Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 88

Yohana Anambatiza Yesu

Yohana Anambatiza Yesu

MWONE njiwa akishuka juu ya kichwa cha mtu huyu. Huyu ni Yesu. Sasa amekuwa na miaka karibu 30. Na yule pamoja naye ni Yohana. Tumekwisha kujifunza habari fulani juu yake. Wakumbuka wakati Mariamu alipomtembelea Elisabeti, na kitoto tumboni mwa Elisabeti kikaruka kwa furaha? Huyo alikuwa Yohana. Lakini Yohana na Yesu wanafanya nini sasa?

Yohana amemtumbukiza sasa hivi Yesu katika maji ya Mto Yordani. Ndivyo mtu anavyobatizwa. Kwanza, anatumbukizwa ndani ya maji, kisha anainuliwa tena. Kwa sababu Yohana anafanyia watu hivyo, anaitwa Yohana Mbatizaji. Lakini kwa nini Yohana amembatiza Yesu?

Yohana alifanya hivyo kwa sababu Yesu alikuja kumwomba Yohana ambatize. Yohana anabatiza watu wanaotaka kuonyesha kwamba wanatubu mabaya waliyofanya. Lakini je! Yesu alipata kufanya ubaya wa kusikitikia? Hapana, kwa sababu yeye ni Mwana wa Mungu aliyetoka mbinguni. Alimwomba Yohana ambatize kwa sababu tofauti. Na tuchunguze sababu hiyo.

Kabla Yesu hajamfikia Yohana, alikuwa seremala. Seremala ni mtu anayetengeneza vitu vya mbao, kama meza na viti. Yusufu mume wa Mariamu alikuwa seremala, naye akamfundisha Yesu kuwa seremala. Amempa kazi ya pekee afanye, na wakati umefika Yesu aanze kuifanya. Basi ili aonyeshe kwamba amekuja kufanya mapenzi ya Baba yake, Yesu anamwomba Yohana ambatize. Je! Mungu anafurahia hilo?

Ndiyo, kwa sababu, baada ya Yesu kutoka katika maji, sauti kutoka mbinguni inasema: ‘Huyu ni Mwanangu, ninayefurahia.’ Pia, inaonekana kama mbingu zinafunguka na njiwa huyu anashuka juu ya Yesu. Lakini si njiwa halisi. Ni roho takatifu ya Mungu.

Sasa Yesu ana mambo mengi ya kufikiria, basi anakwenda zake mahali pa upweke kwa siku 40. Shetani anamfikia huko. Mara tatu Shetani anajaribu kumfanya Yesu avunje sheria za Mungu. Lakini Yesu anakataa.

Baada ya hayo, Yesu anarudi na kukuta wanaume wanaokuwa wafuasi wake wa kwanza, au wanafunzi. Majina ya wachache wao ni Andrea, Petro (pia aitwa Simoni), Filipo na Nathanaeli (pia aitwa Bartholomayo). Yesu na wanafunzi hao wapya wanaenda kwenye wilaya ya Galilaya. Katika Galilaya wanafika Kana, mji wa nyumbani kwake Nathanaeli. Yesu anahudhuria karamu kubwa ya arusi, na kufanya mwujiza wake wa kwanza huko. Unajua? Anageuza maji kuwa divai.