Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kufuga na Kuzoeza Tembo

Kufuga na Kuzoeza Tembo

Kufuga na Kuzoeza Tembo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA

MZOEZAJI wa tembo anayeitwa mahout, alipokuwa akipika chakula chake kando ya Mto Narmada, alimwacha mtoto wake kati ya mkonga na miguu ya mbele ya tembo wake aliyekuwa akipumzika. Mtoto wake alijaribu mara nyingi kutoka hapo, lakini “tembo huyo aliyekuwa akipumzika aliinua mkonga wake na kumshika mtoto huyo kwa wororo na kumrudisha mahali baba yake alikuwa amemwacha,” kinasimulia kitabu Project Elephant. “Baba aliendelea kupika na ilionekana hakuwa na wasiwasi wowote kwamba mtoto wake alikuwa chini ya ulinzi mzuri.”

Tembo wametumiwa na wanadamu kufanya kazi tangu miaka ya 2000 K.W.K. Zamani, tembo walizoezwa hasa kwa ajili ya vita. Siku hizi nchini India, tembo wanazoezwa kufanya kazi. Wanatumiwa kubeba miti iliyokatwa, kwenye sherehe za kidini na harusi, katika matangazo ya biashara, katika sarakasi, na hata kuombaomba. Tembo hao wanafugwa jinsi gani? Wao huzoezwa namna gani?

Kuwazoeza Tembo

Kuna vituo mbalimbali nchini India vya kuwatunza ndama wa tembo walioshikwa mateka, kuachwa na wazazi, au kujeruhiwa porini. Kituo kimoja kama hicho kiko huko Koni, katika jimbo la Kerala. Ndama huzoezwa kuwa tembo wa kufanya kazi. Kwanza, ni lazima ndama amwamini mahout. Njia moja ya kufanya hivyo ni wakati anapolishwa. Ndama hutambua sauti ya mzoezaji, na anapoitwa ili apewe chakula yeye humkimbilia ili apewe maziwa na uji wa mtama. Tembo wachanga huzoezwa kufanya kazi wanapofikia umri wa miaka 13 hivi. Wao huanza kufanya kazi wanapofikia umri wa miaka 25. Huko Kerala, kulingana na sheria za serikali, tembo hustaafu wanapofikia umri wa miaka 65.

Ili kumwongoza tembo kwa njia salama, lazima mahout awe amezoezwa vizuri. Kulingana na Shirika la Masilahi ya Tembo la Trichur, Kerala, mahout mpya anahitaji kuzoezwa kikamili kwa angalau miezi mitatu. Mazoezi hayo hayatii ndani tu kujifunza kumwamrisha tembo. Yanahusisha kujifunza sehemu zote za maisha ya tembo.

Inachukua muda mrefu zaidi kumzoeza tembo aliyekomaa. Mzoezaji akiwa nje ya mahali tembo huyo amefungiwa, yeye huanza kumfunza mnyama huyo amri fulani za maneno. Huko Kerala, mahout hutumia amri na ishara 20 hivi ili tembo wake afanye kazi. Mzoezaji huyo hutoa amri zilizo wazi kwa sauti ya juu na, wakati huohuo, anamgonga tembo kwa kijiti na kumwonyesha anachopaswa kufanya. Anapotii amri, tembo huthawabishwa kwa kupewa kitu anachopenda. Mtu huyo anayemzoeza anapokuwa na hakika kwamba tembo ameanza kuwa na urafiki, anaingia ndani ya sehemu hiyo na kumpapasa. Kufanya hivyo kunaonyesha wanaweza kuaminiana. Baada ya muda, tembo huyo anaweza kupelekwa nje, lakini lazima yule anayemzoeza awe mwangalifu kwa kuwa bado ana tabia fulani za mwituni. Hadi inapobainika kwamba tembo huyo amekuwa wa kufugwa, yeye hufungwa katikati ya tembo wawili wanaotumiwa kuwazoeza tembo wengine anapopelekwa nje akaoge na kwa shughuli nyingine.

Baada ya tembo kuelewa amri za maneno, mahout anaketi kwenye mgongo wake na kumfundisha jinsi ya kuitikia amri nyingine kwa kumgonga kwa vidole vya miguu au kwa visigino. Ili tembo asonge mbele, mahout humfinya kwa vidole vikubwa vya miguu nyuma ya masikio yake. Ili tembo arudi nyuma, anamfinya mabegani kwa visigino vyote viwili. Ili kuepuka kumtatanisha tembo, amri za maneno hutolewa na mahout mmoja tu. Tembo ataelewa amri zote baada ya miaka mitatu au minne. Baada ya hapo, hawezi kusahau amri hizo kamwe. Hata ingawa tembo ana ubongo mdogo unapolinganishwa na ukubwa wa mwili wake, yeye ni mnyama mwenye akili sana.

Kumtunza Tembo

Tembo anahitaji kutunzwa akiwa mwenye afya na furaha. Ni muhimu kwake kuoga kila siku. Anapomwosha, mahout hutumia mawe na makumbi ya nazi yaliyokatwa vizuri ili kusugua ngozi yake ngumu lakini laini.

