Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Katika kipindi cha miaka 35 tangu 1970 hadi 2005, asilimia 25 ya samaki, amfibia, reptilia, ndege, na mamalia, walitoweka.—SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, UJERUMANI

Mnamo Agosti (Mwezi wa 8) 2008, Zimbabwe iliondoa sufuri kumi kutoka kwenye noti zake za benki katika jitihada za kukabiliana na inflesheni ya asilimia milioni 2.2. Kwa hiyo, noti ya dola bilioni 10 ilibadilishwa na kuwa dola moja ya Zimbabwe.—AGENCE FRANCE PRESSE, ZIMBABWE.

“Iliripotiwa kwamba zaidi ya watu 12,000 waliuawa kwa bunduki nchini Marekani mnamo 2005. Lakini idadi ya watu waliojeruhiwa kwa bunduki ni kubwa zaidi—karibu watu 53,000 walitibiwa katika vyumba vya matibabu ya dharura mnamo 2006.”—THE SEATTLE TIMES, MAREKANI.

Kuna Shangwe Wakati wa Krismasi?

Asilimia 20 hivi ya maombi ya talaka nchini Australia hutolewa mara tu baada ya kipindi cha Krismasi na Mwaka Mpya, linasema gazeti Sunday Telegraph la Sydney. “Sisi huwaona watu wengi sana wakipigana au kuachana na wakija ofisini mwetu mara tu tunaporudi kazini,” anasema wakili wa talaka Barry Frakes. “Watu hutazamia kwamba Krismasi itakuwa nzuri kama inavyoonyeshwa kwenye televisheni na matangazo ya kibiashara.” Anaongezea kusema kwamba maisha yao yasipopatana na mawazo ambayo watu huwa nayo kuhusu jinsi familia inavyopaswa kuwa, wao hutafuta talaka. Hata hivyo, kulingana na Angela Conway, msemaji wa Shirika la Masuala ya Familia la Australia, “mara nyingi talaka haisuluhishi matatizo ya muda mrefu au kuleta amani na furaha ambayo watu hufikiri italeta.” Anapendekeza hivi: “Ni vizuri kukaa katika ndoa na kujaribu kuifanikisha.”

“Nyumba za Kujifungua” Zinaokoa Uhai

Serikali ya Peru imejitahidi kupunguza idadi ya akina mama wanaokufa wanapojifungua. Ili kuwatia moyo akina mama wajawazito katika Milima ya Andes watafute matibabu katika kliniki badala ya kuzalia nyumbani, ‘nyumba 390 za kujifungua’ zimefunguliwa nchini Peru katika miaka kumi iliyopita. Mwanamke mjamzito na familia yake wanaweza kukaa katika mojawapo ya nyumba hizo, ambazo ziko karibu na kliniki, hadi atakapojifungua. Jambo moja linalofanya kliniki hizo zipendwe ni kwamba zinachanganya “matibabu ya kisasa na mazoea ya kitamaduni,” kama vile “mwanamke kuzaa akiwa amesimama,” jambo ambalo “hupunguza uchungu na wakati wa kuzaa . . . na humruhusu mama atazame vizuri zaidi mtoto wake akizaliwa kuliko anapozaa akiwa amelala,” inasema ripoti ya shirika la habari la Reuters kutoka Cuzco.

Zinachelewa Kila Wakati

Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Usafiri ya Marekani mnamo 2008 inasema kwamba asilimia 30 hivi ya safari za ndege nchini Marekani huchelewa kwa zaidi ya dakika 15. Ndege iliyochelewa zaidi ilikuwa ile iliyotoka Texas hadi California ambayo ilichelewa kwa saa 24.