Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sura ya 5

Nguvu za Kuumba​—“Aliyezifanya Mbingu na Nchi”

Nguvu za Kuumba​—“Aliyezifanya Mbingu na Nchi”

1, 2. Jua linaonyeshaje nguvu za Yehova za kuumba?

JE, UMEWAHI kusimama karibu na moto usiku wenye baridi? Labda ulinyoosha mikono yako umbali ufaao kutoka kwenye miali ya moto ili ufurahie joto lake. Uliposonga karibu zaidi, ulishindwa kustahimili joto hilo kali. Uliporudi nyuma zaidi, hewa baridi ya usiku ilikulemea, nawe ukaanza kutetemeka.

2 Kuna “moto” unaopasha joto miili yetu wakati wa mchana. “Moto” huo uko umbali wa kilometa milioni 150! * Ni wazi kwamba jua lina nguvu nyingi kiasi cha kwamba unaweza kuhisi joto lake kutoka umbali huo! Lakini, dunia inazunguka tanuru hiyo kubwa yenye joto kali la nyuklia kwa umbali barabara. Ikiwa dunia ingekaribia jua, maji yote duniani yangekuwa mvuke; na ikiwa dunia ingesonga mbali zaidi, maji yote yangekuwa barafu. Joto au baridi kali ingeangamiza kila kiumbe duniani. Nuru ya jua ni muhimu sana kwa uhai duniani, ni safi na ina manufaa tele, na inapendeza.—Mhubiri 11:7.

Yehova ‘aliufanya mwanga na jua’

3. Jua huthibitisha ukweli upi muhimu?

3 Hata hivyo, watu wengi wanaona jua kuwa kitu cha kawaida tu, ingawa uhai wao unalitegemea. Hivyo basi, hawajifunzi somo lolote kutokana na jua. Biblia inasema hivi kumhusu Yehova: “Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.” (Zaburi 74:16) Naam, jua humletea sifa Yehova, “Aliyezifanya mbingu na nchi.” (Zaburi 19:1; 146:6) Jua ni mojawapo ya sayari chungu nzima zilizo angani ambazo zinatufundisha kuhusu nguvu nyingi za Yehova za kuumba. Hebu tuchunguze baadhi ya sayari hizo kwa undani zaidi halafu tuchunguze dunia na viumbe mbalimbali waliomo.

“Inueni Macho Yenu Juu, Mkaone”

4, 5. Jua lina nguvu nyingi kadiri gani, na ni kubwa kadiri gani, lakini likoje linapolinganishwa na nyota nyinginezo?

4 Huenda unajua kwamba jua letu ni nyota. Jua huonekana kubwa kuliko nyota tunazoona usiku kwa sababu liko karibu sana kuliko nyota hizo. Lina nguvu nyingi kadiri gani? Kipimo cha joto kwenye kiini cha jua ni nyuzi Selsiasi 15,000,000 hivi. Kama ungeweza kuchukua kipande cha kiini cha jua kinachotoshana na kichwa cha pini ndogo na kukiweka duniani, ungeteketea hata ukiwa umbali wa kilometa 140 kutoka kwenye chanzo hicho kidogo sana cha joto! Kila sekunde, jua hutoa nishati inayolingana na mlipuko wa mamia ya mamilioni ya mabomu ya nyuklia.

5 Jua ni kubwa sana hivi kwamba zaidi ya dunia 1,300,000 zinaweza kutoshea ndani yake. Je, jua ni nyota kubwa kupindukia? La, wataalamu wa nyota husema kwamba jua ni nyota ndogo sana yenye mwangaza hafifu. Mtume Paulo aliandika kwamba “nyota hutofautiana na nyota kwa utukufu.” (1 Wakorintho 15:41) Paulo hakuweza kuelewa kabisa maneno hayo ya Mungu. Kuna nyota moja kubwa hivi kwamba ikiwa ingewekwa mahali lilipo jua, basi ingefika ilipo dunia yetu. Endapo nyota nyingine ambayo ni kubwa sana ingewekwa lilipo jua, ingefikia sayari ya Zohali—japo sayari hiyo iko mbali sana na dunia hivi kwamba roketi ya angani ilisafiri kwa muda wa miaka minne ili kufika huko. Mwendo wake ulizidi mara 40 mwendo wa risasi inayofyatuliwa na bunduki yenye nguvu!

