Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maktaba Funguo za Kupata Ujuzi

Maktaba Funguo za Kupata Ujuzi

Maktaba Funguo za Kupata Ujuzi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

MAKTABA zimeitwa “mojawapo ya nguzo za ustaarabu.” Kichapo World Book Encyclopedia kinasema kwamba maktaba huchangia sehemu muhimu zaidi ya utamaduni na teknolojia ya wanadamu. Mshairi Mjerumani Goethe aliziita kumbukumbu za wanadamu.

Ni maktaba zipi ambazo zimekuwa miongoni mwa ‘nguzo muhimu za ustaarabu’? Ni kitabu gani ambacho kimekuwa na uvutano mkubwa zaidi katika maktaba na katika kusambazwa kwa elimu? Na maktaba kubwa zaidi leo zina vitabu vingapi? Ili kujibu swali la kwanza, na tuwazie kwamba tuliishi nyakati za zamani na tutembelee mojawapo ya maktaba ya zamani zaidi.

‘Ensaiklopedia ya Kale ya Ujuzi wa Mwanadamu’

Wazia kwamba uko katika nchi ya Mashariki ya Kati ambayo leo ni Iraq. Ni mwaka wa 650 K.W.K. Uko katika jiji la Ninawi lenye kuta ndefu (karibu na Mosul ya leo). Mbele yako kuna jengo kubwa la kifalme la Mfalme Ashurbanipali, mtawala wa Ashuru, Misri, na Babiloni. * Ukiwa umesimama karibu na mlango wa jumba hilo unawaona wanaume wakikokota magudulia ya udongo ndani ya jumba hilo. Wanaume hao wamerudi tu kutoka sehemu za mbali za ufalme wa Ashuru kwani wanajitahidi kukusanya kitabu chochote kinachozungumzia masuala ya kijamii, kitamaduni, na desturi mbalimbali za kidini za watu wanaoishi chini ya Mfalme Ashurbanipali. Unapofungua moja ya magudulia hayo unaona yamejaa mabamba ya udongo yenye umbo la mstatili na ambayo yana upana wa sentimeta 8 na urefu wa sentimeta 10 hivi.

Unamfuata mwanamume mmoja ndani ya jumba hilo na kuwaona waandishi wenye kalamu za mfupa wakichora maumbo kama ya kabari katika mabamba madogo ya udongo wenye unyevu. Wanatafsiri hati za lugha ya kigeni katika Kiashuri. Baadaye, mabamba hayo yataokwa katika joko, na hivyo kuyahifadhi kabisa maandishi hayo. Maandishi hayo yanawekwa katika vyumba vyenye rafu nyingi ambazo zina mamia ya magudulia. Kwenye miimo ya milango ya vyumba hivyo, kuna mabamba yenye habari kuhusu maandishi yaliyohifadhiwa katika kila chumba. Mabamba ya udongo zaidi ya 20,000 katika maktaba hiyo yana habari kuhusu masuala ya biashara, desturi za kidini, sheria, historia, tiba, na fiziolojia ya binadamu na wanyama, nayo hufanyiza kile ambacho msomi mmoja alieleza kuwa “ensaiklopedia ya ujuzi wa mwanadamu.”

Maktaba Nyingine Kabla na Baada ya Ile ya Ninawi

Kulikuwa na maktaba nyingine kubwa kabla ya ile ya Ashurbanipali huko Ninawi. Mfalme Hammurabi alijenga maktaba katika jiji la Borsippa, la Babiloni miaka elfu moja kabla ya Ashurbanipali. Ramesesi wa Pili alianzisha maktaba maarufu katika jiji la Thebesi, Misri, zaidi ya miaka 700 kabla ya Ashurbanipali. Lakini maktaba ya Ashurbanipali ndiyo maktaba “kubwa zaidi katika ulimwengu wa kale” kwa sababu ilikuwa na habari za aina nyingi na rekodi nyingi sana. Miaka 350 ilipita kabla maktaba nyingine kubwa zaidi kujengwa.

