Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nani Anayekusaidia Wakati wa Dharura?

Ni Nani Anayekusaidia Wakati wa Dharura?

Ni Nani Anayekusaidia Wakati wa Dharura?

Swichi inapobonyezwa, taa za ambulansi yetu zinaanza kumweka kwenye magari na majengo. Sauti ya juu ya king’ora cha ambulansi inafanya magari na wapita-njia wasimame ili kutupisha tunapojitahidi kujibu kilio cha kuomba msaada.

KWA zaidi ya miaka 20, nimekuwa mhudumu wa hali za dharura nikiwapa wagonjwa na majeruhi matibabu ya dharura kabla ya kufikishwa hospitalini. * Kila siku tunakabiliana na hali mpya za dharura. Nimekumbana na hali mbalimbali, zile za kawaida na zile mbaya sana, na matokeo yake yamekuwa yenye kufurahisha na mengine yenye kuhuzunisha sana.

Msaada kwa Jamii

Wahudumu wa hali za dharura ni sehemu muhimu katika mfumo wa huduma za afya za Kanada. Msaada wa kitiba ambao wao huwapa watu kabla ya kufika hospitalini unaweza kuokoa maisha au angalau kupunguza madhara au hatari ya ugonjwa fulani. *

Katika maeneo mengi wahudumu wa afya wanafanya kazi saa 24 kwa siku, siku 365 kwa mwaka. Wanaweza kuwa wameajiriwa na manispaa, kampuni, au hospitali inayotoa huduma za dharura. Wengine hufanya kazi katika ambulansi au idara ya wazima moto.

Wanaume na wanawake hao waliozoezwa kwa njia ya pekee huitikia haraka mwito wa kuomba msaada. Mwito huo unaweza kuja wakati wowote bila kutarajiwa. Fikiria kile ambacho mhudumu wa hali za dharura amezoezwa kufanya.

Wamezoezwa Kuokoa Uhai

Ingawa mazoezi ambayo wahudumu wa hali za dharura hupata na maneno yanayotumiwa kufafanua viwango vya mazoezi hayo hutofautiana katika wilaya mbalimbali nchini Kanada, kwa kawaida mazoezi hayo yamegawanywa katika hatua nne—mhudumu wa kuitikia hali ya dharura, mhudumu wa kutoa huduma ya msingi, mhudumu wa kutibu wagonjwa mahututi kadiri fulani, na mhudumu wa kuhudumia wagonjwa mahututi sana. Idara mbalimbali za serikali na pia wataalamu wa tiba huomba kuona cheti cha kuthibitisha kwamba mtu amehitimu kuwa mhudumu wa hali za dharura.

Mazoezi yangu ya msingi huku Kanada yalitia ndani kufundishwa kwa saa nyingi darasani, hospitalini, na katika ambulansi. Tulifundishwa jinsi ya kuchunguza dalili za kuonyesha kwamba mtu yuko hai, kutumia vifaa vya kumpa mtu oksijeni na mashini ya kupumulia, na jinsi ya kufanya moyo uanze kupiga tena na mtu apumue (CPR), na pia jinsi ya kufunga bendeji, vibanzi, na kutumia mbao za kuzuia uti wa mgongo usisonge.

Pia nilipata mazoezi mengine muhimu kwa saa 300 katika idara za hospitali kadhaa ya kushughulikia hali ya dharura, wagonjwa mahututi, na akina mama wanaojifungua. Siwezi kusahau kisa changu cha kwanza cha kumsaidia mwanamke fulani kuzaa—ilikuwa sawa na kushuhudia muujiza! Kisa hicho na vingine vingi vilinitayarisha kwa ajili ya hatua iliyofuata katika mazoezi yangu ambayo ilihusisha kufanya kazi kwa zaidi ya saa 300 katika ambulansi nikizoezwa na wahudumu wawili wa hali za dharura wenye uzoefu. Baada ya kupita mitihani ya kuandika na ya kushughulikia visa halisi, nilipewa cheti cha kuwa msaidizi wa mhudumu wa matibabu ya hali ya dharura, ambaye sasa anaitwa mhudumu wa kutoa huduma ya msingi.

Kwa miaka kadhaa nilifanya kazi vijijini na pia mjini. Upesi nilijifunza umuhimu wa ujuzi wangu wa kuokoa uhai wakati mjenzi alipoingia kwenye idara ya hali za dharura ya hospitali moja. Baada tu ya kuingia, moyo wa mtu huyo uliacha kupiga. Nilimhudumia pamoja na madaktari na wauguzi waliojaribu kufanya moyo wake uanze kupiga tena na aanze kupumua huku wakimpiga kwa umeme kifuani wakitumia kifaa fulani na kumpa dawa. Baada ya dakika chache, moyo wa mtu huyo ulianza kupiga tena na akaanza kupumua. Kisha akapelekwa kwenye chumba cha kuwatunzia wagonjwa mahututi (CCU). Siku iliyofuata nilipelekwa kwenye chumba hicho na daktari akanijulisha kwa mwanamume aliyekuwa ameketi kitandani akizungumza na mke wake. Sikumtambua hadi aliponiuliza: “Unanikumbuka? Uliokoa uhai wangu jana!” Nilijihisi vizuri wee!

