila wanyama,” asema Roberto. “Wanyama ni muhimu kwa uchavushaji na usambazaji wa mbegu. Tunajitahidi sana kutosumbua wanyama-pori. Kwa mfano, tunapanga kwa uangalifu barabara za kuingia msituni ili ziwe chache. Iwezekanapo, tunachimba barabara nyembamba ambazo zitaacha majani ya miti yakiwa yameshikana. Hilo huwaruhusu wanyama kama vile dubu wa mitini na tumbili kuvuka barabara bila kushuka miti.”

Roberto aonyesha sehemu fulani zenye rangi kwenye ramani yake. Hizo hazipaswi kuguswa kamwe. Kwa mfano, kuacha safu ya miti kwenye kingo za kila kijito huwaruhusu wanyama watoke sehemu moja hadi nyingine bila kuvuka eneo lisilo na miti.

“Mbali na mazingira muhimu yaliyo kando ya vijito,” anaeleza, “tunalinda pia mapango, miamba mikubwa, miti ya kale yenye mapengo, na miti ya matunda yenye maji mengi, yaani, eneo lolote ambalo ni muhimu kwa viumbe fulani. Ili kuzuia uwindaji haramu, tunawakataza wafanyakazi wetu kuwa na bunduki, na tunawaletea nyama ya ng’ombe na kuku kwenye kambi yao ili wasiwinde wanyama-pori. Kisha, tunapomaliza kukata miti sehemu moja, sisi hufunga au kulinda barabara ili kuzuia wawindaji au wakataji-miti haramu kuingia msituni.

“Mimi binafsi hufurahi kufanya hivyo kwa sababu ninapenda kuhifadhi uumbaji wa Mungu. Lakini karibu hatua zote nilizoeleza ziko kwenye sheria za kimataifa za kupokea cheti cha msitu uliotunzwa ifaavyo. Ili kampuni ipate cheti, lazima iwathibitishie wakaguzi wa mashirika ya kimataifa kwamba inafuata sheria hizo.”

Je, misitu inayotunzwa ifaavyo ina faida? Kwa kawaida wakataji-miti hawakubali kwa utayari kuhifadhi wanyama-pori isipokuwa watunzaji wachache tu wa misitu kama Roberto. Mara nyingi wanaona kwamba sheria hizo zinawazuia kupata faida.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa mashariki mwa Amazonia mwishoni mwa miaka ya 1990 uligundua kwamba gharama ya kuchora ramani za miti, kukata mimea inayotambaa, na kuondoa miti ilikuwa ndogo sana, kwa sababu ya kutumia mbinu bora. Kwa mfano, ni miti michache tu iliyopotea. Mara nyingi bila ramani hizo, watu wanaokata miti kwa msumeno hukata mti lakini wale wanaoikusanya miti hawaupati kwa sababu msitu huo una miti mingi sana.

Pia, mbao ambazo zimeidhinishwa kutoka kwa msitu unaotunzwa ifaavyo zinaweza kuuzwa kwa urahisi. Lakini je, kukata miti bila kuharibu mazingira kwaweza kweli kulinda viumbe? Ni wanyama-pori wangapi ambao hubaki baada ya miti kukatwa kwenye misitu ya mvua?

Je, Wanyama-Pori Wanaweza Kubaki Baada ya Miti Kukatwa?

Ni kweli kwamba, mimea na viumbe walio kwenye misitu ya mvua ni tata na wanahitaji kutunzwa kwa uangalifu. Hata hivyo, kwa kushangaza, wanaweza kuokoka chini ya hali fulani. Kwa mfano, ikiwa miti inakatwa katikati ya msitu, miche ya miti hiyo hukua polepole na kufunika sehemu hizo. Lakini vipi wanyama, ndege, na wadudu?

Jamii chache za wanyama huathiriwa sana, na mara nyingi ukataji wa miti hupunguza idadi ya ndege na wanyama mbalimbali katika sehemu hiyo. Hata hivyo, kwa kawaida kukata miti bila kuharibu mazingira hakuathiri jamii nyingi za viumbe. Ama kweli, kukata miti kadhaa katika msitu kwaweza kuzisaidia jamii fulani ziongezeke. Uchunguzi wa hivi karibuni unadokeza kwamba viumbe mbalimbali wa misitu ya mvua wanaweza kuongezeka kwa sababu ya kuwapo kwa wanadamu—hata kama baadhi yao wanakata miti hususa.

Kwa hiyo ushuhuda mwingi unadokeza kwamba miti inaweza kukatwa katika misitu ya mvua bila kuharibu viumbe mbalimbali. Gazeti Economist la London lilisema: “Asilimia 10 tu ya misitu inayobaki, ambayo inatunzwa ifaavyo, inaweza kutokeza mbao ngumu za kutosha. Sehemu kubwa inayobaki inaweza kulindwa.”

Msitu uliotajwa mwanzoni ni mfano wa msitu unaolindwa kabisa. Ramiro anaulinda kwa sababu wanasayansi wamegundua jamii fulani zilizo katika hatari ya kutoweka. Misitu ya mvua kama hiyo ni haba na ina viumbe wengi sana isivyo kawaida. Ramiro aneleza kwamba “siri ya kuhifadhi misitu ni kuwaelimisha watu. Wanakijiji walipogundua kwamba maji yao yanatokana na msitu huo, walijitahidi kuuhifadhi.”

Ramiro aongezea: “Watalii wa kuhifadhi mazingira ni muhimu pia kwa sababu wanajifunza kwa nini miti na mimea tofauti-tofauti inastahili kulindwa. Wanapoondoka wanakuwa wamethamini zaidi msitu na wanyama-pori.”

Mfano wa Ramiro na Roberto unaonyesha kwamba mwanadamu anaweza kutumia msitu wa mvua bila kuuharibu wala kuangamiza wanyama-pori. Lakini jambo hilo halimaanishi kwamba itakuwa hivyo. Leo watu fulani wanaweza kuhakikisha kwamba mbao wanazonunua zinatoka kwenye msitu uliothibitishwa kuwa unatunzwa ifaavyo. Hata hivyo, wengine hawawezi kuthibitisha jambo hilo. Je, jitihada za kuhifadhi misitu zitaokoa viumbe mbalimbali wenye kupendeza?

[Ramani katika ukurasa wa 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BOLIVIA

Ramani iliyo upande wa kulia inatoa habari za kila mti; kama ilivyo juu, ramani hiyo inaonyesha sehemu ndogo tu ya Bolivia

[Hisani]

All maps except top left: Aserradero San Martin S.R.L., Bolivia

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kila mti hutiwa nambari na jina la jamii yake. Kisha, mahali pake hususa hurekodiwa kwa kutumia kifaa (kilicho juu) cha kupokea habari kutoka kwa setilaiti

[Picha katika ukurasa wa 7]

‘Ramani ya kuhesabu miti ni muhimu katika kupanga ukataji wa miti bila kuharibu msitu au wanyama-pori.’—Roberto

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

“Siri ya kuhifadhi misitu imekuwa kuwaelimisha watu.”—Ramiro

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]

Foto: Zoo de Baños