Maktaba hiyo kubwa zaidi ilijengwa na Tolemi wa Kwanza Soteri, mmoja wa majenerali wa Aleksanda Mkuu, karibu mwaka wa 300 K.W.K. Ilijengwa katika jiji la bandarini la Aleksandria, Misri, na wasimamizi wa maktaba hiyo walijitahidi kukusanya nakala nyingi za maandishi yaliyokuwapo ulimwenguni. * Kulingana na mapokeo, wale wasomi 70 hivi walianza kutafsiri Maandiko ya Kiebrania katika Kigiriki huko Aleksandria. Baadaye, tafsiri hiyo iliitwa Septuajinti ya Kigiriki na ilitumiwa sana na Wakristo wa mapema.

Maktaba za Nchi za Mashariki

Ashurbanipali alipokuwa akiboresha maktaba yake, ukoo wa wafalme walioitwa Chou walikuwa wakitawala China. Wakati wa utawala huo, kuanzia mwaka wa 1122 K.W.K. hadi 256 K.W.K., mkusanyo wa vitabu vilitokezwa vilivyokuja kuitwa Vitabu Bora Sana Vitano. Vilitia ndani kitabu kimoja cha kutabiri wakati ujao, mkusanyo wa hotuba za watawala wa mapema, mashairi, maagizo kuhusu sherehe na mila za kidini, na historia kuhusu jimbo la Lu kuanzia 722 K.W.K. hivi hadi 481 K.W.K., kitabu cha mwisho kikisemekana kuwa kiliandikwa na mwanafalsafa Mchina Confucius. Vile Vitabu Bora Sana Vitano pamoja na maandishi mengi kuvihusu yaliathiri sana kufikiri kwa Wachina na kuweka msingi wa maktaba za kifalme na za kibinafsi kwa zaidi ya milenia mbili.

Huko Japani, Hojo Sanetoki, mshiriki wa familia ya samurai iliyokuwa ikitawala, alianzisha maktaba mnamo 1275 katika makao ya familia yake huko Kanazawa (sasa ni sehemu ya Yokohama). Alijaribu kukusanya vitabu vyote vya Kichina na vya Kijapani vilivyopatikana. Ingawa vitabu vimepungua, mkusanyo huo ungali upo.

Biblia, Maktaba za Nyumba za Watawa, na Utamaduni wa Nchi za Magharibi

Kitabu A History of Libraries in the Western World, kinasema kwamba “nguvu za maandishi yaliyopigwa chapa, na umuhimu wa maktaba, unaonekana wazi katika kuinuka, kuenea, na kudumu kwa dini ya Kikristo.” Kuna uhusiano gani kati ya kusitawi kwa maktaba na kuenea kwa Ukristo?

Baada ya Milki ya Roma kuvunjika na vichapo vilivyokuwa katika maktaba zake kubwa kuharibiwa au kutawanywa, makao ya watawa wa Jumuiya ya Wakristo yaliibuka kotekote Ulaya na kukusanya vichapo vilivyobaki vya maktaba hizo za kale. Jambo moja muhimu lililofanywa katika makao hayo ya watawa lilikuwa kunakili kwa mkono hati za Biblia na hati nyinginezo. Kwa mfano, watawa wa Mtakatifu Benedict waliongozwa na “Sheria ya Mtakatifu Benedict,” iliyowaamuru wasome na kunakili vitabu hivyo.

Maktaba huko Constantinople zilihifadhi na kutokeza nakala za hati za kale ambazo mwishowe zilipatikana Italia. Inaaminika kwamba hati hizo zilichangia sehemu kubwa sana katika kuanzisha Kipindi cha Mwamko. Mwanahistoria Elmer D. Johnson anasema: “Hatuwezi kupuuza sehemu iliyotimizwa na maktaba ya makao ya watawa katika kuhifadhi utamaduni wa nchi za Magharibi. Kwa miaka elfu moja hivi, ilikuwa kituo cha elimu cha Ulaya, na kama haingalikuwapo ustaarabu wa nchi za magharibi usingalijulikana.”

