Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Linda Ngozi Yako!

Linda Ngozi Yako!

Linda Ngozi Yako!

“Watu hawatambui hatari kubwa inayosababishwa na jua . . . na jinsi linavyoweza kudhuru chembe za urithi za ngozi. Madhara ya muda mrefu yanaweza kutokeza kansa ya ngozi baadaye.” —Dakt. Mark Birch-Machin, mtaalamu wa kansa ya ngozi.

NGOZI ndicho kiungo kikubwa zaidi mwilini. Ngozi ya mwanamume ina urefu wa meta 1.8 za mraba na ile ya mwanamke ina urefu wa meta 1.6 za mraba. Ina vipokezi ambavyo hufanya mtu ahisi uchungu, mguso, na halijoto. Ndicho kiungo cha kwanza kukinga mwili hasa dhidi ya joto, baridi, majeraha, na vilevile sumu, kemikali, na vichafuzi. Huzuia umajimaji usiingie au kutoka mwilini. Hata hivyo, ngozi inaweza kudhuriwa na jua. Lakini je, kwani nuru ya jua si muhimu kwa uhai?

Ndiyo, ni muhimu. Mimea ambayo hutegemeza uhai wetu huhitaji nuru ya jua ili ikue. Isitoshe, kiasi kidogo cha nuru ya jua huchochea mwili kutokeza vitamini D, ambayo huvunja-vunja kalisi, na kufanya mifupa iwe yenye nguvu. Lakini hiyo haimaanishi kwamba kwa kuwa kiasi kidogo cha jua kinafaa, kiasi kikubwa kitafaa zaidi. Jua hutokeza mnururisho wa miale ya urujuanimno inayoweza kuharibu ngozi kabisa. Jambo hilo husababisha ngozi ipatwe na makunyanzi mapema.

Kitabu Saving Your Skin kinaonya kuhusu hatari kubwa zaidi: “Miale ya urujuanimno huharibu DNA [chembe za urithi ambazo hudhibiti utendaji wa chembe, kama vile kugawanyika kwa chembe], hudhoofisha mfumo wa kinga na inaweza kuchochea kemikali mwilini ambazo hutokeza kansa.” Neno “kansa” huogopesha. Lakini kansa ya ngozi imeenea kadiri gani? Je, tunapaswa kuhangaishwa na jambo hilo?

Kansa ya Ngozi Ni Tatizo Kubwa Leo

Kichapo The Merck Manual kinasema kwamba hiyo ndiyo kansa inayopata watu wengi sana ulimwenguni. Nchini Marekani, mtu 1 kati ya kila watu 6 hadi 7 hupatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi. Lakini idadi ya watu wanaopatwa na kansa hiyo inaongezeka. Katika kitabu The Skin Cancer Answer, Dakt. I. William Lane anasema: “Sasa inakadiriwa kwamba asilimia 50 ya watu ambao hufikisha umri wa miaka 65 watapatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi.” Kulingana na Taasisi ya Magonjwa ya Ngozi ya Marekani, kansa ya ngozi inayoathiri chembe za ndani za ngozi husababisha vifo 7,500 hivi kila mwaka nchini humo na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Si rahisi kwa watu wenye ngozi nyeusi kupatwa na kansa ya ngozi, lakini wao pia wamo hatarini.

Kwa nini kansa ya ngozi imeenea hivyo? Ingawa huenda ikasababishwa na mambo mengi kama vile mwinuko kutoka usawa wa bahari, latitudo, kiasi cha mawingu, na hali ya tabaka la ozoni, huenda kisababishi kikuu kikawa kupigwa na jua kwa muda mrefu. Mitindo ya maisha imebadilika. Imekuwa rahisi kwa watu wengi wanaofanya kazi ofisini kwenda likizo kwenye fuo na kufurahia tafrija kama vile kupanda mlima na kuteleza kwenye barafu. Mitindo ya mavazi imebadilika. Ingawa zamani wanaume na wanawake walivaa nguo ndefu za kuogelea, siku hizi nguo za kuogelea hazifuniki sehemu kubwa ya mwili. Kwa sababu hiyo kansa ya ngozi imeongezeka. Huenda watu walioishi jangwani kama vile Wabedui walijua jambo hilo na ndio sababu walivalia kanzu ndefu na vilemba.

Kansa ya Ngozi Ni Hatari!

