Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Katika mwaka wa kwanza na nusu wa kampeni ya kukomesha biashara ya kuuza watu, “polisi nchini China waliwaokoa wanawake 10,621 na watoto 5,896 waliokuwa wametekwa nyara.” Washukiwa 15,673 hivi walikamatwa.—CHINA DAILY, CHINA.

“Zaidi ya walimu 1,000 nchini Kenya wamefutwa kazi kwa sababu ya kuwatendea wasichana wa shule vibaya kingono katika miaka miwili iliyopita. . . . Kituo fulani cha kitaifa cha siri . . . kilikuwa kimeonyesha kwamba tatizo hilo lilikuwa limeenea kwa kadiri kubwa zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.”—DAILY NATION, KENYA.

Kulingana na uchunguzi mmoja, watu ambao wametumia vitanda vinavyotokeza mnururisho wa jua wana uwezekano wa asilimia 75 zaidi wa kupata kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi kuliko wale ambao hawajawahi kuvitumia. Wale ambao wametumia vifaa kama hivyo kwa zaidi ya saa 50 wanaweza kupata kansa hiyo ya chembe za ndani za ngozi kwa urahisi zaidi.—CANCER EPIDEMIOLOGY, BIOMARKERS & PREVENTION, MAREKANI.

“Ni asilimia 8 tu [ya wanawake wanaokaribia kufunga ndoa nchini Kanada] ambao hufikiri kwamba inafaa kuepuka kufanya ngono kabla ya ndoa,” na “asilimia 74 ya wapenzi huishi pamoja kabla ya kufunga ndoa.”—WEDDINGBELLS, KANADA.

Athari za Kutumia Maji Machafu

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, “watu wanaokufa sasa kutokana na maji machafu ni wengi zaidi kuliko wale wanaokufa kutokana na aina zote za uhalifu kutia ndani vita.” Ripoti hiyo inasema kwamba tani milioni mbili za takataka—iwe ni kutoka kwenye mashamba na viwanda, pamoja na maji-taka—humwagwa kila siku kwenye mito na bahari, na hivyo kueneza magonjwa na kuharibu mazingira. Zaidi ya hayo, mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitano hufa kila baada ya sekunde 20, kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji machafu. Achim Steiner, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, anasema hivi: “Ikiwa tungependa ulimwengu uendelee, . . . sote tunapaswa kushirikiana na kutumia akili zaidi ili tupunguze na kuondoa takataka tunazotokeza.”

Kuimba Kunasaidia Kurudisha Uwezo wa Kusema

Baadhi ya wagonjwa ambao wamepoteza uwezo wao wa kusema baada ya kupatwa na kiharusi wamesaidiwa kuupata tena kwa kuimba. Wataalamu wa mfumo wa neva huwatia moyo watu waliopatwa na kiharusi wapange fikira zao kwa njia ya muziki na kuimba maneno hayo badala ya kuyasema tu. Matibabu hayo yanayojulikana kama matibabu ya kutumia muziki, yamekuwa na matokeo mazuri sana. Baada ya kutibiwa kwa majuma 15, “hatua kwa hatua wagonjwa hujifunza kuzungumza kwa kutumia maneno waliyokuwa wameimba,” linasema gazeti The Wall Street Journal.

‘Wanafunzi Wengi Zaidi Wanaiba Mitihani’

Kulingana na uchunguzi uliofanyiwa wanafunzi 20,000 wa mwaka wa kwanza wa chuo kikuu nchini Kanada, asilimia 73 “walikiri kwamba waliiba katika mtihani mmoja au zaidi walipokuwa katika shule ya sekondari,” linasema Baraza la Masomo la Kanada (CCL). Chuo kimoja kikuu kiliripoti kwamba visa vya kuiba mitihani viliongezeka kwa asilimia 81 kati ya mwaka wa 2003 na 2006. Dakt. Paul Cappon, msimamizi wa CCL, anasema kwamba “katika miaka kumi iliyopita, Intaneti pamoja na vifaa vya kiteknolojia vimechangia sana wanafunzi zaidi kuiba mitihani.”