Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mambo Unayopaswa Kujua Kuhusiana na Kuokoa Nishati

Mambo Unayopaswa Kujua Kuhusiana na Kuokoa Nishati

TUNATEGEMEA umeme na mafuta katika shughuli mbalimbali. Tunatumia umeme kupasha joto na kupoza nyumba zetu, na tunahitaji mafuta kwa ajili ya magari yetu. Hata hivyo, wanadamu duniani kote wanakabili changamoto mbalimbali zinazohusiana na nishati.

Kwa mfano, tatizo kubwa ambalo Gary, anayeishi Afrika Kusini anakabili ni “kuongezeka kwa bei ya mafuta.” Jennifer, kutoka Ufilipino, anahangaishwa sana na tatizo la umeme, kwa sababu “umeme hukatika mara kwa mara.” Fernando, anayeishi El Salvador, anasema “anahangaishwa na uharibifu wa mazingira.” Katika maeneo mengi duniani, vyanzo vya nishati vinaharibu sana mazingira.

Huenda ukajiuliza, ‘Ninawezaje kukabiliana na changamoto hizi zinazohusiana na nishati?’

Kila mmoja wetu anaweza kutumia nishati kwa busara. Kuna faida nyingi za kutunza na kutumia nishati kwa uangalifu. Tukitumia nishati kidogo, tutaokoa pesa. Pia, tutakuwa tunatunza mazingira, kwa sababu hatutaongeza uhitaji wa nishati ambao kwa sasa unazidi kuwa mkubwa.

Acheni tuchunguze maeneo matatu ambayo tunaweza kuboresha matumizi yetu ya nishati: nyumbani, kwenye usafiri, na katika shughuli za kila siku.

NYUMBANI

Tumia vifaa vya kupasha na kupoza joto kwa busara. Uchunguzi fulani uliofanywa katika nchi moja ya Ulaya, ulionyesha kwamba kupunguza nyuzi mbili tu kwenye kifaa cha kupasha joto wakati wa msimu wa baridi, kulipunguza matumizi ya umeme kwa kiwango kikubwa sana ndani ya mwaka mzima. Derek, anayeishi Kanada, anakubaliana na hilo. Anasema hivi: “Familia yetu huokoa nishati kwa kuvaa sweta wakati wa msimu wa baridi badala ya kuwasha vipasha joto.”

Kanuni hiyohiyo inaweza kutumika katika maeneo ya joto. Rodolfo, kutoka Ufilipino, hurekebisha kwa makini utendaji wa kiyoyozi chake na hivyo kutumia nishati kidogo. Kwa nini? Anasema, “Tunaokoa pesa na nishati.”

Funga madirisha na milango unapokuwa umewasha kifaa cha kudhibiti joto au baridi ndani ya nyumba. * Tunaweza kupunguza matumizi ya nishati kwa kuzuia hewa ambayo tayari ni yenye baridi au joto isitoke nje. Kwa mfano, kuacha mlango ukiwa wazi wakati wa msimu wa baridi hufanya utumie nishati nyingi zaidi kupasha joto nyumba.

Zaidi ya kufunga milango na madirisha, baadhi ya watu wamepunguza matumizi ya nishati kwa kujenga kuta zao na madirisha kwa njia ya pekee inayozuia hewa iliyo ndani ya nyumba isipotee.

Weka taa zinazotumia nishati kidogo. Jennifer aliyetajwa mwanzoni anasema hivi: “Badala ya kutumia balbu za kawaida tuliamua kutumia balbu mpya zinazotumia nishati kidogo.” Ingawa balbu za aina hiyo zinauzwa kwa bei ya juu, zitaokoa sana nishati kwa muda wote zitakaotumika na hivyo kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.

USAFIRI

Inapowezekana tumia usafiri wa umma. Andrew, anayeishi Uingereza anasema hivi: “Kila inapowezekana mimi hutumia treni au baiskeli kwenda kazini.” Kitabu Energy: What Everyone Needs to Know kinasema kwamba “magari binafsi hutumia nishati angalau mara tatu zaidi kwa kila abiria ukilinganisha na mabasi ya umma au treni.”

Panga vizuri safari zako. Ukipanga mapema, huenda utakuwa na safari chache zaidi na hivyo kupunguza kiasi cha mafuta utakachotumia na wakati huohuo utaokoa muda na pesa.

Jethro, anayeishi Ufilipino, hutenga kiasi hususa cha pesa za mafuta ya gari lake kila mwezi. “Hilo hunifanya nipange safari zangu kwa busara.”

SHUGHULI ZA KILA SIKU

Punguza matumizi ya maji ya moto. Kulingana na utafiti mmoja uliofanywa nchini Australia, “kwa wastani, kiasi cha nishati inayotumiwa kuchemsha maji kwenye nyumba za watu binafsi huchukua asilimia 1.3 ya nishati inayotumiwa katika majiji” nchini humo, sawa na “asilimia 27 ya kiasi cha nishati kinachotumiwa katika shughuli zote za nyumbani.”

Kwa kuwa kiasi kikubwa cha nishati kinahitajika ili kuchemsha maji, kupunguza matumizi ya maji ya moto huokoa nishati. Kwa kufaa, Victor, anayeishi Afrika Kusini, anasema hivi: “Sisi hujitahidi kadiri tunavyoweza kutumia kiasi kidogo cha maji ya moto tunapooga.” Kulingana na mwanasayansi Steven Kenway, “kupunguza matumizi ya maji ya moto kuna faida mara tatu,” kwa sababu “hufanya watu watumie nishati na maji kidogo, hupunguza kiasi cha nishati kinachohitajika, na husaidia familia . . . kuokoa pesa.”

Zima vifaa vinavyotumia nishati. Vifaa hivyo vinatia ndani taa na pia vifaa vya umeme na vya kielektroni, kama vile televisheni na kompyuta. Vifaa vingi bado hutumia nishati hata vinapokuwa vimezimwa. Wataalamu fulani wanapendekeza kuvichomoa kwenye umeme au kuzima kwa kutumia kifaa cha kutawanya umeme chenye swichi na hivyo kuokoa nishati. Fernando, aliyetajwa mwanzoni, anatumia mbinu hiyo, na anasema: “Mimi huzima taa na kuchomoa vifaa vya umeme ninapokuwa sivitumii.”

Ni kweli kwamba hatuwezi kudhibiti gharama za nishati au jinsi ambavyo vyanzo vyake vinaathiri mazingira kwa ujumla, lakini tunaweza kutumia nishati kwa busara. Duniani pote, watu wanabuni njia zinazoweza kuwasaidia kuboresha matumizi yao ya nishati. Bila shaka, jitihada na mipango mingi huhitajika ili kuokoa nishati, lakini hebu fikiria faida zake. Valeria, anayeishi Mexico, anasema, “Ninaokoa pesa, na kutunza mazingira.”

^ fu. 10 Fuata kwa uangalifu maagizo ya watengenezaji ili usipate madhara unapotumia vifaa vya kupasha au kupoza joto. Kwa mfano, vifaa fulani vina maagizo maalum kuhusu kuacha milango na madirisha wazi vinapokuwa vimewashwa, ili visisababishe madhara.