Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuitazama Mihiri kwa Ukaribu

Kuitazama Mihiri kwa Ukaribu

Kuitazama Mihiri kwa Ukaribu

MNAMO Agosti (Mwezi wa 8) 2003, Mihiri ilikaribia sana sayari yetu. Kwa miaka 60,000 hivi Mihiri haijawahi kuwa karibu hivyo na dunia kwani ilikuwa umbali wa kilomita milioni 56 hivi. Watu wanaochunguza nyota walifurahi sana kwani sayari hiyo nyekundu haikuwa mbali sana, ni kana kwamba ilikuwa kwenye ujirani wetu.

Mapema katika mwaka wa 2004, vyombo kadhaa vya angani vilitua juu ya Mihiri. Baadhi ya vyombo hivyo vilichunguza sayari hiyo vikiwa kwenye sayari yenyewe na vingine kutoka angani. Vyombo hivyo vimetufundisha nini kuhusu jirani huyo wetu?

Kuchunguza Sayari Nyekundu

Chombo cha angani kinachoitwa Mars Global Surveyor kiliwasili kwenye Mihiri mnamo 1997. Kiligundua kwamba wakati mmoja Mihiri ilikuwa na nguvu nyingi za sumaku. Pia chombo hicho kilichora ramani ya Mihiri ambayo ilionyesha mambo mengi kutia ndani umbali kutoka sehemu ya chini zaidi ya sayari hiyo hadi sehemu refu zaidi. Umbali huo ni wa kilomita 29 ilhali umbali kama huo wa dunia ni kilomita 19. *

Sehemu ya chini zaidi ya Mihiri ni bonde kubwa la Hellas ambalo huenda lilitokea baada ya kugongwa na jiwe kubwa sana la angani. Sehemu ya juu zaidi ni kilele cha mlima mkubwa wa volkano unaoitwa Olympus Mons ulio na urefu wa kilomita 21. Pia kamera iliyo ndani ya chombo cha angani kilichotajwa awali ilipiga picha ya mawe yaliyoonekana kuwa na upana wa zaidi ya mita 18, vilevile ilionyesha marundo makubwa ya mchanga na makorongo yaliyokuwa yamefanyizwa muda mfupi kabla. Kifaa kingine kilionyesha kwamba miamba mingi ilikuwa ya volkano.

Ingawa mnamo Novemba (Mwezi wa 11) 2006 mawasiliano kati ya wanasayansi na chombo cha Mars Global Surveyor yalipotea, waliendelea kuchunguza sayari hiyo nyekundu kupitia vyombo vitatu vya angani, yaani, Mars Odyssey ya 2001, Mars Express, na Mars Reconnaissance. * Wakitumia kamera za hali ya juu na vifaa vingine walichunguza angahewa ya Mihiri na mazingira yake na hata wakagundua na kupiga picha barafu nyingi kwenye ncha ya kaskazini ya sayari hiyo.

Wanasayansi walirusha chombo kinachoitwa Phoenix Mars ambacho kiliwasili salama kwenye sayari nyekundu Mei 25, 2008 (25/5/2008) kuchunguza barafu hiyo. Chombo hicho kina vifaa vya hali ya juu vinavyoweza kuchunguza angahewa na eneo linaloganda daima kwenye ncha za sayari hiyo. Wanasayansi wanatumaini kujifunza ikiwa mchanga huo wenye barafu umewahi kuwa na vijidudu. Hata hivyo, juhudi za kutafuta viumbe hai au hali zinazoruhusu uhai uendelee katika sayari hiyo zilikuwa zimeanza zamani.

