Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nani Wanaosababisha Tisho la Vita vya Nyuklia?

Ni Nani Wanaosababisha Tisho la Vita vya Nyuklia?

Ni Nani Wanaosababisha Tisho la Vita vya Nyuklia?

“Kuna uwezekano kwamba wanadamu wataangamizwa katika vita vya nyuklia. Tisho hilo lingalipo leo, . . . ingawa Vita Baridi vilikoma zaidi ya miaka kumi iliyopita.”—Robert S. McNamara, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani na James G. Blight, profesa wa mahusiano ya kimataifa katika Taasisi ya Watson ya Uchunguzi wa Kimataifa.

KATIKA MWAKA WA 1991, Vita Baridi vilipomalizika, ile saa maarufu ya siku ya maangamizi ilirudishwa nyuma hadi “saa sita usiku” kasoro dakika 17. Saa ya siku ya maangamizi inaonyeshwa kwenye jalada la gazeti Bulletin of the Atomic Scientists na inaonyesha jinsi inavyodhaniwa kwamba ulimwengu unakaribia vita vya nyuklia (saa sita usiku). Wakati huo, saa hiyo ilirudishwa nyuma zaidi kutoka saa sita za usiku tangu ilipoanzishwa mwaka wa 1947. Hata hivyo, tangu wakati huo, mkono wa dakika umeanza kusonga mbele tena. Kwa mfano, katika Februari 2002, saa hiyo ilisogezwa mbele hadi saa sita kasoro dakika saba usiku, na hiyo ilikuwa mara ya tatu kusogezwa tangu Vita Baridi kumalizika.

Kwa nini wachapishaji wa gazeti hilo la kisayansi walisogeza saa hiyo mbele? Kwa nini wanaona kwamba bado kuna tisho la vita vya nyuklia? Na tisho la amani linatoka wapi?

Kupunguza Silaha kwa Ujanja

Gazeti Bulletin of the Atomic Scientists linasema hivi: “Zaidi ya silaha 31,000 za nyuklia bado zinahifadhiwa.” Linaongezea hivi: “Asilimia 95 ya silaha hizo zinapatikana Marekani na Urusi, na zaidi ya 16,000 zimetegwa.” Huenda watu fulani wakaona hila iliyopo katika idadi ya silaha za nyuklia zilizopo. Je, mataifa yenye silaha nyingi zaidi za nyuklia hayakusema kwamba tayari yamepunguza silaha zao hadi 6,000 kwa kila nchi?

Hapa pana ujanja fulani. Ripoti ya Shirika la Carnegie la Amani ya Kimataifa inasema hivi: “Idadi ya makombora 6,000 inategemea njia fulani ya kuhesabu iliyokubaliwa katika Mashauriano ya Kupunguza Silaha za Nyuklia. Mataifa yote mawili yatabaki na maelfu ya silaha za ziada za masafa mafupi na nyingine akibani.” (Italiki ni zetu.) Kulingana na gazeti Bulletin of the Atomic Scientists, “makombora mengi ya Marekani yaliyoteguliwa yatahifadhiwa (pamoja na makombora 5,000 hivi yaliyo akibani) badala ya kuharibiwa.”

Kwa hiyo, mbali na maelfu ya silaha za nyuklia zilizotegwa—ambazo zinaweza kurushwa kutoka bara moja hadi lingine—kuna maelfu ya makombora ya nyuklia na ya masafa mafupi yaliyotengenezwa kushambulia maeneo ya karibu. Bila shaka, mataifa mawili yenye silaha nyingi zaidi za nyuklia bado yana silaha tele za nyuklia katika maghala yao zinazoweza kuua watu wote ulimwenguni mara kadhaa! Kuhifadhi idadi kubwa hivyo ya silaha hatari kunaleta tisho lingine, yaani kurusha makombora ya nyuklia bila kukusudia.

Vita vya Nyuklia Visivyokusudiwa

Kulingana na Robert S. McNamara na James G. Blight, walionukuliwa mwanzoni, “nguvu za nyuklia za Marekani zimedhibitiwa na ‘mfumo wa kurusha makombora kunapokuwa na mashambulizi.’” Hiyo inamaanisha nini? Wanaeleza hivi: “Makombora yetu yako tayari kurushwa wakati uleule makombora ya Urusi yako angani. Kulingana na mfumo huo, dakika 15 haziwezi kupita kabla ya makombora yetu kurushwa baada ya kuonywa kwa mara ya kwanza kwamba Urusi inashambulia.” Kulingana na aliyekuwa afisa wa Marekani wa kurusha makombora ya nyuklia yaliyotegwa, “karibu makombora yote yaliyotegwa yako tayari kurushwa baada ya dakika mbili.”

