Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Njia ya 4—Linda Afya Yako

Njia ya 4—Linda Afya Yako

Njia ya 4—Linda Afya Yako

“Mtu mwerevu ni yule ambaye ameona msiba na kujificha.” (Methali 22:3) Kuchukua hatua rahisi za kujilinda kunaweza kukusaidia uepuke magonjwa na kuteseka kwingi, na pia kupoteza wakati na pesa.

◯ Dumisha usafi. “Kunawa mikono ndilo jambo moja muhimu unaloweza kufanya ili kuzuia kuenea kwa maambukizo na kuwa na afya na hali njema,” inasema ripoti ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa ya Kuambukiza vya Marekani. Asilimia 80 hivi ya maambukizo huenezwa kupitia mikono michafu. Kwa hiyo, nawa mikono mara nyingi iwezekanavyo kila siku. Fanya hivyo hasa kabla ya kutayarisha chakula, au kugusa au kusafisha kidonda, na pia baada ya kumgusa mnyama, kwenda msalani, au kumbadili mtoto nepi.

Kunawa kwa kutumia sabuni ni bora kuliko kutumia kemikali za kuua viini zilizo na alkoholi. Watoto watakuwa na afya bora ikiwa wazazi watawazoeza kunawa mikono na kutogusa midomo na macho yao kwa mikono. Kuoga kila siku na kuwa na nguo na matandiko safi pia kutachangia kuwa na afya bora.

◯ Epuka magonjwa ya kuambukizwa. Epuka kuwa karibu au kutumia vyombo vya kulia vya mtu mwenye mafua au homa. Mate yao na umajimaji unaotoka puani unaweza kukuambukiza magonjwa hayo. Magonjwa yanayoambukizwa kupitia damu kama vile mchochota wa ini aina ya B na C na UKIMWI hupitishwa kupitia ngono, kutumia sindano kujidunga dawa za kulevya, na kutiwa damu mishipani. Chanjo zinaweza kuzuia maambukizo fulani, lakini bado mtu mwenye hekima atachukua hatua zinazofaa za kujilinda anapokuwa karibu na mtu mwenye ugonjwa wa kuambukizwa. Epuka kuumwa na wadudu. Usiketi au kulala nje bila kinga wakati kuna mbu wengi au wadudu wengine wanaoeneza magonjwa. Tumia chandarua cha kuzuia wadudu, hasa kwa ajili ya watoto, na ujipake dawa ya kuzuia wadudu. *

◯ Hakikisha nyumba yako ni safi. Jitahidi sana kudumisha nyumba yako ikiwa nadhifu na safi, ndani na nje. Hakikisha kwamba maji hayajikusanyi mahali popote na hivyo kufanya mbu wazaane. Takataka, uchafu, na vyakula ambavyo havijafunikwa huvutia wadudu na wanyama wenye viini ambavyo husababisha magonjwa. Ikiwa hakuna choo, jenga choo cha shimo badala ya kwenda choo shambani. Funika shimo la choo ili kuzuia nzi ambao hupitisha maambukizo ya macho na magonjwa mengine.

◯ Epuka kujijeruhi. Fuata sheria za usalama unapofanya kazi, unapoendesha baiskeli, pikipiki, au gari. Hakikisha kwamba gari lako ni salama. Vaa nguo za kujikinga na vifaa vinavyofaa vya kujikinga kama vile miwani, kofia, viatu, na pia mikanda ya usalama na vifaa vya kulinda masikio. Epuka kukaa kwenye jua kwa muda mrefu kwa kuwa hilo husababisha kansa na pia kufanya ngozi ipate makunyazi mapema. Ikiwa wewe huvuta sigara, acha. Kuacha sasa kutapunguza sana hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo, kansa ya mapafu, na kiharusi. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Ona makala zenye kichwa, “Jinsi ya Kuacha Kuvuta Sigara,” katika toleo la Amkeni! la Mei 2010.