Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Watu Hulibusu Jiwe la Blarney?

Kwa Nini Watu Hulibusu Jiwe la Blarney?

Kwa Nini Watu Hulibusu Jiwe la Blarney?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND

HADITHI moja inasema hivi: Mtu mmoja alisimama akitetemeka mbele ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. Alikuwa tu amemweleza habari mbaya kutoka kwa mkuu mmoja wa Ireland na alifikiri Malkia angekasirika. Bila kutazamia, Malkia akaangua kicheko na kusema: “Hayo ni mambo ya mkuu wa Blarney. Yeye huongea tu!” Mara moja wasiwasi wa mtu huyo ukatoweka.

Malkia huyo aliyetawala kati ya mwaka wa 1558 mpaka 1603, hakutarajia kwamba maneno yake yangeanzisha desturi ya pekee nchini Ireland, yaani, kulibusu Jiwe la Blarney. Kila mwaka, maelfu ya watu huja kwenye mji mdogo wa Blarney ulio kilometa chache kaskazini mwa jiji la Cork, kwa ajili ya desturi hiyo ya ajabu. Wao hulibusu jiwe hilo kwa kuwa wanaamini kwamba watapata zawadi fulani, yaani, kusema kwa ufasaha.

Hadithi hiyo ilianzia wapi? Na zoea la kulibusu jiwe hilo lilianzaje? Ili kupata majibu, itatubidi tuchunguze mambo yaliyotukia karibu miaka 1,000 iliyopita.

Kasri Yenye Historia Ndefu

Kasri ya Blarney ilianzishwa katika karne ya 10 W.K., ikiwa ngome ndogo ya mbao. Baadaye, jengo la mawe lilijengwa badala yake. Kufikia katikati ya karne ya 15, familia ya MacCarthy ilikuwa imeifanya kasri hiyo kuwa mji mdogo. Wakati huo, hiyo ndiyo iliyokuwa kasri thabiti zaidi katika sehemu hiyo ya Ireland. Kuta nyingi za mawe zilikuwa na unene wa meta 5.5.

Mkuu wa familia hiyo, Cormac MacCarthy, aliyeishi kuanzia mwaka wa 1411 mpaka 1494, alitaka kuacha kitu ambacho kingefanya akumbukwe daima. Alichagua jiwe kubwa la chokaa, akachonga maandishi ya Kilatini juu yake ambayo yakitafsiriwa yanasema: “Shujaa Cormac MacCarthy ndiye aliyenijenga katika mwaka wa 1446 wa Bwana wetu.” Waashi waliliweka jiwe hilo juu ya mnara mkubwa wa Kasri ya Blarney. Hapo awali lilikuwa jiwe la kumbukumbu tu. Halikuhusianishwa na kusema kwa ufasaha mpaka zaidi ya karne moja baadaye.

Blarney na Kusema kwa Ufasaha

Ingawa hadithi iliyotajwa mwanzoni huenda ikawa upuuzi mtupu, inapatana na hali za wakati huo. Malkia Elizabeth alitaka wakuu wa Ireland waheshimu utawala wa Uingereza. Familia ya MacCarthy ilikuwa na wanajeshi elfu moja waliokuwa tayari kumsaidia Malkia vitani angalau mara moja. Kwa hiyo Malkia alikuwa na uhakika kwamba mkuu wa familia ya MacCarthy, Cormac McDermod MacCarthy, angeshawishiwa kwa urahisi kuwa mwaminifu kabisa kwake.

Kwa kuwa Malkia Elizabeth hangefanya makubaliano mwenyewe, alimtumia mwakilishi. Kulingana na hadithi hiyo iliyosimuliwa katika kitabu The Blarney Stone, wakati mwakilishi huyo alipowatuma maafisa ili wajaribu kumsadikisha MacCarthy kuapa kuwa mwaminifu kwa Malkia, Cormac alitoa “hotuba ndefu zenye ufasaha na za kurai, akiahidi mambo mengi bila kuyatimiza.”

Kulingana na hadithi hiyo, baadaye mwakilishi wa Malkia Elizabeth mwenyewe alienda kuzungumza na MacCarthy. Baadaye, mwakilishi huyo alirudi Uingereza kumpelekea malkia ripoti. Alijua kwamba malkia angechukizwa na habari zake kwamba, MacCarthy “aliomba muda zaidi” tena ili ajadiliane na washauri wake.