Hali hiyo ya kuwa chonjo inaonyesha kwamba makombora yanaweza kurushwa bila kukusudia kwa sababu ya onyo la uwongo. Makala moja katika gazeti U.S.News & World Report inaeleza hivi: “Amri za kurusha makombora zimetolewa kimakosa mara kadhaa wakati wa majaribio ya nyuklia ya Marekani.” Maonyo ya uwongo kama hayo yametolewa nchini Urusi pia. Roketi ya uchunguzi ya Norway ilipotoa onyo la uwongo mwaka wa 1995, rais wa Urusi alianza kujitayarisha kurusha makombora ya nyuklia.

Mfumo huo wa kurusha makombora kunapokuwa na onyo huwatia mfadhaiko mwingi wale wanaofanya maamuzi hayo. Jambo zuri ni kwamba wakati uliopita makamanda walitambua kwamba maonyo hayo ni ya uwongo na hivyo kufikia sasa vita vya nyuklia vimeepukwa. Mtafiti mmoja alisema hivi kuhusu tukio la mwaka wa 1979: “Wamarekani hawakurusha makombora yao kwa sababu ya setilaiti zinazotoa maonyo mapema zilizoonyesha hakukuwa na makombora yoyote ya Sovieti angani.” Hata hivyo, baada ya muda setilaiti hizo huharibika. Watafiti na wachanganuzi wana wasiwasi kwamba “setilaiti nyingi za Urusi za kuonya zimeharibika au zimeondoka kwenye njia yake.” Kama vile aliyekuwa naibu wa kamanda wa jeshi la wanamaji la Marekani alivyosema miaka mingi iliyopita, “uwezekano wa kushambuliwa bila kutambua au kurusha makombora kimakosa, au kwa sababu mtu fulani asiyefaa amepewa mamlaka ni mkubwa leo kuliko wakati mwingine wowote uliopita.”

Washiriki Wapya wa Chama cha Nyuklia

Ijapokuwa silaha nyingi za nyuklia zinamilikiwa na mataifa mawili yenye nguvu, kuna mataifa mengine yenye silaha za nyuklia kama vile China, Ufaransa, na Uingereza. Mataifa hayo yanaitwa chama cha nyuklia, na hivi majuzi India na Pakistan zimekuwa wanachama. Mbali na nchi hizo, nchi nyingine kadhaa, kutia ndani Israel, mara nyingi huonwa kuwa zinataka kuunda au tayari zina silaha hizo.

Migogoro ya kisiasa kati ya washiriki wa chama cha nyuklia, kutia ndani wanachama hao wapya, inaweza kuchochea vita vya nyuklia. Gazeti Bulletin of the Atomic Scientists linasema kwamba “mgogoro kati ya India na Pakistan . . . ni mfano wa jinsi mataifa mawili yalivyokaribia vita vya nyuklia zaidi tangu Mgogoro wa Makombora wa Kuba.” Watu wengi walianza kuogopa sana kwamba vita vya nyuklia vingetokea wakati hali zilipochacha mapema mwaka wa 2002.

Isitoshe, kutengenezwa kwa silaha zinazoweza kuangamiza watu wengi kumeongeza uwezekano wa matumizi ya mabomu ya nyuklia. Likizungumzia ripoti ya siri ya jeshi la Marekani, gazeti The New York Times lilisema kwamba huenda “uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia kuharibu hifadhi za adui za silaha za kibiolojia, za kemikali, na nyingine za kuangamiza watu wengi,” umekuwa sehemu ya sera ya Marekani ya silaha za nyuklia.

Mashambulizi ya magaidi huko Marekani katika Septemba 11, 2001, yanaonyesha kwamba kuna tisho la vita vya nyuklia. Watu wengi leo wanaamini kwamba mashirika ya kigaidi yanajaribu kutengeneza au tayari yana silaha za nyuklia. Inawezekanaje?

Magaidi na Mabomu ya Kujitengenezea

Je, inawezekana kutengeneza bomu la nyuklia kwa kutumia vifaa vinavyouzwa kimagendo? Kulingana na gazeti Time, jibu ni ndiyo. Gazeti hilo liliripoti kuhusu kikundi kilichoundwa ili kuzuia magaidi wasitumie silaha za nyuklia. Kufikia sasa, kikundi hicho “kimeunda zaidi ya [mabomu] kumi na mawili” kwa kutumia “vifaa vinavyopatikana katika maduka ya vifaa vya elektroni na kemikali za nyuklia zinazouzwa kimagendo.”

Kubomoa na kutegua silaha za nyuklia kumeongeza uwezekano wa wizi wa vifaa vya nyuklia. Gazeti Time linasema hivi: “Kuondoa maelfu ya silaha za nyuklia za Urusi kutoka kwenye mizinga iliyolindwa sana, vifaa vya kurusha mabomu, na nyambizi na kuzihifadhi katika sehemu zisizo na ulinzi mkali kutawavutia magaidi sugu.” Iwapo kikundi kidogo cha watu kingepata visehemu vya silaha za nyuklia zilizobomolewa na kuviunganisha, kingekuwa mwanachama wa chama cha nyuklia!

