Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ni Baraka au Laana?

Je, Ni Baraka au Laana?

Je, Ni Baraka au Laana?

Dereva anashindwa kulidhibiti gari lake na kugonga mlingoti na kumjeruhi vibaya abiria wake. Mara moja, anatumia simu yake ya mkononi kuomba msaada. Lakini kwa nini alishindwa kulidhibiti gari lake? Alikengeushwa fikira kidogo alipokuwa akijibu simu yake ya mkononi.

KAMA mfano huo unavyoonyesha, kifaa cha teknolojia kinaweza kuwa baraka au laana—uamuzi ni wako. Hata hivyo, watu wengi hawangependa kutumia vifaa vya zamani vilivyopitwa na wakati. Kwa mfano, kompyuta inatupunguzia kazi nyingi, inatuwezesha kununua vitu na kufanya shughuli za benki kupitia Intaneti, na hata inatuwezesha kuwasiliana na wengine.

Juzijuzi tu watu wa familia walikuwa wakiachana asubuhi na hawakuwasiliana tena hadi jioni. Lakini sasa, “asilimia 70 ya wenzi wa ndoa walio na simu za mkononi hupigiana simu kila siku ili kujuliana hali, asilimia 64 huwasiliana ili kupanga ratiba zao, na asilimia 42 ya wazazi huwasiliana na watoto wao kila siku kupitia simu ya mkononi,” inasema ripoti katika gazeti USA Today.

Usipuuze Madhara ya Teknolojia

Je, mtu anaweza kupata madhara ya kiakili na kimwili kwa kuitumia teknolojia kupita kiasi au vibaya? Fikiria mfano wa wenzi waliooana hivi karibuni katika nchi moja huko Ulaya. Kulingana na ripoti moja, wenzi hao “walikuwa wakiwasiliana kila mara kupitia simu za mkononi—wakiwa ndani ya magari yao, kwenye chumba cha kufanyia mazoezi, hata waliwasiliana kwa simu nyumbani wakiwa katika vyumba tofauti.” Pindi fulani, walizungumza kwenye simu kwa dakika 4,000 kwa mwezi, yaani, zaidi ya saa 66, na walisema kwamba hawawezi kuishi bila simu zao. Dakt. Harris Stratyner, mtaalamu wa matatizo ya akili alisema ni “wazi kwamba wana dalili za uraibu. Ni kana kwamba uhusiano wao unategemea kifaa fulani.”

Huenda mfano huo ukaonekana kuwa wenye kupita kiasi, lakini unaonyesha tabia inayozua wasiwasi. Watu wengi wanaona kwamba hawawezi kukaa bila kutumia mfumo fulani wa kuwasiliana hata kwa saa moja. “Kila mara tunahitaji kusoma barua pepe, kutumia Intaneti, na kuwatumia marafiki wetu ujumbe mfupi,” anasema mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 20 na kitu.

Ikiwa kutumia teknolojia “kunachukua wakati wako mwingi na ndilo jambo la maana zaidi unalopenda kufanya kuliko jambo lingine lolote, hiyo ni ishara ya wazi kwamba kuna shida fulani,” anasema Dakt. Brian Yeo katika gazeti The Business Times of Singapore. Isitoshe, mara nyingi watu wanaojitenga kwa saa nyingi sana ili kutumia vifaa vyao hawafanyi mazoezi ya kutosha na hivyo wanakabili hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kisukari, au magonjwa mengine mabaya.

Madhara mengine hutukia papo hapo. Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba watu wanaoendesha gari huku wakizungumza kwenye simu walizoshika mkononi au kwa kutumia vifaa vya kuzungumza bila kuishika, hawana uwezo kamili wa kudhibiti gari kama tu dereva anayeendesha akiwa amelewa! Pia, ni hatari kuandika ujumbe mfupi wa simu huku ukiendesha gari. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 40 hivi ya madereva walio na umri wa kati ya miaka 16 na 27 huandika ujumbe mfupi huku wakiendesha gari. Na pia, ikiwa unataka kutumia simu yako ya mkononi kuzungumza au kutuma ujumbe huku ukiendesha gari, kumbuka kwamba iwapo utapata aksidenti, polisi na kampuni ya bima watachunguza ikiwa simu yako ilikuwa ikitumiwa muda mfupi kabla ya aksidenti hiyo. Kuzungumza kwenye simu au kuandika ujumbe mfupi kunaweza kukugharimu sana! * Uchunguzi uliofanywa baada ya aksidenti ya gari-moshi iliyosababisha vifo vya watu 25 iliyotokea mwaka wa 2008 huko California, Marekani, ulionyesha kwamba dereva alikuwa ametuma ujumbe mfupi sekunde chache tu kabla ya aksidenti hiyo. Hata hakuwa na wakati wa kufunga breki.

Kwa sababu watoto wengi hutumia simu za mkononi na kompyuta, na pia vifaa vingine vya teknolojia, wanahitaji kujifunza jinsi ambavyo wanaweza kutumia vifaa hivyo vizuri. Wanaweza kusaidiwa jinsi gani? Tafadhali soma makala inayofuata.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Wote wanaojitahidi kuishi kupatana na mafundisho ya Biblia wanapaswa kuwa waangalifu wasikengeushwe na kitu chochote kinachoweza kusababisha hali yoyote hatari.—Mwanzo 9:5, 6; Waroma 13:1.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Je, kutumia teknolojia kunachukua wakati wako mwingi?