Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mitishamba Inaweza Kukusaidia?

Je, Mitishamba Inaweza Kukusaidia?

Je, Mitishamba Inaweza Kukusaidia?

TANGU jadi, mitishamba imetumiwa kutibu magonjwa. Mafunjo ya Ebers, yenye mamia ya majina ya dawa za mitishamba za kutibu magonjwa mbalimbali, yalitayarishwa huko Misri karibu na karne ya 16 K.W.K. Hata hivyo, kwa kawaida vizazi mbalimbali vilifundishwa kwa mdomo kuhusu mitishamba.

Inaonekana taaluma ya mitishamba ilianzishwa huko Magharibi na daktari Mgiriki Dioscorides, aliyeandika kitabu De Materia Medica. Hicho kilikuwa kitabu kikuu cha dawa kwa miaka 1,600 iliyofuata. Katika sehemu nyingi duniani, mitishamba hutumiwa. Huko Ujerumani, serikali hata hugharimia matibabu ya mitishamba.

Ingawa inadaiwa kwamba mitishamba na dawa za kienyeji ni salama kuliko dawa za kawaida, zina hatari pia. Hivyo maswali haya yanazuka: Ni mambo gani tunayopaswa kuzingatia kabla ya kutumia mitishamba? Je, kuna wakati ambapo mitishamba inafaa kuliko dawa za kawaida? *

Faida za Mitishamba

Inasemekana kwamba mitishamba hutibu magonjwa mengi. Inadhaniwa kwamba mingine husaidia mwili kupambana na maambukizo, mingine husaidia kusaga chakula, kutuliza mwili, au kudhibiti tezi.

Mitishamba inaweza kutumiwa kama chakula ama dawa. Kwa mfano, mimea fulani inayosaidia mwili kuondoa maji kama vile kitimiri, ina madini mengi ya potasiamu. Kwa hiyo mimea hiyo husaidia kurudisha madini hayo ambayo hupotea mtu anapokojoa. Vivyo hivyo, mmea unaoitwa Valeriana officinalis, ambao umetumiwa kwa muda mrefu kutuliza mwili una kalisi nyingi. Kalisi hiyo husaidia kutuliza neva.

Jinsi ya Kutumia Mitishamba

Mitishamba inaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali kama vile kuichanganya na maji, kutengeneza tinkcha, na kuipaka mwilini. Unaweza kutengeneza kinywaji cha mitishamba kwa kuitia ndani ya maji ya moto. Lakini wataalamu wanaonya kwamba mitishamba hiyo haipaswi kuchemshwa na maji. Pia dawa zilizotokana na mizizi na magamba ya miti huchemshwa ndani ya maji.

Vipi tinkcha? Kitabu kimoja kinasema kwamba “hiyo ni mitishamba iliyotengenezwa kwa vileo fulani kama vile brandi au vodka.” Pia kuna mitishamba inayopakwa mwilini ambayo hutayarishwa kwa njia mbalimbali. Mara nyingi hupakwa kwenye sehemu zilizoambukizwa au zenye maumivu.

Tofauti na vitamini na dawa nyingine, mitishamba mingi huonwa kuwa chakula, hivyo huliwa peke yake mtu akiwa na njaa. Ni rahisi kumeza vidonge vya mitishamba. Ukiamua kutumia mitishamba, omba mashauri ya wataalamu.

Tangu zamani, mitishamba imetumiwa kutibu mafua, matatizo ya tumbo, kufunga choo, matatizo ya kupata usingizi, na kichefuchefu. Hata hivyo, mitishamba pia hutumiwa nyakati nyingine kuponya magonjwa hatari na hata kuyazuia. Kwa mfano, nchini Ujerumani na Austria, mmea unaoitwa saw palmetto hutumiwa kutibu uvimbe wa tezi ya kibofu. Katika nchi fulani asilimia 50 mpaka 60 ya wanaume hupata uvimbe huo. Hata hivyo, ni muhimu daktari atambue chanzo cha uvimbe huo ili kuhakikisha kwamba huhitaji matibabu ya hali ya juu zaidi, kama ya kansa.

Tahadhari!

Hata kama mtishamba fulani huonwa kuwa salama, unahitaji kutahadhari. Usidhani kwamba dawa hiyo ni salama kwa sababu tu inatokana na mti wa “kiasili.” Ensaiklopidia moja kuhusu mitishamba inasema: “Jambo la kusikitisha ni kwamba mitishamba fulani ni hatari sana. [Inasikitisha kwamba] watu fulani hawaitumii mitishamba ifaavyo—iwe ni hatari au la.” Kemikali zilizo katika mitishamba zinaweza kubadili mpigo wa moyo, shinikizo la damu na kiwango cha sukari. Kwa hiyo, watu wenye matatizo ya moyo, kupanda kwa shinikizo la damu, au ugonjwa fulani wa sukari wanapaswa kutahadhari.

Hata hivyo, kwa kawaida, athari za mitishamba zinahusiana na mizio. Zinatia ndani kuumwa na kichwa, kizunguzungu, kichefuchefu au vipele. Pia inasemekana kwamba mitishamba humfanya mgonjwa aonekane kuwa anazidiwa kwa kutokeza dalili za mafua na nyinginezo. Inadaiwa kwamba hilo hutokea wakati uchafu unapoondolewa mwilini baada ya kuanza kutumia mitishamba.

