Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mfumo wa Mbawakawa wa Kujikinga

Mfumo wa Mbawakawa wa Kujikinga

Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Mfumo wa Mbawakawa wa Kujikinga

▪ Ingawa ana urefu usiozidi sentimita mbili, mbawakawa anayeitwa bombardier anajulikana kwa mfumo wake wa pekee wa kujikinga. Anapotishwa, mdudu huyo hurusha umajimaji unaochemka na kunuka vibaya pamoja na mvuke kutoka kwenye sehemu zake za nyuma, na hivyo kuwafukuza buibui, ndege, na pia vyura.

Fikiria hili: Mbawakawa huyo ana “tezi mbili ambazo hufunguka kwenye ncha ya tumbo [lake].” Kila tezi lina mtungi ambao una asidi na hidrojeni peroksaidi na chemba iliyojaa vimeng’enya vilivyochanganywa na maji ambapo kemikali huchangamana. Ili ajilinde, mdudu huyo anaweza kufinya mchanganyiko ulio ndani ya mitungi uingie kwenye chemba na hivyo kufanya kemikali zichangamane. Matokeo ni nini? Zikichemka kwa karibu digrii 100 Selsiasi, kemikali zenye harufu mbaya, maji, na mvuke hurushiwa adui. Chemba hizo zenye kemikali zina urefu usiozidi milimita moja, hata hivyo, mbawakawa huyo anaweza kubadili mwendo, mwelekeo, na kiwango cha sumu anayorusha.

Watafiti wamechunguza mbawakawa huyo ili kujifunza jinsi ya kubuni mabomba ya kurusha maji yanayofanya kazi vizuri zaidi na yasiyoharibu mazingira. Wamegundua kwamba mbawakawa huyo ana valvu zinazoruhusu umajimaji uelekee upande mmoja na hivyo kufanya kemikali ziingie ndani ya chemba. Pia ana valvu zinazofunguka wakati tu chemba inapokuwa na shinikizo la kutosha kurusha kemikali hizo. Wataalamu wanatumaini kwamba watatumia tekinolojia wanayopata kutoka kwa mbawakawa anayeitwa bombardier katika injini za magari na vifaa vya kuzima moto, na vilevile katika vifaa fulani vya kutoa dawa. Profesa Andy McIntosh wa Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza, anasema: “Hakuna mtu ambaye amemchunguza mbawakawa huyo kifizikia na kiinjinia kama tulivyofanya, na hatukutarajia kwamba tungejifunza mambo mengi hivyo.”

Una maoni gani? Je, mfumo tata wa mbawakawa anayeitwa bombardier wenye valvu, uwezo wa kuchemsha mchanganyiko wa kemikali, na kuzirusha, ulijitokeza wenyewe? Au je, ulibuniwa?

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Oxford Scientific/photolibrary