Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 15

Mke wa Lutu Alitazama Nyuma

Mke wa Lutu Alitazama Nyuma

LUTU na jamaa yake walikaa Kanaani pamoja na Ibrahimu. Siku moja Ibrahimu alimwambia Lutu hivi: ‘Hapa hapana nchi ya kufaa wanyama wetu wote. Tafadhali, tutengane. Ukienda huku, na mimi nitakwenda kule.’

Lutu akaitazama nchi. Akaona sehemu ya nchi iliyo nzuri sana yenye maji na majani mazuri mengi ya wanyama wake. Hiyo ilikuwa Wilaya ya Yordani. Basi Lutu alipeleka jamaa yake na wanyama huko. Mwishowe wakakaa katika mji wa Sodoma.

Watu wa Sodoma walikuwa wabaya sana. Lutu alisumbuliwa, maana alikuwa mtu mzuri. Hata Mungu alisumbuliwa. Mwishowe, Mungu alituma malaika wawili wakamwonye Lutu kwamba Mungu ataharibu Sodoma, na Gomora mji wa karibu, maana ni miji mibaya.

Malaika hao wakamwambia Lutu hivi: ‘Fanya haraka! Chukua mke wako na binti zako wawili mwondoke huku!’ Malaika mmoja alisema: ‘Kimbieni mponye uhai wenu! Msitazame nyuma. Kimbieni kwenye mlima msiuawe.’

Lutu na binti zake walitii, wakatoka Sodoma. Lakini mke wa Lutu hakutii. Walipokwisha kutembea mwendo fulani kutoka Sodoma, mke alisimama akatazama nyuma, akawa nguzo ya chumvi. Unaweza kumwona katika picha?

Tunaweza kujifunza somo zuri kwa hayo. Yanatuonyesha kwamba Mungu anaokoa wale wanaomtii, lakini wale wasiomtii watapoteza uhai wao.