Kwa kuwa mara nyingine watu hufa wanapotumia mitishamba fulani, ni muhimu kutahadhari na kufuata maagizo. Kwa mfano, mmea unaoitwa ephedra, ambao hutumiwa kupunguza uzito, unaweza pia kupandisha shinikizo la damu. Imeripotiwa kwamba zaidi ya watu 100 nchini Marekani wamekufa baada ya kutumia dawa zilizotengenezwa kwa mmea huo, lakini mtaalamu wa magonjwa huko San Francisco, Steven Karch anasema: “Kama nijuavyo, watu waliokufa [baada ya kutumia ephedra] walikuwa na ugonjwa mbaya wa moyo au waliitumia kupita kiasi.”

Mwandishi wa kitabu kinachozungumzia mitishamba Dakt. Logan Chamberlain, anasema hivi: “Katika miaka ya majuzi, karibu kila mtu ambaye aliathiriwa na mitishamba hakufuata maagizo. . . . Maagizo ya kutumia mitishamba inayofaa ni salama na hata hayapiti kiasi. Usiyapuuze isipokuwa tu umeshauriwa na daktari wa mitishamba.”

Daktari wa mitishamba Linda Page anaonya hivi: “Hata kama una ugonjwa hatari, inafaa kutumia mitishamba kwa kiasi. Utapata matokeo mazuri ukiwa na subira na kutumia mitishamba kwa kiasi. Inachukua muda kupona.”

Kitabu kimoja cha mitishamba kinaeleza kwamba mitishamba fulani inaweza kuzuia mwili usiathiriwe hata ikitumiwa kupita kiasi. Kwa mfano, mtishamba mmoja unaotumiwa kutuliza mwili humfanya mtu atapike akiutumia kupita kiasi. Hata hivyo, kwa kuwa si mitishamba yote inayoweza kufanya hivyo, hiyo si sababu ya kutofuata maagizo.

Hata hivyo, watu wengi wanaamini kwamba ili mtishamba ufanye kazi, ni lazima kiasi kikubwa kitumiwe na kwa njia inayofaa. Wakati mwingine njia pekee ya kufanya hivyo ni kutumia sehemu fulani za mti huo. Mfano mmoja wa jambo hilo ni mti wa ginkgo biloba, uliotumiwa kwa muda mrefu kuboresha kumbukumbu na mzunguko wa damu. Majani mengi ya mti huo hutumiwa ili kumsaidia mgonjwa.

Mchanganyiko Hatari

Mitishamba inaweza kusababisha athari mbalimbali inapotumiwa pamoja na dawa za kawaida. Kwa mfano, inaweza kuongeza au kupunguza nguvu za dawa, kuondoa dawa hiyo mwilini haraka, au kuongeza athari za dawa hiyo. Mtishamba wa St. John’s wort, ambao hutumiwa mara nyingi huko Ujerumani na watu walioshuka moyo, hufanya dawa ziondolewe mwilini haraka, hivyo kupunguza nguvu za dawa hizo. Kwa hiyo, ikiwa unatumia dawa za kawaida kama vile dawa za kupanga uzazi, pata ushauri wa daktari kabla ya kutumia mitishamba.

Kitabu kinachozungumzia matibabu ya mitishamba kinasema: “Kileo, bangi, kokeini, dawa nyingine za kutuliza akili, na tumbaku zinaweza kusababisha kifo zinapotumiwa pamoja na mitishamba fulani. . . . Ni jambo la akili kuepuka [vitu hivyo], hasa unapokuwa mgonjwa.” Pia wanawake wajawazito na akina mama wanaonyonyesha wanapaswa kuzingatia mashauri hayo. Bila shaka, Wakristo wanalindwa kutokana na matumizi ya tumbaku na dawa za kulevya wanapotii amri ya Biblia ya ‘kujisafisha wenyewe kila unajisi wa mwili na roho.’—2 Wakorintho 7:1.

Kitabu kimoja kinaonya hivi kuhusu mitishamba: “Ukipata mimba unapokuwa ukitumia mitishamba, mwambie daktari na usiitumie kabla hujaongea naye. Jaribu kukumbuka uliitumia kwa kadiri gani na kwa muda gani.”

Ensaiklopidia moja ya mitishamba inasema, “kuna hatari mbalimbali za kujitibu kwa mitishamba.” Katika sanduku, “Hatari za Kujitibu” utaona hatari zinazoweza kusababishwa na mitishamba.

Kama ilivyo na dawa nyingine, mitishamba inapaswa kutumiwa ifaavyo, kwa hekima, na kwa kiasi. Inafaa kukumbuka kwamba kwa sasa magonjwa mengine hayana tiba. Wakristo wa kweli wanatazamia wakati ambapo kisababishi cha magonjwa na kifo, yaani, kutokamilika tulikorithi kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza, kitakomeshwa kabisa chini ya utawala mzuri wa Ufalme wa Mungu.—Waroma 5:12; Ufunuo 21:3, 4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Amkeni! si jarida la tiba, kwa hiyo halipendekezi matibabu hususa, iwe ni ya mitishamba au la. Habari zinazopatikana katika makala hii ni za kuelimisha tu. Wasomaji wanapaswa kujiamulia wenyewe masuala yanayohusu afya na tiba.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

Hatari za Kujitibu

Zifuatazo ni hatari za kutumia mitishamba bila kupata ushauri wa kitaalamu.

Labda hujui ugonjwa wako.

Hata ikiwa unajua ugonjwa wako, huenda unajitibu kwa njia isiyofaa.

Huenda unatibu dalili za ugonjwa wako badala ya kutibu ugonjwa wenyewe.

Huenda mitishamba unayotumia ikazuia utendaji wa dawa zilizopendekezwa na daktari kama vile dawa za mizio au za shinikizo la damu.

Huenda unapotibu ugonjwa fulani ukazidisha ugonjwa mwingine, kama vile kupanda kwa shinikizo la damu.

[Hisani]

Source: Rodale’s Illustrated Encyclopedia of Herbs