Kazi ya kunakili Biblia ilisaidia kudumisha “kituo cha elimu cha Ulaya” katika kipindi hicho. Wakati wa kipindi cha Marekebisho Makubwa ya Kidini huko Ulaya, tamaa ya kusoma Biblia iliwachochea watu wa kawaida kujifunza kusoma na kuandika. Kitabu The Story of Libraries kinasema: “Wazo la kwamba kila mtu katika jamii anapaswa kuwa na elimu ya kumwezesha angalau kusoma Biblia lilianza wakati wa yale Marekebisho Makubwa ya Kiprotestanti. Mizozo ya kidini ilipoongezeka, uwezo wa kusoma vitabu vingi vya kidini ulikuwa muhimu. Hilo lilihitaji mtu awe na uwezo wa kusoma na pia aweze kupata vitabu hivyo.”

Kwa hiyo, Biblia ilitimiza fungu muhimu katika kueneza maktaba na uwezo wa kusoma na kuandika kotekote katika nchi za Magharibi. Kisha mashini za kuchapisha zilipovumbuliwa, maktaba kubwa za kibinafsi na za kitaifa zenye vitabu vilivyo na habari mbalimbali zilianza kutokea kotekote Ulaya, na hatimaye, katika sehemu nyingine za ulimwengu.

Maktaba za Karne ya 21

Leo maktaba fulani zina vitabu vingi sana. Wazia ukisimama karibu na rafu ya vitabu yenye urefu wa kilometa 850 na yenye vitabu zaidi ya milioni 29. Huo ndio ukubwa unaokadiriwa wa maktaba kubwa zaidi ulimwenguni, Maktaba ya Congress, iliyoko Marekani. Mbali na vitabu, maktaba hiyo ina kaseti na video milioni 2.7 hivi, picha milioni 12, ramani milioni 4.8, na hati milioni 57. Kila siku maktaba hiyo huongezwa vitu 7,000!

Maktaba ya Uingereza iliyoko London ndiyo ya pili kwa ukubwa, nayo ina vitabu zaidi ya milioni 18. Maktaba ya Kitaifa ya Urusi iliyoko Moscow ina vitabu milioni 17, na lina magazeti 632,000 hivi ya kila mwaka. Maktaba ya Kitaifa ya Ufaransa, mojawapo ya maktaba za zamani zaidi Ulaya, ina vitabu milioni 13. Kwa kuongezea, kitabu Library World Records kinasema: “Maktaba ya kitaifa ya Ufaransa ilikuwa maktaba ya kwanza kuingiza vichapo vyake vingi katika Intaneti vikiwa vizima-vizima.” Kwa wale wanaoweza kutumia kompyuta, Intaneti imekuwa njia rahisi zaidi ya kupata ujuzi mwingi.

Kuliko wakati mwingine wowote, habari ambayo watu wanaweza kupata inaongezeka sana. Inakadiriwa kwamba habari yote ambayo wanadamu wanayo huongezeka mara mbili baada ya kila miaka minne na nusu. Nchini Marekani peke yake, zaidi ya vitabu vipya 150,000 huchapishwa kila mwaka.

Kwa hiyo, maoni ya Mfalme Sulemani wa kale aliyekuwa pia msomi na mwandishi yanafaa sana leo. Aliandika hivi: “Hakuna mwisho wa kutungwa kwa vitabu vingi, na kushughulika navyo sana huuchosha mwili.” (Mhubiri 12:12) Hata hivyo, maktaba zinapotumiwa vizuri zitaendelea kuwa kile ambacho Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni huita “funguo za kupata ujuzi zilizo karibu nasi.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Ashurbanipali ambaye anadhaniwa kuwa Asenapari anayetajwa katika Biblia kwenye Ezra 4:10, aliishi wakati mmoja na Mfalme Manase wa Yuda.

