Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jeuri Hutuumiza Sisi Sote

Jeuri Hutuumiza Sisi Sote

Jeuri Hutuumiza Sisi Sote

NI NANI ambaye hajawahi kuathiriwa na jeuri? Tunaiona kila siku katika ripoti za habari. Tunaogopa kutendewa kwa jeuri tukiwa barabarani na kazini, na watoto huogopa kutendewa kwa jeuri na watoto wachokozi shuleni. Hata nyumbani, mahali ambapo kwa kawaida watu huhisi wakiwa salama, mamilioni ya watu​—hasa wanawake​—huhisi kwamba hawako salama. Kwa kweli, ikitegemea nchi, asilimia 70 hivi ya wanawake wanaripoti kwamba wameshambuliwa na mtu ambaye wanaishi pamoja kama mwenzi wa ndoa.

Katika nchi nyingi, watu wanaogopa maasi yenye jeuri ya kisiasa au kijamii au hata ugaidi. Unaweza kutambua kwamba watu wana hofu kwa sababu vifaa vya hali ya juu vya upelelezi vimeongezeka katika nchi fulani, na hasa katika nchi ambazo zimewahi kukumbwa na ugaidi.

Inaeleweka ni kwa nini biashara ya kuuza vifaa vya video vya kupeleleza inanawiri, licha ya kuzorota kwa uchumi ulimwenguni pote. Ni nani anayelipia gharama ya vifaa hivyo vyote? Sisi sote tunavilipia wakati ambapo tunalipa kodi na malipo mengine. Na gharama hizo zitaongezeka kadiri mbinu za kuimarisha usalama zitakavyozidi kuwafanyia watu upelelezi wa ndani zaidi, zitakavyozidi kuenea, na kuwa ghali zaidi.

Athari za jeuri zinapaswa kutufanya tujichunguze zaidi​—tuchunguze maadili yetu na mambo tunayoamini. Makala zinazofuata zitajibu maswali haya: Vyombo vya habari vinachangiaje kuenea kwa jeuri? Ni mambo gani yanayoweza kuathiri mtazamo wetu kuelekea jeuri? Tunaweza kujilindaje dhidi ya mambo hayo yasiyofaa?