Vyombo Vingine vya Angani

Vyombo vingine viwili vya kuchunguza Mihiri, yaani, Spirit na Opportunity viliwasili kwenye sayari hiyo mnamo Januari (Mwezi wa 1) 2004. Mahali ambapo vilitua palikuwa pamechaguliwa mapema kutokana na habari zilizoletwa na vyombo vya awali. Vyombo hivyo viwili ambavyo kila kimoja kilikuwa na ukubwa wa gari dogo linalotumiwa kwa mbio za magari, vilipunguza mwendo katika angahewa la Mihiri kwa kutumia ngao zinazokinga joto, parachuti, na roketi. Vilipotua vilidunda-dunda vikiwa vimefunikwa kwa mifuko ya hewa kama chombo kinachoitwa Mars Pathfinder kilivyotua mnamo 1997. *

Sehemu ya juu ya Mihiri ina ukubwa unaokaribia ukubwa wa nchi kavu duniani, hivyo kuna nafasi ya kutosha ya kuichunguza kwa kutumia roboti. Chombo cha Opportunity kilitua huko Meridiani Planum, nchi tambarare yenye miamba ya kale yenye matabaka iliyo na madini yenye chuma. Chombo cha Spirit kilitua upande mwingine wa Mihiri ili kichunguze kina cha Bonde kubwa la Gusev ambalo wataalamu fulani wanasema kwamba huenda zamani lilikuwa na ziwa. Kulingana na NASA, kusudi la kurusha vyombo hivyo lilikuwa “kuchunguza mazingira ya maeneo fulani ambayo huenda wakati mmoja yalikuwa na maji na yangeweza kutegemeza uhai.”

“Wanajiolojia” Waenda Kwenye Mihiri

Chombo cha Spirit kilipowasili kwenye sayari hiyo Januari 4, 2004, eneo hilo lilikuwa kavu, lenye miamba, na mashimo ya duara yasiyo na kina kirefu. Chombo hicho kilichunguza eneo hilo kama vile mwanajiolojia mwanadamu anavyochunguza udongo mbalimbali, miamba, na mambo mengine. Wanasayansi waliokuwa wakiongoza Spirit waligundua kwamba mahali chombo hicho kilitua kulikuwa kumejaa miamba ya volkano na mashimo yaliyosababishwa na vimondo. Kisha chombo hicho kikasafiri umbali wa kilomita 2.6 ili kuchunguza safu ya vilima. Huko kiligundua miamba isiyo ya kawaida na miamba mingine myepesi ambayo huenda ilitokana na milipuko ya volkano.

Januari 25, 2004, baada ya kusafiri kilomita milioni 456, chombo cha Opportunity kilitua kilomita 25 hivi kutoka eneo lililopaswa kutua. Chombo hicho kilichokuwa kimefunikwa na mfuko wa hewa kilidunda-dunda juu ya eneo tambarare la Meridiani na kwenda moja kwa moja na kuingia kwenye bonde ndogo. Mwanasayansi mmoja alisema kwamba hilo lilikuwa jambo la ajabu sana.

Chombo cha Opportunity kilichunguza mabonde kadhaa ambayo yana miamba yenye matabaka yaliyokuwa na kiasi kidogo cha madini ya duara yanayoitwa blueberries. Rangi ya madini hayo ya kijivu ni tofauti sana na udongo na miamba ya rangi nyekundu. Miamba fulani ina miundo inayofanana na mchanga uliomwagiliwa maji. Wanasayansi fulani wanahisi kwamba miundo hiyo pamoja na klorini na bromini katika miamba, inaonyesha kwamba wakati fulani kulikuwa na maji ya chumvi katika eneo hilo.

Chombo kinachoitwa Phoenix Mars cha 2008 kimetoa habari zaidi kuhusu Mihiri hasa kuhusu maeneo yake yenye barafu. Kifaa fulani kimechimba barafu na kuchukua udongo na barafu na kuvipeleka kwenye “maabara” mawili ya Phoenix kwa ajili ya uchunguzi. Hata hivyo, chombo hicho kilikusudiwa kutumika kwa muda mfupi kwani miezi michache baada ya kazi ya chombo hicho kumalizika, gazeti Science lilieleza kwamba majira ya baridi kali yangefunika “Phoenix na theluji yenye kaboni dioksidi.”

