Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuwazoeza Watoto Wachanga Ni Muhimu Kadiri Gani?

Kuwazoeza Watoto Wachanga Ni Muhimu Kadiri Gani?

Kuwazoeza Watoto Wachanga Ni Muhimu Kadiri Gani?

FLORENCE alikuwa mwenye umri wa miaka 40 na alitamani sana kupata mtoto. Lakini alipokuwa mjamzito daktari alimwambia kwamba huenda akapata mtoto aliye na matatizo ya kujifunza. Hata hivyo, Florence hakukata tamaa. Mwishowe, alipata mtoto mwenye afya.

Muda mfupi baada ya kumzaa mwana wake anayeitwa Stephen, Florence alianza kumsomea na kuzungumza naye mara nyingi. Stephen alipoendelea kukua, walicheza pamoja, wakaenda matembezi, wakahesabu vitu, na kuimba pamoja. Florence anakumbuka hivi: “Hata nilipokuwa nikimwosha, tulicheza pamoja.” Hilo lilikuwa na matokeo mazuri.

Alipokuwa na umri wa miaka 14 hivi, Stephen alihitimu katika Chuo Kikuu cha Miami kwa shahada ya juu. Miaka miwili baadaye, akiwa na umri wa miaka 16, alimaliza masomo katika shule ya sheria, na kulingana na maelezo kuhusu maisha yake, akawa mwanasheria mwenye umri mdogo zaidi nchini Marekani. Mama yake, Dakt. Florence Baccus, ambaye zamani alikuwa mwalimu na mshauri, ametumia wakati mwingi kujifunza kuhusu kuwafundisha watoto wakiwa wachanga. Anasadiki kwamba maisha ya mtoto wake yalibadilika kwa sababu ya uangalifu na kichocheo alichompa alipokuwa mchanga.

Mjadala Kati ya Kurithi na Kufundishwa

Hivi karibuni, wataalamu wanaoshughulikia watoto wamejadiliana sana kuhusu ikiwa ukuzi wa mtoto unategemea mambo ambayo amerithi au mambo ambayo amefundishwa maishani. Watafiti wengi wanasadiki kwamba ukuzi wa mtoto unategemea mambo hayo mawili.

Dakt. J. Fraser Mustard, ambaye ni mtaalamu wa ukuzi wa watoto, anasema hivi: “Baada ya uchunguzi, tumejua kwamba ukuzi wa ubongo wa mtoto hutegemea mambo yanayotukia katika miaka yake ya mapema.” Pia, Profesa Susan Greenfield, anasema: “Tunajua kwamba sehemu ya ubongo inayowawezesha wachezaji wa fidla kusogeza vidole vya mkono wa kushoto, huwa imesitawi zaidi ya ile ya watu wengine.”

Watoto Wanahitaji Mazoezi Gani?

Kutokana na uchunguzi huo, mbali na kuwapeleka watoto wao kwenye shule bora za watoto wadogo, wazazi wengi hutumia pesa nyingi kuwapeleka kwenye shule za muziki na sanaa. Wengine wanaamini kwamba mtoto akijizoeza kufanya mambo yote akiwa mchanga, basi atafanya mambo yote akiwa mtu mzima. Shule zinazotoa elimu ya pekee na za kuwatunza watoto wachanga zinaongezeka. Wazazi wengine wanajitahidi juu chini ili kuwasaidia watoto wawe bora kuliko wengine.

Je, jitihada hizo hufanikiwa? Ijapokuwa jitihada hizo zinamsaidia mtoto afanye mambo mengi, zinamnyima jambo muhimu zaidi, yaani, kujifunza kwa kucheza kama kawaida. Walimu wanasema kwamba kucheza kama kawaida humchochea mtoto kubuni mambo na kusitawisha ustadi wa kuchangamana na watu, ustadi wa kiakili, na wa kihisia.

Baadhi ya wataalamu wanaona kwamba michezo iliyopangiwa na wazazi hutokeza tatizo jipya kwani inawafanya watoto wafadhaike, wawe na matatizo ya kihisia, washindwe kulala, na kupatwa na maumivu. Mtaalamu mmoja anasema kwamba watoto hao wanapobalehe, wengi wao huwa hawajasitawisha ustadi wa kushughulika na matatizo nao huwa “wachovu, wasiotaka kufanya urafiki, na waasi.”

Hivyo, wazazi wengi hawajui la kufanya. Wanataka kuwasaidia watoto wao kutumia vipawa vyao kikamili. Hata hivyo, wanaona kwamba haifai kuwalemea watoto wao wachanga. Je, inawezekana kuwa na usawaziko? Uwezo wa mtoto ni mkubwa kadiri gani, nao unaweza kusitawishwaje? Wazazi wanahitaji kufanya nini ili kuwasaidia watoto wao wafanikiwe? Makala zinazofuata zitazungumzia maswali hayo.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Ukuzi wa ubongo wa mtoto hutegemea mambo yanayompata utotoni

[Picha katika ukurasa wa 4]

Kucheza humchochea mtoto awe mbunifu na kusitawisha ustadi wake