Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wanaweza Kuokolewa Wasitoweke?

Je, Wanaweza Kuokolewa Wasitoweke?

Je, Wanaweza Kuokolewa Wasitoweke?

KATIKA mwaka wa 2002, shirika la Umoja wa Mataifa lilitangaza kwamba limejiwekea mradi wa kuhakikisha kwamba baada ya miaka kumi litakuwa limepunguza kiwango ambacho viumbe vinatoweka na mazingira kuharibiwa. Kupatana na mradi huo, mwaka wa 2010 ungekuwa Mwaka wa Kimataifa wa Unamna-namna wa Viumbe.

Kwa kusikitisha, mwaka huo ulipofika hakukuwa na dalili zozote za kuufikia mradi huo. “Kwa sababu ya shughuli za wanadamu,” inasema ripoti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), “aina mbalimbali za viumbe zinatoweka mara 1,000 zaidi ya inavyopaswa kuwa.” Gazeti la New Zealand Herald lilifafanua mambo wazi zaidi kwa kusema: “Ulimwenguni pote sasa, moja kati ya jamii tano za mimea, moja kati ya jamii tano za mamalia, moja kati ya jamii saba za ndege, na moja kati ya jamii tatu za amfibia zimo katika hatari ya kutoweka.” Tutafahamu vizuri zaidi jambo linalosababisha hali hiyo tunapochunguza mambo yaliyotukia baada ya karne kadhaa huko New Zealand.

Unamna-namna wa Viumbe Huko New Zealand

Kabla ya watu kuanza kuishi New Zealand, mazingira yake yalisitawi vizuri. Hata hivyo, watu wa kwanza kuhamia huko walipeleka viumbe ambao walileta madhara makubwa kwa mimea na wanyama walioishi huko. Kwa mfano, Wamaori walivuka Bahari ya Pasifiki wakiwa na mbwa na pengine kiore (au panya wa Polinesia), ambao waliliwa.

Halafu, katika karne ya 17 na ya 18, Wazungu waliwasili na panya wengine wa aina mbili na paka​—ambao baadaye walikuja kuwa paka-mwitu. Wazungu pia walikuja na mbuzi, nguruwe, na paa kwa ajili ya chakula. Katika karne ya 19, walileta pia kifaurongo mwenye mkia kama brashi (brush-tailed possum) na sungura​—kwa ajili ya chakula na manyoya​—bila kufikiria jinsi ambavyo wanyama hao wangeathiri miti, ndege, na mimea.

Kufikia miaka ya 1860, idadi ya sungura ilikuwa imeongezeka kwa kiasi kisichoweza kudhibitiwa, kwa hiyo mnyama wa jamii ya kicheche wa Ulaya akaletwa. Hata hivyo, vicheche hao wakapendelea kula ndege wenyeji walioshikika kwa urahisi badala ya kufukuza sungura wenye mbio. Kwa sababu hiyo, idadi ya sungura ikazidi kuongezeka.

Idara ya Kuhifadhi Mazingira ya New Zealand inaripoti kwamba kwa sababu ya kuwa na wanyama wengi hivyo waharibifu, asilimia 9 kati ya 10 ya makinda ya kiwi wa rangi ya kahawia wanaozaliwa mwituni watakufa kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja. Tayari jamii kadhaa zimetoweka: zaidi ya jamii 40 za ndege; jamii 3 za vyura; jamii 1 ya popo; na angalau jamii 3 za mijusi​—hali kadhalika jamii nyingi za wadudu. Zaidi ya nusu ya jamii 5,819 za mimea na za wanyama wa asili wa New Zealand zimeorodheshwa kuwa hatarini, na hilo linafanya viumbe wa mwituni wa nchi hiyo kuwa miongoni mwa wale wanaokabili hatari kubwa zaidi ya kutoweka.

Jitihada Nzuri

Sasa, mashirika ya kiserikali yako makini sana kuzuia mimea na wanyama hatari wasiingie nchini New Zealand. Kwa kuongozea, Idara ya Kuhifadhi Mazingira imefanya jitihada za kuangamiza jamii za wadudu na wanyama waharibifu, hasa kwenye visiwa, na pia imeanzisha hifadhi za wanyama wa porini.