Wazo la kwamba wanasayansi wanaweza kuchunguza sayari zingine zilizo umbali wa mamia ya mamilioni ya kilomita linaonyesha jambo linaloweza kutimizwa watu wanapofanya kazi pamoja kwa lengo moja. Pia mambo kama hayo yanaonyesha uwezo wa wanadamu. Bila shaka, kuchunguza mambo ya anga na sayansi kumewezeshwa kwa sababu sheria za kiasili zinategemeka kabisa. Sheria hizo hazikujiumba zilianzishwa na Mchoraji ramani Mkuu zaidi katika ulimwengu, Yehova Mungu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Kilomita 19 zinawakilisha umbali kutoka sehemu ya chini zaidi ya Bonde la Mariana katika Bahari ya Pasifiki hadi kilele cha Mlima Everest.

^ fu. 7 Vyombo vya angani Mars Odyssey ya 2001 na Mars Reconnaissance vilirushwa angani na shirika la National Aeronautics and Space Administration (NASA), na chombo kinachoitwa Mars Express kilirushwa na Shirika la Anga la Ulaya.

^ fu. 10 Ona makala “Roboti Yachunguza Mihiri,” katika Amkeni! la Juni 22, 1998 (22/6/1998)

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

JE, KUNA UHAI KWENYE MIHIRI?

Wataalamu wawili wa nyota wa karne ya 18 na 19, Sir William Herschel na Percival Lowell, walidokeza kwamba Mihiri, inayoitwa pia sayari nyekundu, imejaa viumbe wenye akili, na nadharia ya Darwin ya mageuzi iliunga mkono wazo hilo. Lakini maoni hayo yote yamethibitishwa kuwa ya uwongo. Picha za satelaiti zimeonyesha sayari kame yenye angahewa lililojaa kaboni dioksidi. Mnamo 1976, majaribio yaliyofanywa na chombo cha Viking 1 yalionyesha kwamba hakuna uhai kwenye Mihiri. *

Hata hivyo, wanasayansi wanaendelea kutafuta dalili za uhai kwenye sayari hiyo. Kurushwa kwa chombo cha Phoenix Mars ndilo jaribio lao la karibuni zaidi. Kwa sababu vijidudu fulani vinaweza kuishi chini ya hali ngumu hapa duniani, wanasayansi wanadhani kwamba vijidudu kama hivyo vinaweza kuishi katika maeneo fulani kwenye Mihiri. Chombo kinachoitwa Beagle 2 kilichounganishwa kwenye chombo cha Mars Express, kilikuwa na vifaa vya kupima vitu vyenye uhai kwenye udongo wa Mihiri, lakini vyombo hivyo havikuweza kutua kwenye sayari hiyo mwishoni mwa mwaka wa 2003. Mwaka uliofuata wanasayansi walipata kiasi kidogo cha methani katika angahewa la Mihiri, na hilo likachochea udadisi ikiwa gesi hiyo ilitokezwa na viumbe au volkano.

Je, uhai unaweza kujitokeza wenyewe mahali popote ulimwenguni? Biblia inajibu hivi: “Kwa [Mungu] iko chemchemi ya uzima.” (Zaburi 36:9) Naam, uhai unaweza tu kutokezwa na uhai mwingine, Mpaji wa Uhai ambaye ndiye Muumba, Yehova Mungu.—Matendo 17:25.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 24 Ona makala “Kuzuru Tena Sayari Nyekundu” katika toleo la Novemba 22, 1999 la Amkeni!

[Hisani]

NASA/JPL/Cornell

[Picha katika ukurasa wa 15]

Roboti ya Phoenix Mars iliyo na kijiko, kifaa cha kuchimba, na kamera

[Picha katika ukurasa wa 15]

Picha ya madini yanayoitwa “blueberries”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Volkano ya Olympus Mons ambayo imeacha kulipuka yenye urefu wa kilomita 21

[Picha katika ukurasa wa 15]

Chombo cha Spirit kilichimba na kuchota mchanga wa mwamba huu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Top left: NASA/JPL-Caltech/University of Arizona/Texas A&M University; top right: NASA/JPL/Malin Space Science Systems; bottom left and right: NASA/JPL/Cornell