Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unastahimili Hali Ngumu

Unastahimili Hali Ngumu

Unastahimili Hali Ngumu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NAMIBIA

HEWA ni safi na yenye kuburudisha katika Jangwa la Namib lililoko kusini-magharibi mwa Afrika. Leo hakuna mawingu. Jua linapochomoza, joto linazidi. Huku kuna marundo ya mchanga na nyanda zenye changarawe zinazopigwa na upepo. Tunastaajabia yale tunayoona. Lile rundo la majani ni nini? Tunapokaribia, tunaona mmojawapo wa mimea ya ajabu zaidi ulimwenguni, mmea wa Welwitschia mirabilis. Neno hilo la pili ni la Kilatini na linamaanisha “ajabu.”

Kwa kawaida, mmea huo hupatikana tu katika maeneo ya jangwani ya Angola na Namibia. Mmea huo ni tofauti sana na mimea mingine hivi kwamba wanasayansi wameuweka katika kikundi cha aina yake ijapokuwa hakuna mmea mwingine ulio katika jamii hiyo. Chris Bornman anasema hivi katika kitabu chake Welwitschia—Paradox of a Parched Paradise: “Kati ya jamii 375,000 hivi za mimea zinazojulikana, hakuna mmea mwingine ambao umewapendeza wataalamu kama Welwitschia; wala hakuna mmea mwingine ambao umewapa wanadamu shida ya kuuainisha kama mmea huu.”

Mtu anapoutazama mmea huo, anaweza kufikiri ni kisiki cha mti kilichozungukwa na majani mengi, lakini mmea huo una majani mawili tu. Majani hayo yamepasuliwa-pasuliwa na upepo wa jangwani. Katika Kiafrikana, unaitwa tweeblaarkanniedood, yaani “majani mawili hayawezi kufa.” Jina mwafaka kwelikweli! Katika sehemu hii, halijoto wakati wa mchana inaweza kufikia nyuzi 40 Selsiasi, na wakati wa usiku kuna baridi kali sana na hakuna miti ya kuzuia pepo kali. Japo miti mingi hutegemea sana mizizi ili kufyonza maji kutoka udongoni, mmea wa welwitschia ni tofauti. Kwa wastani, eneo la Namib hupata mvua isiyozidi milimeta 25 kwa mwaka, na nyakati nyingine mvua hainyeshi kwa miaka mingi! Licha ya hali hizo, mmea huo huendelea kukua na majani yake hubaki yakiwa ya kijani. Wanasayansi wameshangazwa na hilo. Inaonekana mmea huo hufyonza ukungu wa asubuhi unaoletwa jangwani na pepo zinazovuma kwa ukawaida kutoka pwani.

Majani yake hayapukutiki wala kuchipuka. Majani yale mawili huendelea kukua katika maisha yote ya mmea huo. Jani moja liliponyooshwa, ilipatikana kwamba lina urefu wa zaidi ya meta 8.8! Hebu wazia jinsi majani yake yangekuwa marefu ikiwa hayangekauka wala kupukutika! Gazeti la kisayansi Veld & Flora, linasema kwamba ‘mmea huo ukiishi miaka 1500, unaweza kuwa na jani lenye urefu wa meta 225.’ Lakini je, mmea huo unaweza kuishi muda mrefu hivyo? Kitabu The World Book Multimedia Encyclopedia kinasema hivi: “Mimea ya welwitschia hukua polepole na mara nyingi huishi miaka 1,000 hadi 2,000.”

Ama kweli, mmea huo hustahimili hali ngumu. Ni nini kinachouwezesha mmea huo wa pekee kuishi muda mrefu hivyo katika hali ngumu sana za jangwani? Tunapaswa kumshukuru Mbuni mwenye hekima nyingi na Muumba, Yehova Mungu, ambaye anafanya “mimea ili itumikie wanadamu.”—Zaburi 104:14.