Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wakati Ndege Wanapogonga Majengo

Wakati Ndege Wanapogonga Majengo

Wakati Ndege Wanapogonga Majengo

INGAWA ilikuwa mchana, ndege anayeitwa kigogota aligonga jengo ndefu kisha akaanguka chini. Ndege huyo hakuwa ameona kioo. Mpita-njia mwenye huruma alimpata ndege huyo aliyechanganyikiwa na kumsaidia akitumaini kwamba atapata nafuu. Muda si muda ndege huyo alitoa sauti, akasimama, akatikisa mabawa yake, na kuruka angani. *

Inasikitisha kwamba si ndege wote wanaopona wanapogonga majengo. Kwa kweli, nusu ya ndege wanaogonga nyumba hufa. Uchunguzi unaonyesha kwamba nchini Marekani peke yake, ndege zaidi ya milioni 100 hufa kila mwaka baada ya kugonga majengo mbalimbali, linasema Shirika la Audubon. Na wachunguzi fulani wanaamini kwamba huenda idadi hiyo ikakaribia bilioni moja! Lakini, kwa nini ndege hugonga majengo? Na ni nini kinachoweza kufanywa ili kuhakikisha wanaruka kwa usalama zaidi?

Visababishi Vikuu ni Vioo na Mwangaza

Vioo ni hatari kwa ndege. Vioo vinapokuwa safi na bila rangi, mara nyingi ndege wanaona tu vitu vilivyo upande ule mwingine, ambavyo vinaweza kutia ndani mimea na anga. Kwa hiyo, wakati mwingine ndege wasiojua hugonga kioo wakiwa katika mwendo wa kasi. Huenda pia wakaona mimea iliyo ndani ya vyumba au nyumba zenye vioo na kujaribu kutua juu ya mimea hiyo.

Vioo vilivyotiwa rangi vinaweza kuwa hatari. Chini ya hali fulani, huenda ndege wasione kioo bali mandhari iliyo nyuma yao kwenye kioo, na hilo hutokeza msiba. Ndege hata wameuawa na vioo vilivyo katika hifadhi za ndege na wanyama! Mtaalamu wa ndege na mwanabiolojia profesa Dakt. Daniel Klem, Jr., anasema kwamba ndege wengi zaidi hufa kwa sababu ya kugonga vioo kuliko kisababishi kingine kinachohusiana na utendaji wa wanadamu, isipokuwa kuharibiwa kwa makao yao.

Ndege fulani hukabili hatari ya kugonga majengo kuliko wengine. Kwa mfano, ndege wengi waimbaji wanaohama, husafiri usiku na kwa sehemu fulani huongozwa na nyota. Kwa sababu hiyo, huenda wakatatanishwa na taa nyangavu kwenye majengo marefu. Kwa kweli, ndege fulani wamechanganyikiwa hivi kwamba wamezunguka bila mwelekeo kwenye eneo moja hadi wakaanguka kwa sababu ya uchovu. Hatari pia hutokea wakati wa usiku wenye mvua au wenye mawingu mengi. Pindi hizo, ndege huruka chini zaidi na hivyo kuongeza hatari ya kugonga majengo marefu.

Jinsi Idadi ya Ndege Inavyoathiriwa

Kulingana na ripoti moja, jengo moja tu refu huko Chicago, Illinois, Marekani, husababisha kwa wastani vifo vya ndege 1,480 hivi wakati wa msimu wa uhamaji. Hivyo, katika kipindi cha miaka 14 mfululizo, jengo hilo moja lilisababisha vifo vya ndege 20,700 hivi. Bila shaka, jumla ya idadi ya ndege waliogonga jengo hilo ni kubwa kuliko hiyo. Zaidi ya hilo, ndege hao “si njiwa, shakwe, au bata-bukini, . . . ndege hao ni wale wanaokabili hatari ya kutoweka,” anasema Michael Mesure, msimamizi wa Programu ya Kuwahamasisha Watu Kuhusu Mwangaza Hatari huko Toronto, Kanada.