6. Biblia inaonyeshaje kwamba idadi ya nyota ni kubwa sana wanadamu wasiweze kuhesabu?

6 Lakini idadi ya nyota inastaajabisha zaidi ya ukubwa wake. Kwa kweli, Biblia inasema kwamba nyota haziwezi kuhesabiwa, kama vile “mchanga wa bahari” usivyoweza kuhesabiwa. (Yeremia 33:22) Maneno hayo yanadokeza kwamba kuna nyota nyingi sana ambazo hatuwezi kuona pasipo vifaa maalumu. Endapo mwandikaji wa Biblia, kama Yeremia, angetazama angani wakati wa usiku na kujaribu kuhesabu nyota zionekanazo, angefaulu kuhesabu nyota zipatazo 3,000 hivi. Wanadamu huweza kuona idadi hiyo tu ya nyota katika anga jangavu la usiku bila kutumia vifaa maalumu. Idadi hiyo yaweza kulinganishwa na idadi ya chembe za mchanga zinazoweza kujaza kiganja kimoja tu cha mkono. Hata hivyo, idadi halisi ya nyota haijulikani, ni nyingi kama mchanga wa bahari. Ni nani awezaye kuhesabu idadi kubwa hivyo? *

“Aziita zote kwa majina”

7. (a) Kundi letu la Kilimia lina nyota ngapi, na hiyo ni idadi kubwa kadiri gani? (b) Kushindwa kwa wataalamu wa nyota kuhesabu makundi ya nyota kwaonyesha nini, na hilo latufundisha nini kuhusu nguvu za Yehova za kuumba?

7 Andiko la Isaya 40:26 linajibu hivi: “Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina.” Zaburi 147:4 yasema: “Huihesabu idadi ya nyota.” “Idadi ya nyota” ni ngapi? Hilo si swali rahisi. Wataalamu wa nyota wanakadiria kwamba kuna zaidi ya nyota bilioni 100 katika kundi letu la nyota la Kilimia peke yake. Lakini kuna makundi mengine mengi mbali na kundi letu, ambayo yana nyota nyingi zaidi. Kuna makundi mangapi? Baadhi ya wataalamu wa nyota wamekadiria kwamba kuna makundi bilioni 50. Wengine wamekadiria kwamba kuna makundi yapatayo bilioni 125. Kwa hiyo, mwanadamu hawezi hata kujua idadi ya makundi ya nyota, sembuse kujua idadi kamili ya mabilioni ya nyota zilizomo. Lakini, Yehova anajua idadi yake. Isitoshe, yeye huipa kila nyota jina lake!

8. (a) Kundi la Kilimia ni kubwa kadiri gani? (b) Yehova anapangaje mizunguko ya sayari na nyota mbinguni?

8 Tunakuwa na kicho zaidi kwa Mungu tunapotafakari juu ya ukubwa wa kundi moja la nyota. Kundi la Kilimia limekadiriwa kuwa na upana wa kipimo cha miaka 100,000 cha mwendo wa mwanga. Hebu wazia mwali wa mwanga unaosafiri kwa mwendo wa kasi sana wa kilometa 300,000 kwa sekunde. Ingechukua mwali huo miaka 100,000 kuvuka kundi letu la nyota! * Na makundi fulani ni makubwa zaidi ya Kilimia. Biblia inasema kwamba Yehova ‘amezitandika mbingu’ hizi pana kana kwamba ni pazia tu. (Zaburi 104:2) Pia anapanga mizunguko ya sayari na nyota alizoumba. Kila kitu kinazunguka kupatana na sheria za asili ambazo Mungu ametunga na kutekeleza, kuanzia chembe ndogo sana ya vumbi lililo angani hadi kundi kubwa zaidi la nyota. (Ayubu 38:31-33) Ndiyo sababu, wanasayansi wamelinganisha mizunguko barabara ya sayari na nyota na miendo hususa ya wachezaji-dansi wenye utaratibu wa hali ya juu! Basi fikiria Muumba wa vitu hivyo vyote. Je, hustaajabishwi na Mungu huyo mwenye nguvu nyingi hivyo za kuumba?

“Ameiumba Dunia kwa Uweza Wake”

9, 10. Nguvu za Yehova zinadhihirishwaje na mahali ambapo mfumo wetu wa jua, Jupita, dunia, na mwezi ulipo?

9 Nguvu za Yehova za kuumba zinadhihirishwa katika makao yetu, dunia. Ameiweka dunia mahali pafaapo katika ulimwengu huu mkubwa. Wanasayansi fulani wanaamini kwamba mazingira ya makundi mengi ya nyota huenda yasifae sayari yenye uhai kama sayari yetu. Ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya kundi letu la nyota la Kilimia haikubuniwa ili iwe makao ya viumbe. Sehemu ya katikati ya kundi hilo imejaa nyota. Mnururisho ni mkali mno, na mara nyingi nyota huponea chupuchupu kugongana. Kingo za kundi hilo la nyota hazina vitu vingi ambavyo ni muhimu kwa uhai. Mfumo wetu wa jua uko mahali pafaapo kabisa.

