Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 100

Yesu Katika Bustani

Yesu Katika Bustani

BAADA ya kutoka katika chumba cha juu, Yesu na mitume wake wanaenda kwenye bustani ya Geth·semane. Walikuwa wamekwenda huko mara nyingi. Sasa Yesu anawaambia wawe macho na kusali. Kisha aenda mbali kidogo, na kuinamisha uso ili asali.

Baadaye Yesu arudi mahali walipo mitume wake. Unafikiri wanafanya nini? Wamelala usingizi! Yesu anawaambia mara tatu wawe macho, lakini kila anaporudi anawakuta wamelala usingizi. ‘Mwaweza kulalaje wakati kama huu?’ Yesu anawaambia mara ya mwisho anaporudi. ‘Umenifikia wakati wa kupewa kwa adui zangu.’

Wakati uo huo kelele ya watu wengi inasikiwa. Tazama! Watu wanakuja wakiwa na panga na marungu! Nao wana mienge ya kuwapa nuru. Wanapokaribia zaidi, mtu mmoja anatoka katika kundi la watu na kumfikia Yesu. Anambusu, kama unavyoona hapa. Mtu huyo ni Yuda Iskariote! Kwa nini ambusu Yesu?

Yesu anauliza: ‘Yuda, unanishtaki kwa kunibusu?’ Kumbusu huko ni ishara. Kunawajulisha watu walio pamoja na Yuda kwamba huyu ni Yesu, ndiye mtu wanayetaka. Basi adui za Yesu wanamkamata. Lakini Petro hataki wamkamate Yesu bila kupigana. Anavuta upanga aliokuwa amechukua na kumpiga mtu aliye karibu naye. Upanga wakosa kichwa cha mtu huyo, unakata sikio lake la kuume. Lakini Yesu anagusa sikio la mtu huyo na kuliponya.

Yesu anamwambia Petro: ‘Rudisha upanga wako mahali pake. Hujui naweza kumwomba Baba yangu maelfu ya malaika waniokoe?’ Ndiyo, anaweza! Lakini Yesu hamwombi Mungu atume malaika kwa sababu anajua umefika wakati ili adui zake wamkamate. Basi anakubali wamkamate. Na tuone yanayompata Yesu sasa.