Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nyumba Safi—Kila Mtu Ana Sehemu Yake

Nyumba Safi—Kila Mtu Ana Sehemu Yake

Nyumba Safi—Kila Mtu Ana Sehemu Yake

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Mexico

INAPENDEZA sana kuishi katika mazingira safi. Hata hivyo, takataka na uchafu zinapoongezeka mijini, inakuwa vigumu zaidi kudumisha mazingira yetu yakiwa safi na nadhifu.

Mabaraza ya jiji hujaribu kusafisha barabara kwa kuzoa takataka, hata hivyo, takataka hurundamana katika sehemu fulani ambako hazivutii na kuwa tisho kwa afya ya umma. Takataka zinaporundamana zinaweza kuongeza idadi ya panya, mende, na viumbe wengine wanaoweza kusababisha magonjwa. Je, kuna lolote unaloweza kufanya kuhusu jambo hilo? Bila shaka, hakikisha kwamba nyumba na mazingira yako ni safi na nadhifu.

Mtazamo wa Akili Unaofaa

Watu wengine hufikiri kwamba watu maskini hawawezi kuishi katika nyumba na mazingira safi. Hata hivyo, si lazima iwe hivyo. Kwa kweli, kukosa pesa kunaweza kufanya iwe vigumu kudumisha mazingira yetu yakiwa safi. Lakini methali moja ya Kihispania inasema, “umaskini na usafi hazipingani.” Kwa upande mwingine, kuwa na pesa hakumaanishi kwamba mtu atadumisha mazingira yake yakiwa safi.

Kudumisha usafi ndani na nje ya nyumba hutegemea mtazamo wa akili ambao humchochea mtu atende. Kwa kweli, kudumisha nyumba ikiwa safi hutegemea mtazamo wa akili wa familia yote. Kwa sababu hiyo, inafaa tuchunguze yale tunayoweza kufanya ili kuchangia usafi wa nyumba zetu, kutia ndani ujirani wetu.

Ratiba ya Usafi

Inaonekana kwamba kazi ya akina mama haiishi. Licha ya kupika na kuwatayarisha watoto kwa ajili ya shule, lazima wasafishe nyumba ndani na nje. Je, umeona kwamba mara nyingi mama ndio huokota nguo chafu au vitu vingine ambavyo watoto huacha katika vyumba vyao? Ratiba nzuri ya usafi inayohusisha kila mtu katika familia inaweza kumpunguzia mama kazi.

Wake fulani huwa na ratiba ya kushughulikia na kusafisha vitu fulani kila siku, kusafisha sehemu fulani za nyumba mara moja kwa juma, na nyingine mara moja kwa mwezi. Hata kuna vitu vinavyoweza kuratibiwa visafishwe mara moja kwa mwaka. Kwa mfano, katika Makao ya Betheli, kwenye ofisi za tawi za Mashahidi wa Yehova katika kila nchi, sehemu za kuwekea nguo na kabati husafishwa mara moja kwa mwaka. Huo ni wakati wa kutupa vitu visivyotumiwa na kupanga kabati hizo. Pia kuna ratiba ya kawaida ya kusafisha kuta.

Ili kila mtu awe na afya nzuri, kuna sehemu fulani katika nyumba ambazo zinapaswa kudumishwa zikiwa safi, kama vile choo na bafu. Ingawa zinapaswa kusafishwa kidogo kila siku, sehemu hizo zinapaswa kusafishwa kabisa labda mara moja kwa juma ili kuzuia bakteria zisiongezeke. Wengine hufikiri kwamba madoa ambayo huwa katika bakuli la choo hayawezi kuondolewa. Lakini, kuna nyumba ambazo choo huwa safi kabisa na hung’aa. Unahitaji tu kusafisha kwa ukawaida na kutumia sabuni zinazofaa.