Aina tatu za kansa ya ngozi ambazo huwapata sana watu ni kansa inayoathiri chembe za katikati za ngozi, kansa ya chembe za juu za ngozi, na kansa ya chembe za ndani za ngozi ambayo ni hatari sana. Kansa ya chembe za katikati na za juu ya ngozi huanza katika tabaka la juu la ngozi ambalo lina unene wa milimita moja tu kwa wastani. Yaonekana kansa hizo ambazo si hatari sana husababishwa na kupigwa na jua kwa muda mrefu sana, kama vile watu wanaofanya kazi chini ya jua, nazo hutokea hasa kwenye sehemu za mwili zinazopigwa na jua kama vile uso na mikono. * Aina hizo za kansa huelekea kuanza kama uvimbe mdogo kwenye ngozi ambao hukua, huvuja damu mara nyingi na hauponi kabisa. Unaweza kuanza kuenea na kuathiri tishu zinazouzunguka. Asilimia 75 hivi ya kansa za ngozi huwa kansa zinazoathiri chembe za katikati za ngozi. Ingawa kansa inayoathiri chembe za juu za ngozi si ya kawaida, huenda ikaenea na kuathiri sehemu nyingine za mwili. Ni muhimu kansa za aina hiyo zingunduliwe mapema kwani ingawa zinaweza kutibiwa, zikiachwa kwa muda mrefu bila kutibiwa zinaweza kusababisha kifo.

Kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi ambayo hupata asilimia 5 tu ya watu wanaougua kansa ya ngozi, pia huanza katika sehemu ya juu ya ngozi. Inaonekana kwamba mojawapo ya visababishi vikuu vya aina hii ya kansa ni kujianika juani kwa vipindi virefu sana kama vile watu wanaofanya kazi za ofisini hufanya wanapoenda likizo. Asilimia 50 hivi ya aina hiyo ya kansa hutokana na mabaka meusi hasa kwenye sehemu ya juu ya mgongo na sehemu ya chini ya miguu.

Aina hii ya kansa ndiyo hatari zaidi kwa kuwa isipotibiwa mapema, inaweza kuvamia tabaka la ndani la ngozi, ambako kuna mishipa ya damu na limfu. Kuanzia hapo, inaweza kuenea haraka. Mtalaamu wa matibabu ya uvimbe Dakt. Larry Nathanson anasema: “Jambo la kushangaza ni kwamba kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi inaweza kutibiwa kwa urahisi inapogunduliwa mapema. Kwa upande mwingine, inapoenea haiwezi kutibiwa kwa dawa au mnururisho.” Kwa kweli, ni asilimia 2 au 3 tu ya wagonjwa wenye kansa hiyo iliyoenea ambao huweza kuishi kwa miaka mitano. (Ona dalili za mapema za kansa hiyo kwenye sanduku katika ukurasa wa 7.)

Ni nani wanaoweza kupata kansa ya ngozi? Mbali na watu ambao wamewahi kupigwa na jua kwa muda mrefu sana, au wale wanaojianika juani kwa vipindi virefu sana, wale walio na ngozi nyeupe, nywele na macho ya rangi hafifu, wenye mabaka na madoadoa, na wale ambao mtu fulani katika familia yao amekuwa na ugonjwa huo, wanaweza kuupata. Si rahisi kwa watu wenye ngozi nyeusi kupatwa na kansa ya ngozi. Je, hii inamaanisha kwamba kadiri ngozi yako inavyounguzwa na jua na kuwa nyeusi ndivyo inavyokuwa vigumu kupatwa na kansa ya ngozi? Sivyo, kwa sababu ingawa ngozi hujigeuza rangi na kuwa nyeusi ili kujikinga na mnururisho wa miale ya urujuanimno, inapofanya hivyo hiyo huathirika, na inapoathirika mara nyingi kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kupata kansa ya ngozi.

Kutibu Kansa ya Ngozi

Ikitegemea aina ya uvimbe, mahali ulipo, ukubwa wake, na matibabu ya wakati uliopita, kuna njia mbalimbali za kuutibu: kukata mahali palipoathirika, kukwangua, kuchoma kwa sindano ya umeme, upasuaji wa kugandisha uvimbe, na matibabu ya kutumia miale. Ni vigumu kuondoa chembe zote zilizoathiriwa na kansa. Upasuaji wa Mohs unaofanywa kwa kutumia darubini ni wenye matokeo katika kuondoa kansa inayoathiri chembe za katikati na za juu ya ngozi (inaweza kutibu asilimia 95 hadi 99), huku ukihifadhi kiasi kikubwa cha tishu ambazo hazijaathiriwa na kuacha makovu yasiyoonekana kwa urahisi. Vyovyote vile, ni lazima tishu nyingine zibandikwe.

