Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 103

Ndani ya Chumba Kilichofungwa

Ndani ya Chumba Kilichofungwa

BAADA ya Petro na Yohana kuondoka kwenye kaburi la Yesu, Mariamu anabaki hapo peke yake. Aanza kulia. Ndipo anainama na kuchungulia kaburi, kama ulivyoona picha ya mwisho. Anawaona malaika humo! Wanamwuliza: ‘Kwa nini unalia?’

Mariamu ajibu: ‘Wamemchukua Bwana wangu, sijui walikomweka.’ Ndipo Mariamu ageuka na kuona mwanamume. Anamwuliza: ‘Unamtafuta nani?’

Mariamu anadhani mwanamume huyo anatunza bustani, na labda amechukua mwili wa Yesu. Basi anamwambia hivi: ‘Ikiwa umemchukua, niambie ulipomweka.’ Kumbe huyo ndiye Yesu. Amevaa mwili ambao Mariamu hatambui. Lakini anapomwita jina lake, Mariamu anajua ni Yesu. Anakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi hivi: ‘Nimemwona Bwana!’

Baadaye siku hiyo, wanafunzi wawili wanapotembea kwenye kijiji cha Emau, mtu fulani anajiunga nao. Wanapoendelea njiani, mtu huyo anawaeleza mambo mengi ya kufurahisha kutoka Biblia. Mwishowe, wanapoanza kula, wanafunzi hao wanatambua kwamba mtu huyo ni Yesu. Kisha Yesu anaacha kuonekana, na upesi wanafunzi hao wawili wanarudi Yerusalemu kwenda kuwaambia mitume habari zake.

Hayo yanapoendelea, Yesu anajionyesha tena kwa Petro. Wengine wanapopata habari hizo wanafurahi. Ndipo wanafunzi hao wawili wanakwenda Yerusalemu na kuwakuta mitume. Wanawaambia namna Yesu alivyowatokea pia njiani. Wakati wanaposema hayo, unajua ajabu inayotokea?

Ebu itazame picha. Yesu atokea mle mle chumbani, ijapo mlango umefungwa kwa kufuli. Wanafunzi wanafurahi! Je! hiyo si siku ya furaha? Unaweza kuhesabu mara ambazo Yesu sasa ameonekana kwa wafuasi wake? Unahesabu mara tano?

Mtume Tomaso (Tomasi) hayuko nao wakati Yesu anapoonekana. Basi wanafunzi wanamwambia: ‘Tumemwona Bwana!’ Lakini Tomaso hawezi kusadiki mpaka ajionee mwenyewe Yesu. Basi, siku nane zikiisha kupita wanafunzi wanakusanyika tena katika chumba kilichofungwa, wakati huu Tomaso yuko nao. Mara moja, Yesu atokea mle mle chumbani. Tomaso anasadiki sasa.