Jikoni pia kunahitaji kusafishwa vizuri. Ingawa kila siku mtu husafisha vyombo, jiko, na meza, mara kwa mara, labda mara moja kwa mwezi, ni muhimu kusafisha mahali ambapo jiko na vifaa vingine vya kupikia huwekwa. Kusafisha kabati na stoo kwa ukawaida kutazuia mende na wadudu wengine wanaoweza kudhuru wasifanyize makao humo.

Ushirikiano wa Familia

Wazazi fulani wamewawekea watoto wao sheria na kuwazoeza kwamba kila mara kabla ya kutoka katika vyumba vyao asubuhi ili kwenda shuleni, wanapaswa kutandika vitanda, kuweka nguo chafu mahali panapofaa, na kupanga vitu vyao vingine. Sheria inayofaa ni, “Kila kitu kina mahali pake na basi kila kitu kinapaswa kuwekwa mahali pake.”

Pia, watu fulani katika familia wanaweza kugawiwa kazi au eneo hususa liwe sehemu yao ya kusafisha. Kwa mfano, je, baba huhakikisha gereji imepangwa na kusafishwa kabisa angalau mara moja kwa mwaka? Je, mtoto mmoja anaweza kumsaidia? Nani huhakikisha kwamba hakuna magugu au nyasi ndefu mbele ya nyumba? Hilo linapaswa kufanywa mara ngapi ili kuhakikisha eneo la mbele la nyumba ni nadhifu? Je, nyumba ina dari au stoo inayohitaji kuondolewa vitu visivyohitajika na kupangwa vizuri? Ikiwa ndivyo, ni nani atafanya kazi hiyo? Wazazi wengine hugawia watoto kazi hizo, wakizibadili kwa zamu.

Kwa hiyo, panga ratiba nzuri ya kutunza nyumba yako. Iwe utasafisha nyumba mwenyewe au pamoja na familia yako au utahitaji kumwajiri mtu akusaidie, ni muhimu kuwa na ratiba nzuri. Mama mmoja ambaye hudumisha nyumba yake ikiwa safi sana anatueleza jinsi familia yote hushirikiana kuisafisha: “Mimi na binti zangu watatu hugawana kazi za nyumbani. Norma Adriana husafisha sebule, vyumba viwili vya kulala, ua, na eneo la mbele la nyumba. Ana Joaquina hushughulika na jikoni. Mimi huosha nguo na kushughulikia mambo mengine, naye María del Carmen huosha vyombo.”

Sura Nzuri Nje ya Nyumba

Namna gani nje ya nyumba? Iwe unaishi katika nyumba kubwa au katika nyumba ya hali ya chini, unahitaji kuwa na ratiba ya kusafisha na kudumisha usafi wa nje. Kwa mfano, lango katika ua wa nyumba linaweza kung’oka bawaba moja. Lango hilo litaonekana vibaya ikiwa halitarekebishwa. Pia kutaonekana vibaya ikiwa takataka zitaachwa zirundamane kwenye mwingilio wa nyumba au kwenye vijia vya karibu. Nyakati nyingine pia, mikebe na vitu vingine huachwa nje ya nyumba na vinaweza kuwa makao ya wanyama na wadudu waharibifu.

Familia fulani zimepanga kufagia na kusafisha sehemu za nje za nyumba, kutia ndani vijia vya kando na hata barabara mbele ya nyumba, mara moja kwa siku au kila juma inapohitajika. Ni kweli kwamba katika maeneo fulani serikali zina mipango mizuri ya kusafisha mazingira, lakini kwingine hakuna mipango kama hiyo. Bila shaka, mahali tunapoishi pataonekana safi zaidi na hapatakuwa hatari kwa afya ikiwa sote tutatimiza sehemu yetu kupasafisha.

