Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maisha Yangu Yamekuwa Yenye Kuridhisha

Maisha Yangu Yamekuwa Yenye Kuridhisha

Maisha Yangu Yamekuwa Yenye Kuridhisha

Limesimuliwa na Herawati Neuhardt

Nilizaliwa huko Cirebon, Indonesia, jiji linalojulikana sana kwa vitambaa vya batiki vilivyopambwa kwa kutiwa rangi ya michoro mbalimbali. Kwa njia fulani, maisha yangu nikiwa mmishonari yamekuwa kama kitambaa cha batiki kwa kuwa nimekutana na watu wa tamaduni mbalimbali wanaoishi Kusini-Mashariki mwa Asia na Pasifiki ya Kusini. Acha nisimulie.

KATIKA mwaka wa 1962, nilipokuwa na umri wa miaka kumi, mama yangu alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Baada ya muda, yeye na baba yangu, ambao ni Wachina waliozaliwa Indonesia, pamoja na sisi watoto watano tukawa Mashahidi.

Wamishonari na waangalizi wanaosafiri waliishi nyumbani kwetu walipotembelea kutaniko letu ili kututia moyo. Mfano wao mzuri na mazungumzo yao yenye kujenga yalinichochea sana. Nilipokuwa na umri wa miaka 19, niliamua kuwa mhudumu Mkristo wa wakati wote. Mwaka mmoja hivi baadaye, niliolewa na Josef Neuhardt, mmishonari Mjerumani ambaye aliyekuja Indonesia mwaka wa 1968. Baada ya fungate, tulihamia Sumatra, kisiwa cha pili kwa ukubwa kati ya visiwa zaidi ya 17,000 vya Indonesia. Tukiwa huko, niliandamana na Josef katika kazi yake ya kutembelea makutaniko ya Mashahidi wa Yehova akiwa mwangalizi anayesafiri.

Kuhubiri Sumatra

Mzunguko wetu, au eneo tulilogawiwa lilianzia jiji lenye joto na shughuli nyingi la Padang, Sumatra Magharibi, hadi kwenye Ziwa Toba, ziwa maridadi lililotokezwa na mlipuko wa volkano ambalo lilikuwa kwenye nyanda za juu huko Sumatra Kaskazini. Baadaye tuligawiwa eneo la kusini kwenye kisiwa hicho. Kila mara tulikuwa safarini katika gari letu dogo la Volkswagen, tukipitia barabara za msituni zilizokuwa na mashimo, tukivuka madaraja yenye kutikisika yaliyojengwa kwa minazi, na kupita kando ya milima mikubwa ya volkano, ambayo mingine ilikuwa haitendi na mingine ilikuwa hai. Usiku tulilala sakafuni katika nyumba ambazo hazikuwa na umeme, vyoo, au bafu. Tulioga na kuosha nguo zetu kwenye maziwa na mito. Tuliishi maisha rahisi na tuliwapenda watu. Watu walitukaribisha kwa uchangamfu na kutulisha, na wengi wao walipendezwa na Biblia.

Katika eneo la Padang, watu wa Minangkabau, ambao wengi wao ni Waislamu, walishangaa na kufurahi tulipowaonyesha katika Biblia kwamba Mungu ni mmoja—si Utatu, kama dini zinazodai kuwa za Kikristo zinavyofundisha. (Kumbukumbu la Torati 6:4) Watu wengi walifurahia magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni!, na baadaye wengine waliopendezwa walifanya maendeleo mazuri ya kiroho. Katika eneo la Ziwa Toba, Wabatak, ambao wengi wao walidai kuwa Wakristo, walijua jina la Mungu, Yehova, kwa kuwa waliliona katika Biblia yao ya Kibatak. (Zaburi 83:18) Hata hivyo, walihitaji uelewaji zaidi kumhusu Mungu na kusudi lake kwa wanadamu. Wengi wao walikubali kujifunza Biblia na wakawa Wakristo waeneza-injili wenye bidii.