Taasisi ya Kitaifa ya Uzee ya Marekani inasema hivi: “Aina zote za kansa ya ngozi zinaweza kutibiwa ikiwa zinagunduliwa mapema na kutibiwa kabla ya kuenea.” Kwa hiyo, ni muhimu kugunduliwa mapema. Lakini ni nini kinachoweza kufanywa ili kuzuia kansa ya ngozi?

Jifunze Kuhusu Jinsi ya Kujikinga na Madhara ya Jua

Ni muhimu kujifunza tangu utotoni kuhusu kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kulingana na Taasisi ya Kansa ya Ngozi, ‘watu wengi hupigwa na asilimia 80 hivi ya kiasi cha jua wanachohitaji maishani kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Kuunguzwa sana na jua na kupatwa na malengelenge mara moja tu utotoni, huzidisha maradufu uwezekano wa kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi baadaye maishani.’ Hii ni kwa sababu kansa ya ngozi inaweza kuchukua miaka 20 au zaidi kukua. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 8 ili kupata madokezo ya kujikinga na madhara ya kupigwa na jua.)

Australia ina kiwango cha juu cha visa vya ugonjwa wa kansa ya ngozi, hasa ile inayoathiri chembe za ndani za ngozi. * Hii ni kwa sababu wakazi wengi wa nchi hiyo ambao walihama kutoka Ulaya Kaskazini wana ngozi yenye rangi hafifu, na wengi wao huishi pwani yenye fuo zenye jua. Uchunguzi waliofanyiwa wahamiaji hao unadokeza kwamba wale wanaohamia Australia wakiwa wachanga hukabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ngozi za ndani, jambo linaloonyesha umuhimu wa kujifunza tangu utotoni kuhusu madhara ya kupigwa na jua. Serikali ya Australia imeanzisha kampeni kali ya kuwafunza watu kuhusu hatari za jua kwa kuwaambia wavae t-shati, kofia, na kujipaka losheni ya kujikinga na jua. Mabadiliko hayo madogo katika mtindo wa maisha yamekuwa na matokeo makubwa katika kuzuia kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi kati ya vijana nchini humo.

Losheni ya kujikinga na jua inayofaa ni ile inayoweza kukinga miale ya mnururisho ya UVA na UVB. Ni muhimu kujipaka losheni hiyo hata siku zenye mawingu mengi kwa kuwa asilimia 85 ya mnururisho wa miale ya urujuanimno inaweza kupenya mawingu. Pia miale hiyo inaweza kupenya majini. Wataalamu fulani wanapendekeza losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) ya angalau namba 15. Ili kujua losheni hiyo inaweza kukukinga kwa kiasi gani, hesabu dakika ambazo kwa kawaida wewe huchukua kuunguzwa na jua kisha uzizidishe kwa 15. Mtu anapaswa kujipaka losheni hiyo angalau baada ya kila saa mbili, lakini kufanya hivyo hakuzidishi maradufu muda ambao utakuwa umekingwa na jua.

Isitoshe, kitabu The Skin Cancer Answer kinaonya kwamba hupaswi kufikiri kwamba uko salama eti kwa sababu tu unatumia losheni ya kujikinga na jua. Hakuna losheni ya kujikinga na jua inayoweza kuzuia kikamili kuunguzwa na jua, wala kuzuia kansa ya ngozi. Kwa kweli, kutumia losheni kama hizo kunaweza kuongeza uwezekano wa kupatwa na kansa ya ngozi kwa njia isiyo ya moja kwa moja ikiwa kuzitumia kutafanya ukae muda mrefu zaidi kwenye jua. Kitabu hicho kinasema: “Njia pekee ya kujikinga ni kufuata madokezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kuvaa mavazi ya kujikinga na kukaa ndani ya nyumba wakati jua linapokuwa kali, huonwa kuwa mbinu ‘zenye matokeo’ za kujikinga na kansa ya ngozi.”