Baada ya malkia kuitikia kama ilivyonukuliwa mwanzoni mwa makala hii, alipendekeza jambo fulani kuhusu usemi mpya aliotumia. Alisema: “Tunapaswa kumpa Bwana Shakespeare neno hilo [blarney]! Litamfaa sana.” * Ikiwa hadithi hiyo ni ya kweli, basi Malkia Elizabeth alianzisha matumizi ya neno la Kiingereza “blarney” linalomaanisha “maneno ya kurai au ya kuhadaa au kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa.”

Vyovyote vile, kufikia mwaka wa 1789, desturi ya kulibusu Jiwe la Blarney ilikuwa imetia fora. Ilikuwa hatari kulibusu jiwe hilo kwa sababu ya mahali lilipowekwa kwenye ukuta wa kasri. Hivyo, kasri hiyo ilipofanyiwa ukarabati, jiwe hilo lilihamishwa ili lifikiwe kwa urahisi na limeendelea kuwa hapo hadi leo. Muda si muda, watu waliomiliki kasri hiyo, waliweka jiwe lingine lenye majina yao badala ya lile jiwe la MacCarthy.

Kutembelea Kasri Hiyo

Hivi majuzi tulitembelea kasri hiyo. Mnara mkubwa wenye jiwe maarufu la Blarney unaonekana waziwazi. Tuliingia mnarani na kupanda ngazi nzee zilizopindika za mawe. Hatimaye, tulitokea kwenye mlango mdogo mwembamba. Jiwe la Blarney liko kwenye ukuta ulio mbele.

Tulikaribia ili kumwona mwanamke akilibusu jiwe hilo. Ilimbidi alale chali huku kichwa chake na mabega yake yakiwa juu ya sehemu iliyo wazi yenye urefu wa meta tatu hivi na upana wa meta moja hivi. Mfanyakazi mmoja alisema, “Uko salama salimini. Huwezi kuanguka kwa kuwa kuna vyuma vya kukuzuia. Hata hivyo, nimekushikilia vizuri!”

Mwanamke huyo alipitisha mkono juu ya kichwa na kushika vyuma vilivyokuwa kwenye ukuta juu ya jiwe hilo. Kisha ni kana kwamba kichwa chake kilitoweka kabisa alipoinama zaidi kwenye sehemu hiyo iliyo wazi huku akiingiza kichwa kwanza. Alisogea karibu ili kulibusu jiwe hilo. Tulipomtazama kuanzia mabegani, tuliona kwamba alikuwa karibu meta 25 kutoka sakafuni!

Alilibusu jiwe hilo haraka iwezekanavyo, kisha akaanza kujiinua akitumia vile vyuma. Akisaidiwa na mfanyakazi huyo, alifaulu kujivuta na kuketi, kisha akaweza kusimama. Sasa ilikuwa nafasi ya mtu mwingine kufanya kukurukakara hizo!

Tulilitazama jiwe hilo na kuona kwamba limeparara sana. Mfanyakazi huyo alituambia kwamba, “liko hivyo kwa sababu watu wengi wamelibusu kwa miaka mingi. Lakini msijali, tunalisafisha mara nne au tano kila siku!”

Tayari kulikuwa na foleni ya watu waliotaka kulibusu. Hatukukusudia kulibusu kwani inaonekana desturi hiyo inahusiana na ushirikina, uwongo, na labda hata kuwasiliana na pepo. Hadithi nyingine inasema kwamba desturi hiyo ilianza wakati mwanamke mmoja mzee alipompatia nguvu za ufasaha mfalme mmoja aliyemwokoa asizame. Kwa hiyo, badala ya kushiriki desturi hiyo, tulimwuliza mgeni huyo ambaye alikuwa ametoka tu kulibusu ikiwa anaamini kwamba amepata zawadi ya ufasaha wa kusema au uwezo wa kurai.

“Hata kidogo!” akasema. Alikuwa amefanya hivyo kujifurahisha tu bila kufikiria maana ya tendo hilo. Kama wageni wengi wanaotembelea sehemu hii ya kihistoria, alitaka kuwa akiwaeleza rafiki zake kwamba alilibusu Jiwe la Blarney!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Alikuwa akizungumza kuhusu mwandishi maarufu Mwingereza wa wakati huo, William Shakespeare.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mnara wa Kasri ya Blarney