Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 33

Yesu Anaweza Kutulinda

Yesu Anaweza Kutulinda

Wewe unamwonaje Yesu —kama Mfalme mwenye nguvu au kama mtoto asiye na uwezo?

YESU alipokuwa mtu mzima na kujua jinsi alivyolindwa alipokuwa mtoto, unafikiri alisali kwa Yehova na kumshukuru?— Unafikiri huenda Yesu aliwaambia nini Maria na Yosefu baadaye alipojua kwamba waliokoa uhai wake kwa kumpeleka Misri?—

Yesu si mtoto tena kamwe. Hata haishi duniani kama alivyoishi hapo zamani. Lakini je, unajua kwamba watu wengine siku hizi humfikiria Yesu kama mtoto tu ndani ya hori?— Inakuwa hivyo hasa wakati wa Krismasi ambapo sehemu nyingi Yesu huonyeshwa katika picha akiwa mtoto.

Ijapokuwa Yesu haishi tena duniani, je, unaamini kwamba yuko hai?— Ndiyo, alifufuliwa, na sasa yeye ni Mfalme mwenye nguvu mbinguni. Unafikiri anaweza kufanya nini ili kuwalinda wanaomtumikia?— Alipokuwa duniani, Yesu alionyesha jinsi angewalinda wale wanaompenda. Tuone jinsi alivyofanya hivyo siku moja alipokuwa ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake.

Ni jioni sana. Yesu amekuwa akifundisha mchana kutwa karibu na Bahari ya Galilaya, ambayo ni ziwa kubwa lenye urefu wa karibu kilometa 20 na upana wa kilometa 12. Sasa anawaambia wanafunzi wake hivi: “Na tuvuke mpaka upande ule mwingine wa ziwa.” Basi wanaingia ndani ya mashua na kuanza safari kwenda upande mwingine wa ziwa. Yesu amechoka sana, kwa hiyo anaenda sehemu ya nyuma ya mashua na kutumia mto kujilaza. Usingizi ukamshika haraka.

Yesu anauambia upepo na mawimbi nini?

Wanafunzi wake wanabaki macho ili kuongoza mashua. Hali ni shwari kwa muda, kisha kunatokea upepo mkali wee! Unavuma sana, na mawimbi yanazidi kuwa makubwa. Mashua inayumbayumba na maji yanaanza kuingia.

Wanafunzi wanahofu kwamba wanazama. Lakini Yesu haogopi. Bado analala kule nyuma. Hatimaye wanafunzi wanamwamsha, na kumwambia: ‘Mwalimu, Mwalimu, tuokoe, tuko karibu kufa katika upepo huu.’ Anaposikia hivyo, Yesu anaamka na kuukemea upepo na mawimbi, akisema: “Nyamaza, utulie!”

Mara moja upepo unaacha kuvuma, na ziwa linatulia. Wanafunzi wanastaajabu. Hawajawahi kuona mambo kama hayo. Wanaanza kusemezana: “Kwa kweli huyu ni nani, kwa maana anaagiza hata pepo na maji, nazo zinamtii?”—Luka 8:22-25; Marko 4:35-41.

Je, unajua Yesu ni nani?— Unajua nguvu zake zinatoka wapi?— Wanafunzi hawakupaswa kuogopa wakati Yesu alipokuwa pamoja nao, kwa sababu Yesu si mwanadamu wa kawaida. Yeye angeweza kufanya mambo ya ajabu ambayo hakuna mtu mwingine angeweza kuyafanya. Hebu nikuambie kuhusu jambo jingine alilofanya wakati fulani katika bahari yenye mchafuko.

Ni baadaye siku nyingine. Kunapokuwa jioni, Yesu anawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua na wamtangulie kwenda ng’ambo nyingine ya bahari. Kisha Yesu anaenda peke yake mlimani, mahali patulivu ili asali kwa Baba yake, Yehova Mungu.

Wanafunzi wanaingia ndani ya mashua na kuanza kuivuka bahari. Lakini baadaye kidogo upepo unaanza kuvuma. Unavuma kwa nguvu zaidi na zaidi. Usiku nao umeingia. Wanafunzi hawa wanatoa tanga na kuanza kupiga makasia. Lakini mashua haiendi mbali kwani upepo unawakabili. Mashua inayumbayumba huku na huku katika mawimbi makubwa, na maji yanaingia ndani. Wanang’ang’ana sana kufika ufuoni, lakini wanashindwa.

Yesu bado angali peke yake mlimani. Amekuwa huko kwa muda mrefu. Lakini sasa anaona kwamba wanafunzi wake wako hatarini katika mawimbi hayo makubwa. Kwa hiyo anatoka mlimani na kwenda ufuoni. Yesu anataka kuwasaidia wanafunzi wake, basi anaanza kutembea juu ya bahari yenye dhoruba akiwaelekea!

Kungetokea nini ikiwa ungejaribu kutembea juu ya maji?— Unaweza kuzama na labda kufa. Lakini Yesu ni tofauti. Ana nguvu za pekee. Yesu anahitaji kutembea mbali sana ili afikie mashua. Kwa hiyo ni alfajiri wanafunzi wanapomwona Yesu juu ya maji akija kwao. Lakini hawaamini wanachoona. Wanaogopa sana na kupiga kelele kwa hofu. Kisha Yesu anawaambia: “Jipeni moyo, ni mimi; msiogope.”

Kwa nini Yesu alifanya miujiza?

Mara tu Yesu anapoingia mashuani, dhoruba inakoma. Kwa mara nyingine wanafunzi wanastaajabu. Wanainama mbele ya Yesu na kumwambia: “Wewe kwa kweli ni Mwana wa Mungu.”—Mathayo 14:22-33; Yohana 6:16-21.

Je, haingalipendeza kuishi zamani hizo na kumwona Yesu akifanya mambo kama hayo?—Unajua ni kwa nini Yesu alifanya miujiza hiyo?— Aliifanya kwa sababu aliwapenda wanafunzi wake na alitaka kuwasaidia. Lakini pia alifanya miujiza hiyo ili kuonyesha nguvu alizokuwa nazo na atakazotumia akiwa Mtawala wa Ufalme wa Mungu wakati ujao.

Yesu anawalindaje watumishi wake siku hizi?

Hata leo Yesu hutumia nguvu zake ili kuwalinda wafuasi wake dhidi ya jitihada za Shetani za kutaka kuwakomesha kuhubiria wengine kuhusu Ufalme wa Mungu. Lakini Yesu hatumii nguvu zake kuwalinda wanafunzi wake wasipatwe na magonjwa au kuwaponya wanapokuwa wagonjwa. Hatimaye hata mitume wote wa Yesu walikufa. Yakobo ndugu ya Yohana aliuawa, na Yohana akatiwa gerezani.—Matendo 12:2; Ufunuo 1:9.

Ndivyo ilivyo leo. Wawe wanamtumikia Yehova au la, watu wote wanaweza kuwa wagonjwa na kufa. Lakini mambo yatabadilika karibuni wakati Yesu atatawala akiwa Mfalme wa serikali ya Mungu. Hakuna yeyote atakayeogopa kwa sababu Yesu atatumia nguvu zake ili kuwabariki wote wanaomtii.—Isaya 9:6, 7.

Maandiko mengine yanayoonyesha nguvu nyingi za Yesu, yule ambaye Mungu amfanya kuwa Mtawala katika Ufalme wa Mungu, ni Danieli 7:13, 14; Mathayo 28:18; na Waefeso 1:20-22.