Sehemu ya mwisho ya mazoezi yangu ilitia ndani kufanya kazi na daktari aliyeambatana nami kwa saa 12 ili kuchunguza jinsi nilivyokuwa nikiwatunza wagonjwa. Mwishowe, nilipita mitihani yangu ya kuandika na ya kushughulikia visa halisi na nikapewa cheti cha kuwa mhudumu wa kutibu wagonjwa mahututi kadiri fulani.

Wahudumu wa hali za dharura hufanya kazi chini ya mwelekezo wa msimamizi wa tiba, ambaye kwa kawaida anafanya kazi na halmashauri ya ushauri wa kitiba ili kuandika mbinu zinazofaa za matibabu. Matibabu ya dharura ambayo wahudumu wa hali za dharura hutoa hutegemea mbinu hizo au wao huwasiliana moja kwa moja na kikundi fulani cha madaktari wakitumia redio au simu. Kwa sababu hiyo, imesemekana kwamba wahudumu wa hali za dharura ndio macho, masikio, na mikono ya daktari. Matibabu yanayotolewa nyumbani, kwenye majengo ya umma, au pahali aksidenti imetokea yanaweza kutia ndani kumtia mgonjwa oksijeni, kumpa dawa, kufanya moyo wake uanze kupiga tena, kuingiza mrija katika umio ili kumsaidia mgonjwa kupumua na hata kufanya upasuaji.—Ona sanduku  “Mbinu za Matibabu za Wahudumu wa Hali za Dharura,” kwenye ukurasa wa 15.

Magumu na Hatari

Mhudumu wa hali za dharura hukumbana na magumu na hatari kila siku. Kazi hufanywa chini ya hali zozote zile za hewa na nyakati nyingine katika maeneo na hali zisizo salama. Hata kusafiri kwenda kwenye eneo la msiba kunaweza kuwa hatari.

Kila mara kuna hatari ya kumwagikiwa na damu na umajimaji kutoka mwilini, na kuambukizwa magonjwa. Ili kujilinda, sisi huvaa glavu, vitu vya kujifunika usoni, miwani, na mavazi fulani ya pekee.

Kutunza wagonjwa huhusisha kushughulika na watu wao wa ukoo, marafiki, au hata watu usiowajua, ambao wanaweza kuwa na hisia kali zisizotarajiwa. Ni jambo lenye kuhuzunisha sana mume na mke ambao wameishi pamoja kwa muda mrefu wanapotenganishwa na kifo. Si rahisi kumweleza mwenzi aliye hai kuhusu jambo hilo. Pindi moja nilipaswa kumwambia mwanamke fulani kwamba mume wake amekufa. Alinipiga ngumi na akatimua mbio nje na kuingia barabarani huku akipiga mayowe na kulia. Nilifaulu kumshika, naye akageuka, akanishika, akanikumbatia na kuanza kulia kwa uchungu begani mwangu.

Mtu anahitaji kuwa na hisia-mwenzi, busara, na huruma anaposhughulika na watu waliovurugika kihisia, waliolewa, au waliotumia dawa za kulevya. Watu wa aina hiyo wanaweza kuwa na hisia zisizotarajiwa. Kwa muda ambao nimefanya kazi hii, nimeumwa, kutemewa mate, na kushambuliwa kwa njia nyingine na wagonjwa ambao hawakuweza kujizuia.

Kazi hii pia inachosha kwa kuwa mara nyingi ninahitajika kuinua vitu vizito, nyakati nyingine nikiwa nimekaa vibaya. Mara nyingi tunawatibu wagonjwa tukiwa tumepiga magoti au kuinama. Sisi huumia tunapokuwa kazini. Mara nyingi sisi hujiumiza mgongo, mabega, na magoti. Majeraha mengine ni mabaya sana hivi kwamba mtu hawezi kuendelea kufanya kazi akiwa mhudumu wa hali ya dharura. Pia mtu anatarajiwa kufanya kazi kwa zamu mchana na usiku na hilo pia linaweza kuchosha.

Kuwatunza watu wanaougua ugonjwa au majeraha hatari kwa uhai kunachosha kiakili na kihisia. Ni lazima mhudumu wa hali za dharura awe mtulivu, atumie busara, na afanye maamuzi mazuri wakati wa dharura. Wahudumu wa hali za dharura hujionea maafa na watu wakiteseka. Wao huona na kuwatunza watu waliojeruhiwa vibaya sana. Ninakumbuka kijana mmoja ambaye alikuwa amepondwa vibaya sana katika aksidenti iliyotukia katika kiwanda kimoja. Akiwa amepondwa vibaya sana kuanzia kifuani kwenda chini, alinisihi mimi na mwenzangu tusimwache afe. Kwa kusikitisha, licha ya jitihada zetu na za madaktari na waaguzi, alikufa kabla ya saa moja kwisha.