Kugusa Mioyo ya Watu Huko Java

Mnamo 1973, mimi na Josef tulipewa mgawo huko Java, kisiwa kilicho nusu ya ukubwa wa Uingereza, kilichokuwa na wakazi zaidi ya milioni 80. * Tuliwahubiria Wajava, Wasunda, na watu wa makabila mbalimbali ya Kichina.

Kwa kuwa nililelewa na wazazi Wachina waliozaliwa Indonesia, nilizungumza lugha mbalimbali kama vile Kijava, Kisunda, na Kiindonesia, na pia Kiingereza. Kwa sababu hiyo, nilifurahia kuzungumza kuhusu Biblia na watu katika lugha yao ya kienyeji.

Huko Jakarta, mji mkuu wa Indonesia ambao uko kwenye kisiwa cha Java, nilimweleza msichana mmoja mwenye umri wa miaka 19 aliyeonekana kuwa ameshuka moyo kuhusu tumaini la kuishi milele katika Paradiso duniani. Nilipokuwa nikisoma Biblia, alianza kulia. “Asante sana shangazi kwa kuniambia mambo hayo,” akaniambia huku akitumia neno linaloashiria upendo na heshima. Kisha akaongezea hivi: “Ninahitaji rupia nyingine milioni 1.5 [dola 160 za Marekani] kufikia kesho ili kulipa karo ya chuo kikuu, na nilikuwa nimefikiria kuuza ubikira wangu ili nipate pesa hizo. Nilikuwa tu nimetoka kusali nipate mwongozo. Sasa nimepata jibu. Nimeamua kuahirisha masomo yangu na kubaki safi kiadili.” Msichana huyo alifurahia kujifunza mengi kutoka kwa Biblia.

Tangu wakati huo, Wajava wengi, kutia ndani Wasunda na Wachina, wamepatanisha maisha yao na viwango vya Neno la Mungu. Hilo limewaletea amani ya akili na furaha kama vile Mungu anaahidi.—Isaya 48:17, 18.

Kalimantan—Makao ya Wadayak

Kutoka Java, mimi na Josef tulihamia Kalimantan, mkoa wa Borneo huko Indonesia, ambacho ndicho kisiwa cha tatu kwa ukubwa ulimwenguni (baada ya Greenland na New Guinea). Kisiwa hicho cha Borneo chenye misitu mikubwa, milima yenye miamba, na mito mikubwa, ni makao ya Wachina, Wamalay Waislamu, na Wadayak ambao ni wenyeji wa huko wanaoishi kando ya mito na wakati mmoja walikuwa wakiwakata adui zao vichwa.

Ili kufika maeneo ya mbali ya Wadayak, tulisafiri kwa mashua au mtumbwi kwenye mito safi iliyopitia msituni. Mamba wakubwa waliota jua kwenye kingo za mto, tumbili walitutazama kutoka kwenye miti, na ndege walipeperusha manyoya yao yenye rangi za kupendeza. Naam, utumishi wa umishonari huko ulisisimua sana!

Wadayak wengi waliishi kwenye nyumba zilizojengwa juu ya nguzo kwa vifaa vinavyopatikana msituni. Nyumba fulani zilikuwa ndogo; nyingine zilikuwa ndefu na familia kadhaa ziliishi humo. Watu wengi hawakuwa wamewahi kumwona mzungu, kwa hiyo watu walitaka sana kumwona Josef. Watoto walikimbia kijijini wakisema, “Pasta! Pasta!” Kisha watu walikusanyika kumsikiliza mhudumu huyo mzungu. Josef aliwahubiria kupitia Mashahidi wenyeji ambao walimtafsiria na baadaye wakapanga kujifunza Biblia na wengi waliopendezwa.

Mgawo Mpya Papua New Guinea

Kwa sababu ya kushinikizwa na wapinzani wa kidini, serikali ya Indonesia iliwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova mnamo Desemba (Mwezi wa 12) 1976. Kwa hiyo, mimi na Josef tulipewa mgawo huko Papua New Guinea.