10 Dunia hulindwa na sayari moja kubwa iliyo mbali sana—sayari ya Jupita. Sayari hiyo ya Jupita yenye ukubwa ambao ni mara 1,000 zaidi ya ukubwa wa Dunia, ina nguvu nyingi za uvutano. Matokeo ni nini? Inafyonza au kugeuza mwelekeo wa vitu vinavyosonga kasi angani. Wanasayansi wanasema kwamba kama Jupita haingekuwapo, vitu vikubwa vinavyosonga kasi angani vingegonga dunia na kuiathiri mara 10,000 zaidi ya ilivyo sasa. Dunia yetu hunufaishwa pia na sayari nyingine ya pekee iliyo karibu zaidi—mwezi. Licha ya kuwa sayari maridadi sana na “taa ya usiku,” mwezi hudumisha mwinamo uleule wa dunia. Mwinamo huo huwezesha dunia kuwa na majira thabiti na yasiyobadilika—jambo jingine muhimu kwa uhai duniani.

11. Angahewa ya dunia imebuniwaje ili kulinda dunia?

11 Nguvu za Yehova za kuumba zinadhihirishwa na kila kitu duniani. Fikiria angahewa ambayo inalinda dunia. Jua hutoa miale inayonufaisha mwili na miale hatari. Miale hatari inapofika kwenye angahewa ya juu ya dunia, inabadili oksijeni katika hewa kuwa hewa ya ozoni. Tabaka la hewa ya ozoni linalofanyizwa, linafyonza sehemu kubwa ya miale hiyo. Kwa kweli, sayari yetu imebuniwa ikiwa na kifuniko kinachoilinda!

12. Mzunguko wa maji wa angahewa unathibitishaje nguvu za Yehova za kuumba?

12 Angahewa yetu, ambayo ni mchanganyiko tata wa gesi zifaazo zinazotegemeza viumbe wanaoishi karibu au juu ya uso wa dunia inahusisha mambo mengine mengi. Mzunguko wa maji ni mojawapo ya maajabu ya angahewa. Kila mwaka jua huvukiza zaidi ya kilometa 400,000 za kipimo cha ujazo wa maji kutoka kwa bahari zote duniani. Maji hayo hufanyiza mawingu, ambayo husambazwa kotekote na pepo za angahewa. Maji hayo ambayo yamechujwa na kusafishwa, hunyesha yakiwa mvua, theluji, na barafu, na hivyo kuongeza hifadhi za maji duniani. Ni kama vile Mhubiri 1:7 inavyosema: “Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena.” Yehova tu ndiye aliye na uwezo wa kuanzisha mzunguko huo.

13. Mimea na udongo wa dunia vinadhihirishaje nguvu za Muumba?

13 Kila kitu kilicho hai kinatudhihirishia nguvu za Muumba. Miti mikubwa mno aina ya sequoia ambayo ni mirefu kushinda jengo lenye orofa 30, na mimea mingi midogo mno ya baharini inayotokeza kiasi kikubwa cha hewa tunayopumua, inadhihirisha nguvu za Yehova za kuumba. Hata udongo una mimea na wanyama wengi walio hai—minyoo, kuvu, na vijiumbe vidogo sana, ambavyo hushirikiana kwa njia za pekee sana ili kuchangia ukuzi wa mimea. Ndiyo sababu Biblia inasema kwamba udongo una nguvu.—Mwanzo 4:12ZSB.

14. Atomu ndogo sana ina nguvu zipi zilizofichika?

14 Hapana shaka kwamba Yehova ndiye ‘Aliyeiumba dunia kwa uweza wake.’ (Yeremia 10:12) Nguvu za Yehova zinadhihirishwa pia na vitu vidogo sana alivyoumba. Kwa mfano, atomu milioni moja zikipangwa karibu-karibu haziwezi kufikia unene wa unywele wa mwanadamu. Na hata kama atomu ingerefushwa kufikia kimo cha jengo lenye orofa 14, kiini chake kingelingana na chembe moja tu ya chumvi iliyo kwenye orofa ya 7 ya jengo hilo. Lakini kiini hicho kidogo sana ndicho chanzo cha nguvu za kutisha za mlipuko wa kombora la nyuklia!