Namna gani kujigeuza rangi kwa kutumia taa na vitanda vinavyotokeza mnururisho wa jua ukiwa ndani ya nyumba? Inakadiriwa kwamba kutumia dakika 20 tu katika chumba kama hicho, ni sawa na kujianika kwenye jua kwa saa nne hivi. Ilidhaniwa kwamba kujaribu kugeuza rangi ya ngozi ndani ya nyumba ni salama kwa sababu mnururisho wa miale ya UVA uliotumiwa hasa, ulionekana kuwa hauunguzi ngozi. Lakini kitabu The Skin Cancer Answer kinasema: “Sasa inajulikana kwamba miale ya UVA hupenya ndani zaidi katika ngozi kuliko miale ya UVB, inaweza kusababisha kansa ya ngozi, na huenda ikadhoofisha mfumo wa kinga.” Uchunguzi mmoja ulioripotiwa katika toleo la kimataifa la The Miami Herald ulionyesha kwamba wanawake ambao huenda kwenye vyumba vya kugeuza rangi ya ngozi mara moja kwa mwezi au zaidi “waliongeza uwezekano wao wa kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi kwa asilimia 55.”

Hivyo, ni muhimu kujifunza jinsi ya kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kumbuka kwamba ukiunguzwa na jua leo, huenda ukapatwa na kansa ya ngozi miaka 20 au zaidi baadaye. Watu fulani wamekabilianaje na kansa ya ngozi, na ni nini kimewasaidia kufanya hivyo?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Mnururisho wa miale ya urujuanimno unaweza kuharibu chembe za mfumo wa kinga wa ngozi zilizo katika sehemu ya juu ya ngozi, ambazo ni muhimu katika kuzuia magonjwa. “Kwa hiyo, wanasayansi fulani wanaamini kwamba mfumo wa kinga unapoacha kufanya kazi, kansa ya ngozi inaweza kutokea,” chasema kitabu The Skin Cancer Answer.

^ fu. 19 Kulingana na Baraza la Kansa la New South Wales, “Mwaustralia mmoja kati ya wawili atapatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi maishani mwake.” Huko Queensland, Australia, mnamo mwaka wa 1998, mtu 1 kati ya watu 15 alikabili hatari ya kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

DALILI KUU ZA KANSA HATARI

1. Mara nyingi uvimbe ambao haujakomaa wa kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi huwa na pande mbili ambazo hazitoshani. Mabaka ya kawaida huwa ya mviringo na pande zinazotoshana.

2. Mara nyingi uvimbe ambao haujakomaa wa kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi huwa na kingo zenye maumbo au mikato isiyotoshana. Mabaka ya kawaida huwa na kingo laini zilizotoshana.

3. Dalili za kwanza za kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi ni mabaka yenye rangi ya kahawia, hudhurungi, au nyeusi. Kansa hiyo inapoenea, huenda rangi hizo zikabadilika na kuwa nyekundu, nyeupe, na buluu. Mabaka ya kawaida huwa ya rangi ya kahawia.

4. Uvimbe ambao haujakomaa wa kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi huwa mkubwa zaidi kuliko mabaka ya kawaida nao huwa na kipenyo cha zaidi ya milimita sita.

[Hisani]

Chanzo: Taasisi ya Kansa ya Ngozi

Skin samples: Images courtesy of the Skin Cancer Foundation, New York, NY, www.skincancer.org

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

MADOKEZO YA JINSI YA KULINDA NGOZI YAKO

1. Usikae kwenye jua sana hasa kati ya 4:00 asubuhi na saa 10:00 jioni, wakati kuna mnururisho mwingi wa miale hatari ya urujuanimno.

2. Chunguza ngozi yako kuanzia wayo hadi utosini angalau mara moja kila miezi mitatu.

3. Unapokuwa nje, tumia losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) namba 15 au zaidi. Jipake losheni nyingi dakika 30 kabla ya kujianika juani na baada ya kila saa mbili. (Watoto walio chini ya umri wa miezi sita hawapaswi kupakwa losheni ya kujikinga na jua.)

4. Wafunze watoto wako jinsi ya kujikinga na jua wakiwa wangali wachanga, kwa kuwa madhara ambayo husababisha kansa ya ngozi kwa watu wazima huanza utotoni.

5. Vaa nguo za kujikinga kama vile suruali ndefu, shati zenye mikono mirefu, kofia pana, na miwani inayoweza kuzuia miale ya urujuanimno.