^ fu. 10 Ili kupata habari zaidi kuhusu maktaba ya kale na ya sasa ya Aleksandria, ona toleo la Amkeni! la Januari 8, 2005.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]

Daraka la Msimamizi wa Maktaba

Ikiwa huwezi kupata kitabu unachohitaji katika orodha ya vitabu vya maktaba, usiwe na wasiwasi, mwulize msimamizi. Mara nyingi ujuzi wake huwa muhimu. Roderick, ambaye amekuwa msimamizi wa maktaba kwa miaka 20 anasema: “Mara nyingi watu huogopeshwa na maktaba na wasimamizi wa maktaba. Mara nyingi wao husema, ‘Huenda swali langu ni la kipumbavu, lakini . . . ’ Lakini, hakuna maswali ya kipumbavu. Ustadi wa msimamizi wa maktaba hujulikana anapokuonyesha unachohitaji hata kama hujui kitabu unachotafuta.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]

Tarakimu Hizi Zinamaanisha Nini? 225.7

Mfumo wa Dewey wa Desimali

Maktaba nyingi hutumia mfumo wa Dewey wa desimali ambao huwa mfuatano wa tarakimu zilizochapishwa katika orodha zao na katika sehemu ya kando ya vitabu vyao. Melvil Dewey, Mmarekani mashuhuri aliyekuwa msimamizi wa maktaba, alichapisha mfumo wake kwa mara ya kwanza mnamo 1876. Mfumo huo hutumia tarakimu kuanzia 000 hadi 999 ili kupanga vitabu vyote kulingana na habari ambayo vinazungumzia, na kuvipanga katika vikundi kumi vikuu:

000-099 Habari ya jumla

100-199 Falsafa na saikolojia

200-299 Dini

300-399 Sayansi za kijamii

400-499 Lugha

500-599 Sayansi za asili na hisabati

600-699 Teknolojia (sayansi za kiufundi)

700-799 Sanaa

800-899 Fasihi na ufasaha wa kusema

900-999 Jiografia na historia

Kila kikundi kikuu hugawanywa katika vikundi vidogo kumi na kupewa habari hususa zinazohusiana na kikundi hicho. Kwa mfano, Biblia ina tarakimu yake, yaani, nambari 220 kati ya kile kikundi kinachotambuliwa kwa nambari 200 (Dini). Habari hususa kuhusu Biblia hugawanywa tena. Namba 225 hutambulisha “Agano Jipya” (Maandiko ya Kigiriki). Nambari za ziada huongezewa ili kutambulisha aina ya kitabu:

01 Falsafa na nadharia

02 Maandishi mbalimbali

03 Kamusi, ensaiklopedia, konkodansi

04 Habari za pekee

05 Vichapo vya mfululizo

06 Usimamizi na utaratibu wa kufanya mambo

07 Elimu, utafiti, habari zinazohusiana

08 Historia na ufafanuzi kuhusu watu mbalimbali

09 Habari za historia

Kwa hiyo, ensaiklopedia kuhusu Biblia nzima ingekuwa na namba 220.3, nayo maelezo kuhusu Maandiko ya Kigiriki yangekuwa na namba 225.7.

Maktaba ya Congress hutumia mfumo kama huo lakini maktaba hiyo hutumia mchanganyiko wa herufi na nambari. Pia vitabu vingi hutumia herufi na nambari ili kumtambulisha mwandishi. Katika nchi nyingine, mifumo mingine tofauti ya kuorodhesha vitabu hutumiwa.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mfalme Ashurbanipali wa Ashuru, ambaye maktaba yake ilikuwa na mabamba ya kikabari ya udongo, mwaka wa 650 K.W.K.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Maktaba ya Uingereza, London, Uingereza

[Picha katika ukurasa wa 18]

Maktaba iliyo katika makao ya watawa, huko Uswisi, 1761

[Picha katika ukurasa wa 19]

Maktaba ya Aleksandria, Misri, karibu mwaka wa 300 K.W.K.

[Hisani]

From the book Ridpath’s History of the World (Vol. II)

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Maktaba ya Congress, Marekani, iliyo kubwa zaidi ulimwenguni

[Hisani]

From the book Ridpath’s History of the World (Vol. IX)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Top left and bottom photos: Erich Lessing/ Art Resource, NY; tablet: Photograph taken by courtesy of the British Museum