Zaidi ya kupanga ratiba ya kazi zilizotajwa, familia fulani huandika ratiba yao na kuibandika mahali kila mmoja anaweza kuiona na kuifuata. Hilo linaweza kuwa na matokeo mazuri. Kwa kweli, hatujaorodhesha mambo yote unayopaswa kujua kuhusu usafi. Kwa mfano, unahitaji kuamua bidhaa za kusafishia zinazofaa eneo lenu na vifaa ambavyo unaweza kununua.

Bila shaka, mapendekezo haya machache yatasaidia familia yote ielewe uhitaji wa kudumisha usafi wa nyumba na mazingira yake. Kumbuka kwamba kudumisha nyumba na mazingira yake yakiwa safi kunategemea si kiasi cha pesa ulizo nazo, bali mtazamo wako wa akilini.

[Sanduku katika ukurasa wa 20, 21]

Ratiba Unayoweza Kutumia Kusafisha Nyumba

Tumia nafasi ya ziada kuongeza mambo yako mwenyewe kwenye orodha hii

Jambo muhimu: Kuchanganya bidhaa za kusafisha kunaweza kuwa hatari sana. Hasa jihadhari dhidi ya kuchanganya dawa ya kuondoa madoa na amonia

Kila Siku

Chumba cha kulala: Tandika vitanda na kupanga vitu

Jikoni: Safisha vyombo na beseni ya kuvisafishia. Ondoa vitu kwenye meza. Fagia au pangusa sakafu ikihitajika

Bafu na choo: Safisha choo na beseni ya kunawia. Panga vitu

Sebule na vyumba vingine: Panga vitu. Pangusa fanicha. Fagia au pangusa sakafu ikihitajika

Nyumba yote: Tupa takataka mahali panapofaa

Kila Juma

Chumba cha kulala: Badili matandiko. Fagia au pangusa sakafu ikihitajika. Pangusa fanicha

Jikoni: Safisha jiko na vifaa vingine vya kupikia na kuoshea vyombo. Pangusa sakafu

Bafu na choo: Safisha kuta za bafu na mifereji. Safisha choo, kabati, na mahali pengine pote kwa dawa ya kuua viini. Badili taulo. Fagia au pangusa sakafu

Kila mwezi

Bafu na choo: Safisha kabisa kuta zote

Nyumba yote: Safisha miimo ya milango. Pangusa na kusafisha kabisa mifuko ya mito ya kukalia na mifuko mingine kama hiyo

Bustani, sehemu ya nje, gereji: Fagia na kuosha ikihitajika. Epuka kurundika takataka au vitu usivyohitaji

Kila Miezi Sita

Chumba cha kulala: Safisha shuka za kupamba vitanda kulingana na maagizo ya watengenezaji

Jikoni: Toa vitu vyote kwenye friji na uisafishe kabisa

Bafu na choo: Ondoa kila kitu kwenye rafu na kabati na uzisafishe kabisa. Tupa vitu visivyohitajika

Nyumba yote: Safisha taa, feni, na vifaa vingine vya umeme. Safisha milango. Safisha madirisha na fremu za madirisha

Kila Mwaka

Chumba cha kulala: Toa vitu vyote kwenye kabati na uisafishe kabisa. Tupa vitu usivyohitaji. Safisha blanketi. Ondoa kabisa vumbi kwenye godoro. Safisha mito kulingana na maagizo ya watengenezaji

Jikoni: Toa vitu vyote na usafishe rafu na kabati. Tupa vitu visivyohitajika. Songesha vifaa vya jikoni na usafishe eneo chini yake

Nyumba yote: Safisha kuta zote. Safisha vitambaa na sponji za viti na mapazia kulingana na maagizo ya watengenezaji

Gereji au stoo. Fagia kabisa. Panga au tupa vitu visivyohitajika

[Picha katika ukurasa wa 22]

“Kila kitu kina mahali pake na basi kila kitu kinapaswa kuwekwa mahali pake”

[Picha katika ukurasa wa 22]

Huenda ikafaa kuwapa wengine vitu usivyotumia