Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watunza-Bustani Wanaoruka Katika Misitu ya Mvua

Watunza-Bustani Wanaoruka Katika Misitu ya Mvua

KAMA watunza-bustani wanavyojua, ili mbegu iote vizuri inahitaji kupandwa mahali panapofaa na wakati unaofaa. Hata hivyo, inashangaza kwamba mbegu hupandwa kwa wingi sana na viumbe wanaoruka usiku katika misitu ya mvua. Watunza-bustani hao ambao hupanda mbegu ni popo aina ya Old World, na baadhi yao huitwa mbweha wanaoruka. *

Kusambaza Mbegu

JE, WAJUA? Tofauti na popo wengine, popo wanaokula matunda hawategemei mawimbi ya sauti ili kutafuta chakula, badala yake wao hutumia uwezo wa kuona na kunusa. Macho yao makubwa huwasaidia kuona usiku

Popo wengi wanaokula matunda huruka usiku kwenye miti ili kutafuta matunda na nekta ya maua. Wakiwa angani, popo hao hula matunda na kuangusha kinyesi chenye mbegu na maganda. Pia, kazi yao ya kutunza bustani inahusisha kuchavusha maua wanapotafuta nekta wanayopenda sana.

Kwa kuwa popo hao husafiri mwendo mrefu usiku, wanaweza kusambaza mbegu kwenye eneo kubwa sana. Na kwa kuwa mbegu fulani hupatikana katika kinyesi chao, wanatokeza “mbolea” inayosaidia mbegu kukua. Haishangazi kwamba mimea mingi katika misitu ya mvua hutegemea popo ili kuchavusha maua au kusambaza mbegu.

 Kwa kuwa wanasafiri mbali, popo wanaokula matunda wanahitaji ustadi wa kusafiri na uwezo wa kuona vizuri. Gizani popo hao wanaweza kuona vizuri kuliko wanadamu. Hata wanaweza kutofautisha rangi. Na wanaweza kusafiri mchana na pia usiku.

Maisha ya Familia

Popo aina ya Samoan flying fox (Pteropus samoensis) huwa na mwenzi mmoja maisha yote. Katika jamii fulani, popo wa kike humtunza vizuri sana mtoto wake, akimbeba kwa majuma kadhaa na kumnyonyesha mpaka anapokomaa. Aina fulani ya popo wa kike hutafuta huduma za “mzalishaji” wakati wa kujifungua.

Kwa kusikitisha, idadi ya popo wanaokula matunda inapungua kwa kasi sana hasa kwa sababu ya kukatwa kwa misitu. Katika visiwa vya Pasifiki Kusini, kutoweka kwa popo hao kutaleta matatizo makubwa kwa kuwa mimea fulani katika visiwa hivyo hutegemea popo ili kuchavusha maua. Kwa kweli, kazi ya watunza-bustani hao wanaoruka inapaswa kuthaminiwa sana.

^ fu. 2 Popo aina ya Old World wanaokula matunda hupatikana Afrika, Asia, Australia, na Visiwa fulani vya Pasifiki.