Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Mungu wa Wakristo huko Marekani hajafa, lakini katika miaka ya karibuni hana uvutano sana katika siasa zetu na tamaduni zetu.”—NEWSWEEK, MAREKANI.

“Msukosuko na kuzorota kwa uchumi kunatokeza aina nyingine ya waathiriwa: Wenzi waliooana ambao hawawezi kulipia talaka. Katika wakati huu mgumu, watu wengi wameamua kuishi pamoja hata kama hawawezi kuvumiliana.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.

Mama 1 kati ya 3 waliohojiwa nchini Ujerumani hujifunza kutoka kwa binti yake—kuhusu mitindo, urafiki, kuwa mtulivu, na kujiheshimu zaidi.—BERLINER MORGENPOST, UJERUMANI.

Bado Wana Kingamwili

“Miaka 90 baada homa hatari zaidi katika historia kutokomea, bado damu ya waokokaji ina kinga yenye nguvu nyingi sana dhidi ya virusi vya homa hiyo ya mwaka wa 1918, ikionyesha uwezo wa kudumu wa mfumo wa kinga wa mwanadamu,” linasema gazeti International Herald Tribune. Wanasayansi walipochunguza damu ya wakongwe waliookoka homa ya Hispania, walipata kwamba “bado wana kingamwili ambazo zilikuwa zikitafuta kuangamiza virusi vya homa hiyo.” Watafiti walitumia kingamwili hizo kutengeneza chanjo inayoweza kutibu panya waliodungwa virusi vya homa hiyo hatari. Watafiti hao walishangazwa na uwezo wa kuhifadhi habari wa mfumo wa kinga. Mtafiti mmoja alisema hivi kwa mshangao: “Bwana ametubariki na kingamwili maisha yetu yote! Kile kisichoweza kukuua kinakufanya uwe na nguvu hata zaidi.”

Maswali kwa Mungu

“Kwa nini tunateseka sana ikiwa wewe ni mtu mzuri?” Hilo ndilo swali la kwanza ambalo wanafunzi katika chuo cha Sweden wangemwuliza Mungu ikiwa wangekuwa na nafasi ya kufanya hivyo, linasema gazeti Dagen la Sweden. Uchunguzi mmoja ulionyesha kuwa maswali ya kawaida ambayo watu huuliza yalitia ndani: “Ni nini kusudi la uhai?” na “Ni nini kitakachotukia baada ya kifo?” Watu wengi nchini Sweden hawapendezwi na mambo ya dini. Hata hivyo, “bado maswali hayo huzuka,” akasema mwakilishi wa shirika la wanafunzi Wakristo ambao walifanya uchunguzi huo. “Vijana hutafakari maswali kama hayo.”

Ulemavu Huongeza Furaha Katika Ndoa

Watafiti wanasema kuwa “wenzi wa ndoa, waume kwa wake—hata wawe na umri gani—wameripotiwa kuwa na furaha zaidi katika ndoa baada ya kupata ulemavu fulani.” Kupoteza uwezo wa kufanya kazi za kila siku kunaweza kuongeza mkazo, lakini pia kunaweza kuwaunganisha wenzi. Hasa wanaume wazee wameripoti kwamba wao hutumia wakati mwingi zaidi na wenzi wao. Karen Roberto mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kuzeeka katika Chuo cha Virginia, huko Marekani, alisema hivi: “Kuchukua majukumu ya kuwatunza wenzi wao na wajibu ambao huenda ukaonekana kuwa mpya au kuukazia fikira zaidi kuliko wakati uliopita katika ndoa yao, huwapa wanaume nafasi ya kuwategemeza na kutumia wakati mwingi zaidi na wake zao na hilo hufanya wathamini hata zaidi uhusiano wao.”