Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Paka Waliomo Hatarini Zaidi Duniani

Paka Waliomo Hatarini Zaidi Duniani

Paka Waliomo Hatarini Zaidi Duniani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

Uwezo wa kuona na wa kunyumbulika wa simba-mangu unajulikana sana. Wahispania husema kwamba mtu mwenye utambuzi ana “macho ya simba-mangu.” Kwa kusikitisha, simba-mangu wa Iberia (Lynx pardinus) hajawa maarufu kwa sababu ya uwezo wake wa kuona au utambuzi wake. Ametajwa kuwa “paka anayekabili hatari zaidi ulimwenguni.” *

Zamani, simba-mangu wa Iberia alipatikana kotekote nchini Ureno na Hispania na labda hata katika Milima ya Pyrenees huko Ufaransa. Siku hizi, vikundi vidogo vya simba-mangu vilivyotawanyika vinapatikana katika eneo la kusini-magharibi la Rasi ya Iberia. Hata hivyo, ni vikundi viwili tu vinavyoweza kuzaana, na idadi ya simba-mangu imepungua sana.

Kulingana na makadirio fulani, idadi ya simba-mangu wa Iberia ni chini ya 200. Ni nini kimesababisha upungufu huo? Wengine wanasema kwamba sababu kuu ni ukosefu mkubwa wa sungura ambao ni windo lake kuu. Sungura hao wamepungua kwa sababu ya magonjwa mbalimbali. Isitoshe, simba-mangu wengine wameuawa na wawindaji-haramu au wamegongwa na magari. Na makao yao yamepungua sana. Ripoti moja ya karibuni ya Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni inasema kwamba matatizo hayo yamefanya simba-mangu hao waliopungua watawanyike katika maeneo madogo.

Ingawa dola milioni 35 hivi zimetengwa kuhifadhi simba-mangu waliomo hatarini, hivi majuzi wataalamu walisema kwamba tatizo hilo ni “kubwa sana.” Kulingana na Nicolás Guzmán, msimamizi wa Mradi wa Kitaifa wa Kuhifadhi Simba-Mangu wa Iberia, kati ya wanyama hao wasiozidi 200 wanaopatikana msituni, ‘ni simba-mangu 22 hadi 32 tu wa kike wanaoweza kuzaa.’ Aliongeza kwamba ‘kuhifadhiwa kwa jamii hiyo kunawategemea.’ Inasikitisha kwamba hali hiyo inayowakumba simba-mangu wa Iberia, inawapata pia viumbe wengi sana maridadi wanaoishi duniani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Simba-mangu wa Iberia au wa Hispania ameorodheshwa kati ya viumbe waliomo hatarini zaidi katika orodha ya mimea na wanyama waliomo hatarini (Red List) inayotayarishwa na Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Viumbe na Mali za Asili.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Foto © Fernando Ortega

sos lynx