Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hadithi ya 46

Kuta za Yeriko

Kuta za Yeriko

NI NINI kinachoangusha kuta hizo za Yeriko? Ni kama zimepigwa na kombora kubwa. Lakini siku hizo hawakuwa na makombora; wala hawakuwa na bunduki. Ni mwujiza mwingine wa Yehova! Na tujifunze inavyotukia.

Sikiliza Yehova anavyomwambia Yoshua: ‘Wewe pamoja na watu wako wa vita zungukeni mji. Mzunguke mara moja kila siku muda wa siku sita. Mchukue na sanduku la agano. Makuhani saba watangulie na kupiga tarumbeta zao.

‘Siku ya saba mzunguke mji mara saba. Kisha mpige sauti ndefu ya tarumbeta zenu, na kila mtu apige yowe kuu ya vita. Kuta zitaanguka chini kabisa!’

Yoshua na watu wanafanya kama Yehova anavyosema. Wanapozunguka, kila mtu yuko kimya. Hakuna anayesema. Sauti ya tarumbeta na mshindo wa miguu tu ndio unasikika. Bila shaka adui za watu wa Mungu waliogopa huko Yeriko. Unaiona ile kamba nyekundu inayoning’inia katika dirisha? Ni dirisha la nani lile? Ndiyo, Rahabu amefanya alivyoambiwa na wale wapelelezi wawili. Jamaa yake yote imo nyumbani ikitazama pamoja naye.

Mwishowe, siku ya saba, wakiisha kuuzunguka mji mara saba, tarumbeta yalia, watu wa vita wanapiga kelele, na kuta zaanguka. Ndipo Yoshua anasema: ‘Ueni kila mtu mjini. Okoeni tu fedha, dhahabu, shaba na chuma, mvipeleke kwenye hazina ya hema ya Yehova.’

Yoshua anawaambia wale wapelelezi wawili hivi: ‘Ingieni nyumbani kwa Rahabu, mmtoe yeye na jamaa yake yote.’ Rahabu na jamaa yake wanaokolewa, kama wale wapelelezi walivyokuwa wamemwahidi.