Gazeti Peace linasema kwamba hata si lazima kuunda bomu ili ujiunge na chama cha nyuklia. Kinachohitajiwa tu ni kuwa na kiasi cha kutosha cha urani au plutoniamu inayoweza kulipuka. Gazeti hilo linasema hivi: “Magaidi walio na urani inayoweza kutengeneza silaha za kisasa wanaweza kusababisha mlipuko kwa kutupa kipande kimoja cha urani juu ya kile kingine.” Ni kiasi gani cha urani kinachohitajiwa ili kutokeza mlipuko? Kulingana na gazeti hilo, “kilogramu tatu zinatosha.” Kiasi hicho ni sawa na kile wauzaji wa magendo walipokonywa wakati walipokamatwa katika Jamhuri ya Cheki mnamo mwaka wa 1994!

Mabaki ya silaha za nyuklia pia yanaweza kutumiwa kutengeneza silaha za nyuklia. Gazeti The American Spectator linasema hivi: “Wataalamu wanaogopeshwa sana na mchanganyiko hatari unaoweza kutengenezwa kwa mabaki ya silaha za nyuklia na vilipukaji vya kawaida.” Mabaki hayo yanaweza kutumiwa kutengeneza silaha za nyuklia. Ni hatari kadiri gani? Gazeti IHT Asahi Shimbun linasema kwamba mabomu ya kujitengenezea hutumia “vilipukaji vya kawaida kutawanya kemikali hatari ili kutia sumu sehemu fulani badala ya kuzilipua au kuziteketeza.” Linaongezea hivi: “Silaha hizo zinaweza kusababisha magonjwa ya mnururisho au maumivu makali, halafu pole kwa pole mtu hufa.” Ingawa watu fulani wanasema kwamba kutumia mabaki ya silaha za nyuklia zinazopatikana kwa urahisi hakuwezi kusababisha madhara makubwa, kuwapo kwa kemikali hizo za nyuklia za magendo kunawatia wengi wasiwasi. Kulingana na uchunguzi wa hivi majuzi uliofanywa ulimwenguni pote, zaidi ya asilimia 60 ya watu waliohojiwa wanaona kwamba magaidi watatumia silaha za nyuklia katika miaka kumi ijayo.

Bila shaka, kuna tisho la vita vya nyuklia. Gazeti Guardian Weekly la Uingereza la Januari 16-22, 2003, lilisema hivi: “Baada ya vita baridi, sasa ndio kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba Marekani itatumia silaha za nyuklia. . . . Marekani inaongeza uwezekano wa vita vya nyuklia hatua kwa hatua.” Kwa hiyo, inafaa kuuliza hivi: Je, vita vya nyuklia vinaweza kuepukwa? Je, kuna tumaini kwamba kutakuwa na ulimwengu usio na tisho la nyuklia? Maswali hayo yatajibiwa katika makala inayofuata.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Je, Hii Ni Enzi ya Pili ya Nyuklia?

Akiandika katika gazeti The New York Times Magazine, mwandishi Bill Keller (ambaye sasa ni mhariri mkuu wa gazeti The New York Times) alisema kwamba mataifa yako katika enzi ya pili ya nyuklia. Enzi ya kwanza iliisha Januari 1994, wakati nchi ya Ukrainia ilipokubali kusalimisha silaha ilizorithi kutoka kwa ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Kwa nini anasema kuhusu enzi ya pili ya nyuklia?

Keller anaandika hivi: “Enzi ya pili ya nyuklia ilianza kwa kishindo katika jangwa la Rajasthani mwaka wa 1998, wakati serikali mpya ya India ilipolipua mabomu matano ya majaribio. Majuma mawili baadaye Pakistan ikafanya vivyo hivyo.” Ni nini kilichofanya majaribio hayo kuwa tofauti na ya enzi ya kwanza ya nyuklia? “Hizo zilikuwa silaha za nyuklia zilizokusudiwa kutumiwa katika eneo hususa.”

Kwa hiyo, je, ulimwengu unaweza kuwa salama ikiwa kuna nchi mbili mpya zenye silaha za nyuklia? Keller anaongezea hivi: “Kila nchi inayopata silaha za nyuklia inaongeza uwezekano wa vita vinavyohusisha taifa lenye silaha za nyuklia.” —“The Thinkable,” The New York Times Magazine, Mei 4, 2003, ukurasa wa 50.

Hali hiyo inakuwa mbaya zaidi kutokana na habari kwamba huenda Korea Kaskazini ina “kiasi cha kutosha cha plutoniamu inayoweza kutengeneza mabomu sita mapya ya nyuklia. . . . Kila siku kuna hofu zaidi kwamba Korea Kaskazini itafaulu kutengeneza silaha mpya za nyuklia na hata labda kujaribu kutumia mojawapo ili kuonyesha imefaulu.” —The New York Times, Julai 18, 2003.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Afisa wa serikali akionyesha bomu bandia la nyuklia linalofanana na sanduku

[Hisani]

AP Photo/Dennis Cook

[Picha katika ukurasa wa 7]

Setilaiti za kale za kuonya zinaharibika

[Hisani]

NASA photo

[Picha katika ukurasa wa 5]

Earth: NASA photo