Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 86

Wanaume Walioongozwa na Nyota

Wanaume Walioongozwa na Nyota

UNAIONA nyota ile yenye kung’aa ambako mwanamume mmoja anaelekeza kidole? Nyota hiyo ilitokea walipoondoka Yerusalemu. Hao ni watu wa Mashariki, wana elimu ya nyota. Wanaamini nyota hiyo mpya inawaongoza kwa mtu wa maana.

Watu hao walipofika Yerusalemu, waliuliza hivi: ‘Yuko wapi mtoto atakayekuwa mfalme wa Wayahudi?’ “Wayahudi” ni jina jingine la Waisraeli. ‘Tuliiona kwanza nyota ya mtoto tulipokuwa Mashariki,’ watu hao wakasema, ‘tumekuja tumwabudu.’

Herode mfalme wa Yerusalemu, aliposikia hayo alikasirika. Hakutaka mfalme mwingine akae mahali pake. Basi Herode akawaita makuhani wakuu na kuwauliza: ‘Mfalme aliyeahidiwa atazaliwa wapi?’ Wakajibu: ‘Biblia inasema Bethlehemu.’

Herode akawaita watu wa Mashariki, akawaambia: ‘Nendeni mkatafute mtoto huyo. Mkimwona, mnijulishe. Mimi pia nataka kwenda kumwabudu.’ Kumbe Herode alitaka kumwua mtoto huyo!

Ndipo nyota hiyo inatangulia watu hao Bethlehemu, na kusimama mahali alipo mtoto. Watu hao wanapoingia nyumbani, wanamkuta Mariamu na mtoto Yesu. Wanatoa zawadi na kumpa Yesu. Lakini baadaye Yehova anawaonya watu hao katika ndoto wasimrudie Herode. Wanairejea nchi yao kwa njia nyingine.

Herode anapopata habari kwamba watu wa Mashariki wamerudi kwao, anakasirika sana. Anaamuru wavulana wote Bethlehemu kutoka miaka miwili kwenda chini wauawe. Lakini Yehova anamwonya Yusufu mapema katika ndoto, naye Yusufu anaondoka pamoja na jamaa yake kwenda Misri. Baadaye, Yusufu anapopata habari kwamba Herode amekufa, anachukua Mariamu na Yesu warudi kwao Nazareti. Yesu anakua huko.

Unadhani ni nani aliyefanya nyota mpya hiyo ing’ae? Kumbuka, baada ya kuiona nyota hiyo watu hao walikwenda Yerusalemu. Shetani Ibilisi alitaka kuua Mwana wa Mungu, naye alijua Mfalme Herode wa Yerusalemu angejaribu kumwua. Basi, bila shaka ni Shetani aliyefanya nyota hiyo ing’ae.