Kwa mfano, katika mwaka mmoja hivi karibuni nchini Australia vioo viliua kasuku 30 hivi wanaoitwa swift, ambao ni 2,000 tu wanaobaki. Katika majumba ya makumbusho huko Marekani, idadi kubwa ya aina fulani ya pepeo waliokaushwa, ambao sasa huenda wametoweka, ni wale waliopatikana wakiwa wamekufa baada ya kugonga mnara fulani hususa wa taa huko Florida.

Ndege wanaoendelea kuishi baada ya kugonga majengo huwa wamejeruhiwa au wanakuwa dhaifu. Hilo linaweza kuwa hatari hasa kwa ndege wanaohama. Wakijeruhiwa na kuanguka mahali penye majengo mengi, huenda wakafa njaa au wakaliwa na wanyama wengine, ambao wamejua mahali pa kupata chakula.

Je, Ndege Wanaweza Kuzuiwa Wasigonge Majengo?

Ili ndege waepuke kugonga vioo, wanahitaji kuviona na kuvitambua. Ili kuwasaidia kufanya hivyo, baadhi ya wenye nyumba wamejinyima starehe za kuangalia mandhari kwa kubandika michoro, vibandiko, na vitu vingine vinavyoonekana wazi kwenye vioo ambavyo huenda vikagongwa na ndege. Kulingana na Klem, jambo muhimu si michoro au vibandiko vyenyewe bali ni mahali vitu hivyo vimebandikwa. Kulingana na utafiti wake, vitu hivyo vinapaswa kuachana kwa upana wa sentimita tano hivi na urefu wa sentimita kumi hivi.

Ni nini kinachoweza kufanywa ili kuwasaidia ndege wanaohama usiku? ‘Inawezekana kuzuia ndege kugonga majengo usiku kwa kuzima taa,’ anasema mtaalamu wa uchunguzi wa mambo ya mazingira Lesley J. Evans Ogden. Katika majiji fulani, taa zinazotumiwa kurembesha majengo marefu sasa zinazimwa au kupunguzwa mwangaza saa fulani za usiku hasa katika msimu wa ndege kuhama. Katika visa vingine, madirisha ya majengo marefu yamewekwa neti ili ndege wasifikiri kwamba wanatazama anga.

Huenda hatua kama hizo zikapunguza vifo vya ndege kwa asilimia 80 hivi, na hivyo kuokoa mamilioni ya ndege kila mwaka. Lakini inawezekana kwamba tatizo hilo halitatatuliwa kwa sababu watu wanapenda mwangaza na vioo. Kwa hiyo, mashirika ambayo yanashughulikia masilahi ya ndege, kama vile Shirika la Audubon, yanajaribu kuwahimiza wachoraji wa ramani za ujenzi na wajenzi wafikirie mahitaji ya viumbe ulimwenguni.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Ni hatari kuwagusa ndege waliojeruhiwa, kwa sababu hawajui kwamba unataka kuwasaidia. Pia, ndege fulani wanaweza kuwaambukiza wanadamu magonjwa. Kwa hiyo, ikiwa unataka kumsaidia ndege aliyejeruhiwa, vaa glavu na unawe mikono baadaye. Ikiwa unahofia afya au usalama wako, usimkaribie ndege huyo. Ikitegemea hali, unaweza kuomba msaada wa wataalamu.

[Sanduku katika ukurasa wa 10]

NDEGE WOTE WAMEENDA WAPI?

Makadirio ya kila mwaka ya vifo vya ndege vilivyosababishwa na utendaji wa wanadamu huko Marekani

▪ Minara ya mawasiliano—milioni 40

▪ Sumu za kuua wadudu—milioni 74

▪ Paka na paka-mwitu—milioni 365

▪ Vioo—milioni 100 hadi bilioni moja

▪ Kupoteza makao—haijulikani, lakini huenda hicho ndicho kisababishi kikuu

[Picha katika ukurasa wa 10]

Huko Marekani ndege milioni 100 hivi hufa kila mwaka baada ya kugonga madirisha

[Hisani]

© Reimar Gaertner/age fotostock