Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Wakitumia darubini za Subaru na Keck kwenye eneo la Mauna Kea [Hawaii], kikundi cha wataalamu wa nyota wamegundua makundi makubwa sana ya galaksi yenye upana wa miaka ya nuru milioni 200.” Makundi hayo yanafanyiza makundi makubwa zaidi kuwahi kugunduliwa.—TOVUTI YA DARUBINI YA SUBARU, JAPANI.

Shirika la Takwimu za Kitaifa la Uingereza linaripoti kwamba “idadi ya harusi [nchini Uingereza na Wales] mnamo 2006 ilikuwa ndiyo ya chini zaidi katika miaka 110. Watu wengi zaidi wanapendelea kuishi pamoja bila kuoana.”—THE GUARDIAN WEEKLY, UINGEREZA.

Kulingana na shirika fulani linalochunguza uhusiano kati ya dini na maisha ya kawaida, “asilimia 44 ya watu wazima wamebadili dini, au wameanza kufuata dini fulani baada ya kutoshirikiana na dini kwa muda, au wameacha kushirikiana na dini yoyote.”—MAREKANI.

Vyuo na Kufanya Ngono

“Isipokuwa vyuo fulani vya kievanjeli . . . , hakuna tofauti kubwa kati vyuo na vyuo vikuu vya umma, vya kibinafsi, na Kikatoliki katika tabia ya kufanya ngono iliyoenea katika vyuo, yaani, tabia ya wanafunzi kufanya ngono na watu mbalimbali.” Hivyo ndivyo alivyosema mwanatheolojia na makamu wa profesa wa chuo kikuu Donna Freitas, baada ya kufanya utafiti kuhusu dini na tabia ya kufanya ngono katika vyuo vya Marekani. Kulingana na gazeti National Catholic Reporter, Freitas alisema kwamba dini haijawa na uvutano wowote katika mambo ya kingono na hilo halionyeshi tu jinsi kulivyo na “uvutano mkubwa katika vyuo wa kufanya ngono ovyoovyo” bali pia “udhaifu wa mafundisho ya kidini katika kupigana na tabia hiyo.”

Wazazi Walipwa Ili Kuwalea Wasichana

Serikali ya India inapanga kuwapa wazazi maskini kiasi kinachotoshana na dola 3,000 hivi (za Marekani) ili wawalee wasichana, inasema ripoti ya Shirika la Habari la BBC. Familia zitapokea pesa taslimu msichana anapozaliwa na pesa zingine katika hatua mbalimbali za maisha yake hadi afikie umri wa miaka 18. Ingawa utoaji-mimba kwa sababu ya jinsia ya kitoto ulipigwa marufuku mnamo 1994, zoea hilo bado limeenea sana. Kwa kweli, inakadiriwa kwamba kwa miaka 20 hivi iliyopita vijusi milioni 10 hivi vya wasichana vilitolewa, na hivyo kufanya maeneo fulani yawe na wavulana wengi kuliko wasichana. Kulingana na idadi ya watu iliyofanywa mwaka wa 2001, nchini kote kulikuwa na wasichana 927 kwa kila wavulana 1,000 walio chini ya umri wa miaka sita na tofauti hiyo ilikuwa ikiongezeka. Katika jimbo moja, kwa kila wasichana 793 waliozaliwa kulikuwa na wavulana 1,000.

Ndege Wanavyoathiriwa na Kelele

Ndege fulani wanatumia sauti ya juu ili wasikike licha ya kelele za majijini. Ingawa huenda wanadamu wakaudhiwa na kelele za mijini, kelele hizo ni hatari zaidi kwa ndege, linasema gazeti New Scientist, kwani ndege wa kiume wanaimba ili “wavutie wenzi na ili waonyeshe mipaka ya eneo lao.” Kwa kuwa kelele katika jiji huwa na sauti nzito, ndege fulani huimba usiku au wanatumia sauti ya juu zaidi. Kwa kuongezea, uwezo huo wa kubadilika kulingana na hali unatumiwa pia na ndege walio katika maeneo ya mashambani, linasema gazeti hilo. Ndege wanaoishi karibu na “maporomoko ya maji na mabonde ya mito pia huimba kwa sauti ya juu zaidi.”