Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 109

Petro Anamtembelea Kornelio

Petro Anamtembelea Kornelio

YULE ni mtume Petro anayesimama pale, na wale nyuma yake ni rafiki zake. Lakini kwa nini mtu huyu anamsujudia Petro. Je! yafaa afanye hivyo? Unamjua?

Ni Kornelio. Ni mkuu wa jeshi la Roma. Kornelio hamjui Petro, lakini aliambiwa amkaribishe nyumbani kwake. Na tuone ilivyokuwa.

Wafuasi wa kwanza wa Yesu walikuwa Wayahudi. Kornelio si Myahudi. Lakini anampenda Mungu, anamwomba, na anawafanyia watu mambo mengi mema. Basi, alasiri moja malaika akamtokea na kumwambia: ‘Mungu anapendezwa nawe, naye atajibu sala zako. Watume watu wakamchukue mtu fulani jina lake Petro. Anakaa katika Yopa nyumbani kwa Simoni, karibu na bahari.’

Basi, mara hiyo Kornelio anatuma watu wakamtafute Petro. Siku inayofuata, watu hao wanapokaribia Yopa, Petro yuko juu ya dari ya nyumba ya Simoni. Hapo ndipo Mungu anamfanya Petro adhani ameona nguo kubwa ikitoka mbinguni. Katika nguo hiyo mna namna zote za wanyama. Sheria ya Mungu ilikataza kula wanyama hao. Lakini sauti yasema: ‘Amka, Petro. Ua, ule.’

‘Sivyo!’ Petro anajibu. ‘Sijapata kula kitu kichafu.’ Lakini sauti hiyo yamwambia Petro hivi: ‘Acha kuita kichafu kitu ambacho sasa Mungu anasema ni safi.’ Inakuwa hivyo mara tatu. Wakati Petro angali akifikiria maana yake, watu waliotumwa na Kornelio wanafika nyumbani wakimtaka Petro.

Petro anashuka chini na kusema: ‘Ni mimi mnayetafuta. Mmekuja kwa sababu gani?’ Watu hao wanapoeleza kwamba malaika alimwambia Kornelio akaribishe Petro nyumbani kwake, Petro anakubali kwenda nao. Kesho yake Petro na rafiki zake wanaondoka wakamtembelee Kornelio huko Kaisaria.

Kornelio amekusanya watu wake wa ukoo na rafiki za karibu. Petro anapofika Kornelio amlaki. Anapiga magoti na kuinamia miguu ya Petro, kama unavyoona hapa. Lakini Petro amwambia: ‘Amka; mimi pia ni mwanadamu.’ Ndiyo, Biblia inaonyesha haifai kusujudu na kuabudu mwanadamu. Imetupasa tumwabudu Yehova peke yake.

Sasa Petro anawahubiri hao waliokusanyika. ‘Naona kwamba Mungu anakubali watu wote wanaotaka kumtumikia,’ Petro anasema. Na wakati angali akisema, Mungu anapeleka roho yake takatifu, na watu hao wanaanza kusema lugha mbalimbali. Hivyo wanafunzi Wayahudi waliokuja pamoja na Petro, wanastaajabu maana walidhani Mungu anapendelea Wayahudi tu. Wanajua kwamba Mungu haoni watu wa taifa fulani kuwa bora kuliko watu wa taifa jingine. Je! hilo si jambo linalofaa sote tulikumbuke?