Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 93

Yesu Analisha Watu Wengi Chakula

Yesu Analisha Watu Wengi Chakula

JAMBO baya sana limetokea. Yohana Mbatizaji ameuawa. Herodia, mke wa mfalme, hakumpenda. Alipanga ili mfalme akate kichwa cha Yohana.

Yesu anaposikia hivyo, anahuzunika sana. Aenda peke yake porini. Lakini watu wanamfuata. Yesu anapoona watu wengi, anawahurumia. Basi anawaambia habari za ufalme wa Mungu, na kuponya wagonjwa wao.

Jioni hiyo wanafunzi wake wanamwendea na kusema: ‘Kumekwisha kuwa jioni, na hapa ni porini. Waruhusu watu waende zao wakajinunulie chakula katika vijiji vya karibu.’

‘Haiwapasi kuondoka,’ Yesu ajibu. ‘Ninyi wapeni chakula.’ Akimgeukia Filipo, Yesu auliza: ‘Twaweza kununua wapi chakula cha kufaa watu wote hawa?’

‘Itapoteza fedha nyingi sana kununua chakula cha kumfaa kila mtu,’ Filipo ajibu. Andrea asema: ‘Mtoto huyu, anayechukua chakula chetu, ana mikate mitano na samaki wawili. Lakini haitawatosha watu wote hawa.’

‘Waambieni watu wakae penye majani,’ Yesu asema. Kisha anamshukuru Mungu kwa chakula, na kuanza kukivunja-vunja. Halafu, wanafunzi wanawapa watu wote mkate na samaki. Kuna wanaume 5,000, na maelfu mengi zaidi ya wanawake na watoto. Wote wanakula na kushiba. Wanafunzi wanapokusanya mabaki, vikapu 12 vinajaa!

Sasa Yesu anawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wavuke Bahari ya Galilaya. Usiku huo kwatokea upepo mkubwa, na mawimbi yanapeperusha mashua uku na huku. Wanafunzi waogopa sana. Halafu, usiku wa manane, wanamwona mtu akitembea juu ya maji akiwaelekea. Wanapiga yowe kwa woga, kwa sababu hawajui wanachoona.

‘Msiogope,’ Yesu anasema. ‘Ni mimi!’ Hawasadiki. Petro asema: ‘Ikiwa kweli ni wewe Bwana, niambie nitembee juu ya maji nije kwako.’ Yesu anajibu: ‘Njoo!’ Petro anatoka na kutembea juu ya maji! Halafu anaogopa na kuzama, lakini Yesu anamwokoa.

Baadaye, Yesu analisha tena maelfu ya watu mikate saba na samaki wachache. Tena wote wanashiba. Yesu analisha watu kiajabu, sivyo? Atakapokuwa mfalme aliyewekwa na Mungu hatutakosa kitu!