Visa fulani vinahuzunisha sana. Siku moja asubuhi sana tulipokea simu kutoka kwa nyumba moja iliyokuwa inachomeka. Mume wa nyumba hiyo alikuwa amefika tu kutoka kazini alipomwona mke wake na binti yao mwenye umri wa miaka mitatu wakitoroka kutoka kwenye nyumba iliyokuwa imeshika moto. Watoto wengine watatu waliokuwa na umri wa kati ya miezi minne hadi miaka mitano pamoja na babu yao walikuwa wamekwama ndani ya nyumba hiyo hadi wazima-moto walipowaokoa. Nilikuwa kati ya vikundi kadhaa vya wahudumu wa hali za dharura waliojaribu bila kufanikiwa kuokoa maisha yao.

Kufikia sasa huenda ukajiuliza kwa nini mtu atake kuwa mhudumu wa hali za dharura? Nyakati nyingine ninajiuliza swali hilo. Mimi hukumbuka mfano wa Yesu kuhusu Msamaria mwenye ujirani aliyejitolea kumsaidia mwanamume aliyejeruhiwa. (Luka 10:30-37) Vivyo hivyo, mhudumu wa hali za dharura hujitolea kimwili na kihisia kumsaidia mtu aliyeomba msaada. Kwangu, kazi ya kuwa mhudumu wa hali za dharura imekuwa yenye kuthawabisha, lakini ninatamani sana wakati ambapo nitafutwa kazi. Kwa nini nifutwe? Kwa sababu Mungu anaahidi kwamba hivi karibuni hakuna atakayesema: “Mimi ni mgonjwa.” Isitoshe, ‘kifo na maumivu hayatakuwapo tena.’ (Isaya 33:24; Ufunuo 21:4)—Limesimuliwa na mhudumu wa hali za dharura nchini Kanada.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Kwa habari zaidi kuhusu mambo yanayoweza kupingana na dhamiri ya Mkristo anayefanya kazi akiwa mhudumu wa hali za dharura, ona gazeti Mnara wa Mlinzi la Aprili 15, 1999, ukurasa wa 29, na la Oktoba 1, 1975 (1/10/1975), ukurasa wa 441-442 au la Aprili 1, 1975, ukurasa wa 215-216 la Kiingereza.

^ fu. 5 Katika nchi fulani hakuna wahudumu wa hali za dharura katika ambulansi. Ni jukumu la dereva wa ambulansi kumpeleka mgonjwa hospitali haraka iwezekanavyo.

[Blabu katika ukurasa wa 13]

Sikumtambua hadi aliponiuliza: “Unanikumbuka? Uliokoa uhai wangu jana!” Nilijihisi vizuri wee

[Blabu katika ukurasa wa 14]

Kwa muda ambao nimefanya kazi hii, nimeumwa, kutemewa mate, na kushambuliwa kwa njia nyingine na wagonjwa ambao hawakuweza kujizuia

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

 MBINU ZA MATIBABU ZA WAHUDUMU WA HALI ZA DHARURA

Mhudumu wa hali za dharura amezoezwa kuhakikisha kwamba mgonjwa ana njia ya kupitishia hewa hadi kwenye mapafu. Huenda hilo likahusisha kumwingiza mgonjwa mrija wa plastiki kupitia mdomoni hadi kwenye koromeo. Au huenda akatumia sindano, mrija mdogo, waya na kisu cha upasuaji kuingiza mrija mkubwa kwenye shingo la mgonjwa hadi kwenye koo. Kuingiza sindano na mrija kupitia kifua hutumiwa kutibu pafu lililoacha kufanya kazi hali ambayo inaweza kusababisha kifo.

Mbinu nyingine ni kuingiza umajimaji mwilini kupitia mishipa. Sindano hutumiwa kuingiza mrija kwenye mshipa. Hivyo, mgonjwa anaweza kutiwa umajimaji mbalimbali kama vile ule wenye chumvi. Au kifaa fulani kinaweza kutumiwa kuingiza umajimaji hadi katikati ya mfupa.

Mhudumu wa hali za dharura anaweza kutumia kifaa cha kuchunguza mpigo wa moyo. Kifaa hicho kinaweza kutumiwa pia kumpiga mtu kwa umeme kifuani ili moyo uanze kupiga tena au kinaweza kutumiwa kupunguza mwendo wa moyo unaopiga kwa kasi. Kifaa hicho pia kinaweza kutumiwa kuusaidia moyo upige haraka zaidi.

[Hisani]

All photos: Taken by courtesy of City of Toronto EMS

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Taken by courtesy of City of Toronto EMS