Kwa ajili ya kiamsha-kinywa, mahout humtayarishia tembo uji mzito wa uliotengenezwa kwa ngano, mtama, na aina fulani ya chakula cha mifugo. Chakula kikuu kinatia ndani mianzi, matawi ya mitende, na nyasi. Tembo hufurahi sana anapopewa karoti na miwa. Tembo hutumia wakati wao mwingi wakila. Wanahitaji kilo 140 hivi za chakula na lita 150 hivi za maji kila siku! Ili wawe marafiki, lazima mahout atosheleze mahitaji hayo.

Matokeo ya Kutendewa Vibaya

Tembo mpole wa India hawezi kufanyishwa kazi nyingi sana. Huenda tembo wakawashambulia mahout ambao huwaadhibu kwa maneno au kwa njia nyingine. Gazeti Sunday Herald la India lilisimulia jinsi tembo dume mwenye pembe “alivyokasirika na kuanza kushambulia . . . mahout waliomtendea vibaya. Tembo huyo aliyekuwa amekasirishwa na kipigo alichopewa na mahout hao alizusha fujo . . . na ikabidi adungwe sindano ya kumfanya alale.” Mnamo Aprili 2007, gazeti India Today International liliripoti hivi: “Katika muda wa miezi miwili tu iliyopita, zaidi ya tembo dume 10 wenye pembe walizusha fujo kwenye sherehe; tangu Januari (Mwezi wa 1) mwaka jana, mahout 48 wameuawa na wanyama hao wenye hasira.” Mara nyingi hasira kama hiyo huonekana wakati wa kipindi kinachoitwa musth. Hicho ni kipindi cha kuzaliana wakati ambapo homoni inayoitwa testosterone huongezeka katika tembo dume waliokomaa na wenye afya nzuri. Kwa sababu hiyo tembo hao huwa na fujo kuelekea tembo dume wengine na wanadamu. Kipindi hicho cha musth kinaweza kuendelea kwa siku 15 hadi miezi mitatu.

Sababu nyingine inayoweza kumfanya tembo akasirike ni wakati anapouzwa na kuanza kuongozwa na mahout mwingine. Upendo wake kwa mahout wa kwanza unaonekana wazi. Ili azoee mazingira yake mapya, kwa kawaida mahout wa kwanza humpeleka hadi kwenye makao yake mapya. Mahout wote wawili hufanya kazi pamoja hadi yule mpya anapoelewa vizuri hisia za tembo. Matatizo yanaweza kuwa makubwa zaidi mahout anapokufa na hivyo mwingine kuchukua usukani. Hata hivyo, mwishowe tembo hutambua na kuzoea hali hiyo mpya.

Ingawa huenda watu fulani wakamwogopa mnyama huyo mkubwa, tembo aliyezoezwa vizuri atamtii bwana mwenye fadhili. Anapotendewa kwa fadhili, si lazima tembo afungwe wakati mahout wake hayupo. Mahout anahitaji tu kuweka ncha moja ya kijiti chake kwenye mguu wa tembo na ncha ile nyingine ardhini na kumwamuru mnyama huyo asisonge. Tembo hutii na kusimama bila kusonga mahali kijiti kilipoachwa. Kama ilivyoonyeshwa mwanzoni mwa makala hii, ushirikiano kati ya tembo na mahout wake unaweza kuwa wenye kustaajabisha na wenye kugusa moyo. Naam, mzoezaji mzuri anaweza kumwamini tembo wake.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

MWANADAMU NA TEMBO WAMESHIRIKIANA KWA MUDA MREFU

Wanadamu wamefuga tembo tangu zamani. Huenda mfano unaojulikana zaidi katika nyakati za kale ni ule wa Hannibal, jenerali wa Karthage. Katika karne ya tatu K.W.K., jiji la Karthage lililo Afrika Kaskazini lilikuwa likipigana na Roma katika vita vilivyoitwa Vita vya Punic vilivyoendelea kwa miaka 100. Hannibal alikusanya jeshi katika jiji la Cartagena, Hispania, akiwa na mpango wa kwenda kushambulia Roma. Kwanza alivuka safu ya Milima ya Pyrenees ili aingie katika eneo ambalo sasa ni Ufaransa. Kisha, katika kile ambacho gazeti Archaeology kiliiita “mojawapo ya kampeni ya kijeshi yenye ujasiri zaidi katika historia,” jeshi lake la wanaume 25,000 likiwa na pamoja tembo 37 wa Afrika na wanyama wengine wengi waliobeba mizigo, lilivuka Milima ya Alps na kuingia Italia. Walihitaji kukabiliana na baridi, dhoruba za theluji, maporomoko ya mawe, na makabila ya milimani yenye uhasama. Safari hiyo ilikuwa ngumu kupita kiasi kwa tembo hao. Hakuna hata mmoja kati yao aliyekuwa hai baada ya mwaka mmoja wa Hannibal kuwa nchini Italia.

[Hisani]

© Look and Learn Magazine Ltd/The Bridgeman Art Library

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mahout anasugua ngozi ngumu lakini laini ya tembo wake

[Picha zimeandiliwa na]

© Vidler/mauritius images/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 16 zimeandiliwa na]

© PhotosIndia/age fotostock