Tulipowasili mji mkuu wa Port Moresby, tulijifunza lugha ya Hiri Motu kwa miezi miwili ambayo inatumiwa katika biashara. Kisha tukahamia Daru, kisiwa kidogo kilicho mbali kwenye mkoa wa magharibi. Nikiwa huko, nilikutana na Eunice, mwanamke mnene, mwenye nguvu, mwenye utu wa kupendeza, ambaye meno yake yalikuwa meusi kwa sababu ya kutafuna tambuu kwa miaka mingi. Eunice alipojifunza kwamba Mungu anataka watumishi wake wawe safi kimwili na pia kiadili na kiroho, aliacha uraibu huo na kuwa Mkristo mwaminifu. (2 Wakorintho 7:1) Kila mara tulipoona watu wanyenyekevu wakifuata mashauri ya Biblia maishani, tuliona ukweli wa maneno haya ya Zaburi 34:8: “Onjeni mwone ya kuwa Yehova ni mwema.”

Baada ya muda, Josef aliwekwa rasmi tena kuwa mwangalizi anayesafiri, na tulitembelea karibu kila sehemu ya Papua New Guinea, nchi iliyo na lugha 820 hivi. Ili tuwafikie watu wengi zaidi, tulijifunza lugha nyingine, yaani, lugha ya Tok Pisin, ambayo hutumiwa katika mawasiliano nchini humo. Ili kufikia miji na vijiji mbalimbali, tulitembea kwa miguu, tukasafiri kwa mashua, mtumbwi, na kwa ndege ndogo, na kuvumilia joto kali, mbu, na malaria.

Kisha katika mwaka wa 1985, tulikubali mgawo mwingine wa umishonari katika Visiwa vya Solomon, vilivyoko mashariki ya Papua New Guinea. Tukiwa huko tulifanya kazi katika ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova na pia tulisafiri kotekote kwenye visiwa hivyo ili kuyatia moyo makutaniko na kuhudhuria makusanyiko ya Kikristo. Kwa mara nyingine tena, ilibidi tujifunze lugha mpya—wakati huu tulijifunza Kipijini cha Visiwa vya Solomon. Tulifurahia sana kuzungumza na wakazi wa Visiwa vya Solomon wanaopenda Biblia!

Safari Ngumu Zaidi

Mnamo 2001, serikali ya Indonesia iliondoa marufuku dhidi ya Mashahidi wa Yehova, nasi tukarudi Jakarta. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kurudi, iligunduliwa kwamba mume wangu mpendwa alikuwa na kansa ya ngozi ambayo huenea haraka. Tulienda Ujerumani nyumbani kwa Josef ili apate matibabu. Lakini, kwa kuhuzunisha, mnamo 2005, miaka 33 tangu tulipofunga ndoa, alilala katika usingizi wa kifo na sasa anasubiri wakati atakapofufuliwa katika ulimwengu mpya utakaokuwa Paradiso. (Yohana 11:11-14) Alikuwa na umri wa miaka 62 na alikuwa ametumika katika utumishi wa wakati wote kwa miaka 40.

Nilibaki Jakarta, ambako ninaendelea kutumika nikiwa mmishonari. Ninamkosa sana mume wangu mpendwa. Lakini kuwafundisha wengine kweli zenye thamani zinazopatikana katika Neno la Mungu kumenisaidia kukabiliana na hali hiyo, kwa kuwa kuhubiri hunipa uradhi na kusudi maishani. Kwa kweli, Yehova amenipa maisha yenye kupendeza na yenye kuridhisha.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Leo Java ina watu zaidi ya milioni 120.

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

INDONESIA

Java

JAKARTA

Cirebon

Sumatra

Padang

Ziwa Toba

Borneo

PAPUA NEW GUINEA

PORT MORESBY

Daru

VISIWA VYA SOLOMON

[Picha katika ukurasa wa 26]

Herawati akiwa na wanafunzi wa Biblia katika Visiwa vya Solomon

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nikiwa na Josef huko Uholanzi, kabla tu ya kifo chake mwaka wa 2005