Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 44

Rahabu Anaficha Wapelelezi

Rahabu Anaficha Wapelelezi

WANAUME hao wana taabu. Lazima waondoke, ama watauawa. Ni wapelelezi Waisraeli, na anayewasaidia ni Rahabu. Rahabu anakaa katika nyumba hiyo juu ya ukuta wa mji wa Yeriko. Ebu tuone sababu gani wanaume hao wana taabu.

Waisraeli wako tayari kuvuka Mto Yordani waingie Kanaani. Lakini kwanza, Yoshua anatuma wapelelezi wawili. Anawaambia hivi: ‘Nendeni mkaitazame nchi na mji wa Yeriko.’

Wapelelezi hao wanapoingia Yeriko, wanakwenda nyumbani kwa Rahabu. Lakini mtu fulani anamwambia mfalme hivi: ‘Waisraeli wawili waliingia mjini usiku huu ili wapeleleze nchi.’ Anaposikia hivyo, mfalme anatuma watu kwa Rahabu, wakimwambia hivi: ‘Watoe wale wanaume walioingia nyumbani mwako!’ Lakini Rahabu ameficha wapelelezi hao juu ya dari lake. Anasema: ‘Wanaume fulani walikuja kwangu, lakini sijui walikotoka. Waliondoka kulipoanza kuwa usiku, kabla ya kufungwa lango. Mkifanya haraka, mtawakuta!’ Watu hao wanaanza kuwafuata.

Wakiisha kuondoka, Rahabu anapanda haraka juu ya dari. ‘Najua Yehova atawapa ninyi nchi hii,’ anawaambia wapelelezi hao. ‘Tulisikia alivyoikausha Bahari Nyekundu mlipoondoka Misri, na alivyowaua wafalme Sihoni na Ogu. Nimewahurumia ninyi, basi tafadhali mnipe ahadi, ya kwamba mtanihurumia mimi. Mwokoe baba na mama yangu, ndugu na dada zangu.’

Wapelelezi hao wanaahidi kufanya hivyo, lakini inampasa Rahabu atende jambo fulani. ‘Chukua kamba hii nyekundu uifunge katika dirisha,’ wapelelezi wanamwambia, ‘kisha ukusanye watu wako wote wa ukoo ndani ya nyumba yako pamoja nawe. Tutakaporudi sote kuutwaa Yeriko, tutaiona kamba hii katika dirisha lako tusimwue yeyote nyumbani mwako.’ Wapelelezi hao wanaporudi kwa Yoshua, wanamwambia kila jambo lililotokea.