Mojawapo ya visiwa vilivyoshughulikiwa kwa njia hiyo ni kile cha Tiritiri Matangi, kwenye Rasi ya Whangaparaoa iliyo kwenye pwani ya Auckland. Eneo hilo lilipandwa miti 280,000 hivi ya asili baada ya panya wote kuangamizwa mwaka wa 1993, na sasa linalindwa, na wageni wanaruhusiwa kuzuru na kufurahia sauti mbalimbali za jamii za ndege wa asili ambao wamerudishwa, kutia ndani ndege aina ya saddleback, takahe, kokako, rifleman, na stitchbird. Kwa sababu mazingira wanayoishi hayana wawindaji, viumbe hao maridadi huwaruhusu wageni wanaotembea kufurahia kuwatazama wakiwa karibu sana.

Katika mwaka wa 2003 Kisiwa cha Campbell kilichoko kaskazini mwa Aktiki kilitangazwa kuwa huru kutokana na panya baada ya kampeni ya miaka miwili ya kuwaangamiza. Tangu wakati huo, mimea ya asili imeanza kusitawi tena na ndege wa baharini wameanza kurudi. Hata teal wa Kisiwa cha Campbell​—aina ya bata ambao hawapatikani kwa urahisi—wamerudishwa tena kisiwani humo.

Hivi majuzi, mradi mkubwa wa ukarabati ulianza katika visiwa vya Rangitoto na Motutapu na kwenye Ghuba ya Hauraki ya Auckland. Lengo la mradi huo ni kuulinda msitu mkubwa zaidi duniani unaoitwa Pohutukawa na kuwatunza viumbe wa asili waliorudishwa tena. Baada ya kuangamiza wanyama wengi waharibifu​—kutia ndani sungura, kicheche wa Ulaya, kalunguyeye, paka-mwitu, panya wa Norway, na aina nyingine za panya​—kasuku wa rangi nyekundu na ndege-mpiga kengele waligunduliwa baada ya kutoweka kwa karne nzima!

Mifano hii inaonyesha mambo yanayoweza kufanywa ili viumbe walio hatarini warudishwe na jinsi ambavyo makosa ya zamani yaliyofanywa bila kufikiria wakati ujao yanavyoweza kushughulikiwa. Watu wote wanaopenda mazingira wanaweza kutazamia kwa hamu ahadi ya Biblia ya kwamba Yehova Mungu, “Mtengenezaji wa mbingu na dunia,” atakomesha mazoea yanayoharibu mazingira yetu, kutia ndani viumbe wa mwituni.​—Zaburi 115:15; Ufunuo 21:5.

[Blabu katika ukurasa wa 25]

Kwa sasa, makinda 9 kati ya 10 ya kiwi hufa kabla ya kumaliza mwaka mmoja

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

KUTUMIA RASILIMALI KWA HEKIMA

Changamoto ambayo wale wanaotaka kuhifadhi mazingira ulimwenguni hupata hasa ni kwamba viumbe wengi zaidi wanazidi kutoweka, na hakuna rasilimali za kutosha kusuluhisha tatizo hilo. Mbinu moja wanayotumia inaitwa conservation triage, ambayo inafanana na mbinu inayotumiwa katika vyumba vya kushughulikia hali za dharura hospitalini ulimwenguni pote ya kushughulikia kwanza wale walio mahututi zaidi. Mbinu hiyo ambayo pia inaitwa ecological triage hufanya kazi kwa kujaribu kukusanya rasilimali na kuzielekeza mahali ambapo kuna matokeo zaidi, hasa kwa kuzingatia mambo kama vile (1) thamani inayokadiriwa ya viumbe wenyewe au eneo wanamoishi, (2) uwezekano wa kufanikiwa kwa mradi, na (3) gharama inayohusika. Ingawa si kila mtu anayekubaliana na mbinu hiyo, wanaounga mkono mpango huo wanadai kuwa unasaidia kutumia vizuri mali zilizopo, na hivyo kukazia uangalifu mahali ambapo kutakuwa na matokeo mazuri zaidi.

[Ramani katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NEW ZEALAND

Ghuba ya Hauraki

Kisiwa cha Tiritiri Matangi

Rangitoto na Motutapu

Kisiwa cha Campbell

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kiwi wa rangi ya kahawia

[Picha Hisani]

© S Sailer/​A Sailer/​age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 27]

“Takahe” aliyekomaa kwenye Kisiwa cha Tiritiri Matangi

[Picha katika ukurasa wa 27]

Kisiwa cha Campbell

[Picha Hisani katika ukurasa wa 27]

Takahe: © FLPA/​Terry Whittaker/​age fotostock; Campbell Island: © Frans Lanting/​CORBIS