“Kila Mwenye Pumzi”

15. Yehova alimfunza Ayubu somo gani alipozungumzia wanyama mbalimbali wa mwitu?

15 Wanyama chungu nzima walio duniani wanathibitisha pia waziwazi nguvu za Yehova za kuumba. Zaburi 148 inaorodhesha baadhi ya viumbe wanaomsifu Yehova, na mstari wa 10 unataja “hayawani, na wanyama wafugwao.” Ili kuonyesha kwa nini mwanadamu anapaswa kuwa na kicho kumwelekea Muumba, pindi moja Yehova alizungumza na Ayubu kuhusu wanyama kama vile simba, punda-milia, nyati, kiboko, na mamba. Yehova alitaka kufunza somo gani? Ikiwa mwanadamu hupigwa na butwaa kwa sababu ya viumbe hao wakubwa, wenye kutisha, na wasioweza kufugwa, je, hapaswi kumhofu hata zaidi Muumba wa viumbe hao?—Ayubu, sura ya 38-41.

16. Ni nini kinachokuvutia kuhusu baadhi ya ndege ambao Yehova ameumba?

16 Andiko la Zaburi 148:10 linataja pia “ndege wenye mbawa.” Hebu fikiria jamii nyingi zilizopo! Yehova alimwambia Ayubu kuhusu mbuni ambaye “humdharau farasi na mwenye kumpanda.” Ijapokuwa ndege huyu mwenye kimo cha meta 2.5 hawezi kuruka, anaweza kukimbia kwa mwendo wa kilometa 65 kwa saa, na anafikia umbali wa meta 4.5 anapopiga hatua moja tu! (Ayubu 39:13, 18) Kwa upande mwingine, ndege aitwaye alibatrosi huruka juu ya bahari muda mwingi wa maisha yake. Kwa kawaida ndege huyo hunyiririka tu hewani, na kipimo cha mabawa yake ni meta 3 kutoka ncha hadi ncha. Anaweza kupaa angani kwa saa nyingi sana bila kupigapiga mabawa yake. Kwa upande mwingine, ndege aina ya bee hummingbird mwenye urefu wa sentimeta 5 tu ndiye ndege mdogo zaidi ulimwenguni. Anaweza kupigapiga mabawa yake mara 80 kwa sekunde! Ndege hao wanaomeremeta kama vito vidogo vyenye mabawa, wanaweza kuelea hewani kama helikopta na hata kupaa kinyumenyume.

17. Nyangumi wa rangi ya buluu-kijivu ni mkubwa kadiri gani, na tunapaswa kufikia mkataa gani baada ya kuchunguza wanyama walioumbwa na Yehova?

17 Andiko la Zaburi 148:7 linasema kwamba hata “nyangumi” wanamsifu Yehova. Mfikirie kiumbe anayedhaniwa na wengi kuwa kiumbe mkubwa zaidi aliyewahi kuishi duniani, nyangumi mwenye rangi ya buluu-kijivu. Mnyama huyo mkubwa sana anayeishi baharini anaweza kuwa na urefu wa meta 30 au zaidi. Anaweza kuwa na uzito wa ndovu 30 wakomavu. Ulimi wake peke yake una uzito wa ndovu mmoja. Moyo wake unalingana na gari ndogo. Moyo huo mkubwa hupigapiga mara 9 tu kwa dakika—tofauti na moyo wa ndege aina ya hummingbird, ambao unaweza kupigapiga mara 1,200 hivi kwa dakika. Angalau mshipa mmoja wa nyangumi huyo ni mkubwa sana hivi kwamba mtoto mdogo anaweza kutambaa ndani yake. Bila shaka mioyo yetu hutuchochea kutangaza himizo la mstari wa mwisho wa kitabu cha Zaburi: “Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA.”—Zaburi 150:6.

Kujifunza Kutokana na Nguvu za Yehova za Kuumba

18, 19. Vitu ambavyo Yehova ameumba duniani ni vingi kadiri gani, na uumbaji hutufundisha nini kuhusu enzi yake kuu?

18 Twajifunza nini kutokana na jinsi Yehova anavyotumia nguvu zake za kuumba? Tunatiwa kicho tunapotambua kwamba vitu vilivyoumbwa ni vingi sana. Mtunga-zaburi mmoja alisema hivi kwa mshangao: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! . . . Dunia imejaa mali zako.” (Zaburi 104:24) Ni kweli kama nini! Wanabiolojia wamegundua jamii zaidi ya milioni moja za vitu hai duniani; lakini hawajui kama kuna jamii milioni 10, milioni 30, au zaidi. Wakati mwingine msanii anaweza kushindwa kubuni jambo jipya. Lakini ubuni wa Yehova—uwezo wake wa kubuni na kuumba vitu mbalimbali vipya—bila shaka hauna kikomo.

19 Tunajifunza kuhusu enzi kuu ya Yehova kutokana na jinsi anavyotumia nguvu zake za kuumba. Neno “Muumba” linamtofautisha Yehova na vitu vyote ulimwenguni, kwani vitu vyote “viliumbwa.” Hata Mwana mzaliwa-pekee wa Yehova, ambaye alikuwa “stadi wa kazi” wakati wa uumbaji, haitwi kamwe Muumba au Muumba-msaidizi katika Biblia. (Mithali 8:30; Mathayo 19:4) Badala yake, yeye ni “mzaliwa wa kwanza wa uumbaji wote.” (Wakolosai 1:15) Cheo cha Yehova akiwa Muumba humpa haki kamili ya kuwa mwenye enzi kuu pekee wa ulimwengu wote.—Waroma 1:20; Ufunuo 4:11.

20. Yehova amepumzikaje tangu alipomaliza kuumba vitu duniani?

20 Je, Yehova ameacha kutumia nguvu zake za kuumba? Ni kweli kwamba Biblia inasema kuwa Yehova alipomaliza kazi yake ya kuumba siku ya sita ya uumbaji, ‘siku ya saba Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote aliyoifanya.’ (Mwanzo 2:2, BHN) Mtume Paulo alionyesha kwamba hiyo “siku” ya saba ina urefu wa maelfu ya miaka, kwa kuwa ilikuwa ikiendelea katika siku zake. (Waebrania 4:3-6) Lakini je, neno ‘alipumzika’ lamaanisha kwamba Yehova ameacha kufanya kazi kabisa? La, Yehova hufanya kazi daima. (Zaburi 92:4; Yohana 5:17) Basi, bila shaka pumziko lake linarejezea tu kuacha kwake kufanya kazi ya kuumba vitu duniani. Hata hivyo, kazi yake ya kutimiza makusudi yake imeendelea bila kukatishwa. Kazi hiyo imetia ndani kupulizia Maandiko Matakatifu. Kazi yake imetia ndani pia kutokeza “kiumbe kipya.” Habari hiyo itazungumziwa katika Sura ya 19.—2 Wakorintho 5:17.

21. Nguvu za Yehova za kuumba zitakuwa na matokeo gani kwa wanadamu waaminifu kwa umilele wote?

21 Siku ya Yehova ya pumziko itakapofikia mwisho hatimaye, ndipo atakapoweza kutangaza kazi yake yote duniani kuwa ‘njema sana,’ kama alivyofanya mwishoni mwa siku sita za uumbaji. (Mwanzo 1:31) Bado tunangoja kuona jinsi atakavyoamua kutumia nguvu zake za kuumba zisizo na mipaka baadaye. Kwa vyovyote vile, tunaweza kuwa na hakika kwamba tutaendelea kustaajabishwa na jinsi Yehova anavyotumia nguvu zake za kuumba. Kwa umilele wote, tutajifunza mengi zaidi kumhusu Yehova kupitia uumbaji wake. (Mhubiri 3:11) Kadiri tunavyojifunza mengi kumhusu, ndivyo tutakavyokuwa na kicho zaidi—na ndivyo tutakavyomkaribia zaidi Muumba wetu Mtukufu.

^ fu. 2 Ili kufahamu vyema umbali huo mkubwa, fikiria hili: Ukisafiri umbali huo kwa gari—linaloenda kwa mwendo wa kilometa 160 kwa saa, saa 24 kwa siku—ungehitaji kusafiri kwa muda wa zaidi ya miaka 100!

^ fu. 6 Watu fulani hufikiri kwamba watu walioishi katika nyakati za Biblia walitumia darubini fulani ya kienyeji. Wanatoa sababu kwamba watu walioishi nyakati hizo hawangeweza kujua kwamba idadi ya nyota ni kubwa sana wanadamu wasiweze kuhesabu. Makisio hayo yasiyo na msingi hayamheshimu wala kumtambua Yehova, Mtungaji wa Biblia.—2 Timotheo 3:16.

^ fu. 8 Fikiria muda ambao ungehitaji kutumia kuhesabu nyota bilioni 100 tu. Kama ungeweza kuhesabu nyota moja kila sekunde—kwa muda wa saa 24 kwa siku—ingekuchukua miaka 3,171!