Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mageuzi—Dhana na Ukweli wa Mambo

Mageuzi—Dhana na Ukweli wa Mambo

“Mageuzi ni jambo hakika kama vile joto la jua lilivyo hakika,” adai Profesa Richard Dawkins, mwanasayansi maarufu wa mageuzi.16 Ni kweli kwamba majaribio na mambo yanayoonekana waziwazi yanathibitisha kwamba jua lina joto. Lakini je, majaribio na mambo yanayoonekana wazi yanatoa uthibitisho kama huo, usioweza kupingwa kuhusu fundisho la mageuzi?

Kabla ya kujibu swali hilo, tunahitaji kutatua jambo fulani la msingi. Wanasayansi wengi wameona kwamba kadiri muda unavyopita, vizazi vya baadaye hubadilika kidogo. Kwa mfano, wanadamu wanaweza kuzalisha aina fulani za mbwa ili hatimaye mbwa watakaozaliwa wawe na miguu mifupi au wawe na manyoya marefu kuliko mbwa waliowazaa. * Wanasayansi fulani huyaita mabadiliko hayo madogo-madogo, “mageuzi madogo.”

Hata hivyo, wanamageuzi wanafundisha kwamba mabadiliko madogo-madogo yalijumlika kwa mabilioni ya miaka na kutokeza mabadiliko makubwa hivi kwamba samaki wakawa amfibia na sokwe wakawa binadamu. Nayo hayo yanayorejelewa kuwa mabadiliko makubwa yanaitwa “mageuzi makubwa.”

Charles Darwin na kitabu chake Origin of Species

Kwa mfano, Charles Darwin, alifundisha kwamba mabadiliko madogo-madogo yanayoonekana ni uthibitisho wa kwamba mabadiliko makubwa zaidi, ambayo hakuna yeyote amepata kuyaona, yanawezekana pia.17 Alihisi kwamba katika vipindi virefu vya wakati, viumbe-hai sahili viligeuka polepole—kukiwa na “mabadiliko madogo-madogo sana”—na hatimaye kuwa mamilioni ya viumbe tofauti-tofauti ambavyo viko duniani leo.18

Watu wengi hukubaliana na maoni hayo. Wanajiuliza, ‘Ikiwa mabadiliko madogo-madogo yanaweza kutokea katika spishi mbalimbali, mbona mageuzi yasitokeze mabadiliko makubwa-makubwa baada ya vipindi virefu vya wakati?’ * Hata hivyo, kihalisi fundisho la mageuzi linategemea dhana tatu. Fikiria dhana zifuatazo.

Dhana ya 1. Mabadiliko ya chembe za urithi hutokeza jamii mpya. Fundisho la mageuzi makubwa linategemea dai la kwamba mabadiliko ya chembe za urithi—au mabadiliko yasiyofuata mpangilio maalum katika chembe za urithi za mimea na wanyama—yanaweza kutokeza spishi mpya au hata makundi mapya kabisa ya wanyama na mimea.19

Mabadiliko ya chembe za urithi yanaweza kuleta mabadiliko kwenye mimea—kama huu mmea wenye maua makubwa—lakini mabadiliko hayo yana mipaka

Ukweli wa mambo. Sifa na tabia nyingi za mimea na wanyama hutegemea maagizo yaliyo katika chembe za urithi zilizo katika kiini cha kila chembe. * Watafiti wamegundua kwamba mabadiliko katika chembe za urithi yanaweza kutokeza mabadiliko katika vizazi vya baadaye vya wanyama na mimea. Hata hivyo, je, kweli mabadiliko katika chembe za urithi hutokeza spishi mpya kabisa? Utafiti ambao umefanywa kwa karne moja hivi kuhusu chembe za urithi umefunua nini?

Kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1930, wanasayansi walianza kuunga mkono wazo jipya. Tayari walikuwa wakiamini kwamba ule mchakato wa uteuzi wa kiasili, yaani, kwamba viumbe bora zaidi katika mazingira yake ndio wanaoweza kuendelea kuishi na kuzaana, ungeweza kutokeza spishi mpya za mimea kutokana na mabadiliko yasiyofuata mpangilio maalum. Kwa hiyo, walikata kauli kwamba uteuzi mnemba, au unaofanywa na wanadamu, unaweza kutokeza spishi mpya kwa njia bora zaidi. “Msisimko huo ulienea miongoni wa wanabiolojia wengi, na hasa miongoni mwa wataalamu wa chembe za urithi na wazalishaji wa mimea na wanyama,” akasema Wolf-Ekkehard Lönnig, mwanasayansi katika taasisi moja nchini Ujerumani (Max Planck Institute for Plant Breeding Research). * Kwa nini kukawa na msisimko hivyo? Lönnig, ambaye kwa miaka 30 hivi amekuwa akichunguza mabadiliko ya chembe za urithi za mimea, anasema: “Watafiti hao walidhani wakati wa kubadili njia za msingi za kuzalisha mimea na wanyama umewadia. Walifikiri kwamba kwa kudukiza mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, wangeweza kutokeza mimea na wanyama wapya walio bora zaidi.”20 Hata wengine kati yao wananuia kutokeza spishi mpya kabisa.

Nzi ambao chembe zao za urithi zimebadilika, ijapokuwa wana kasoro, bado ni nzi

Wanasayansi nchini Marekani, Asia, na Ulaya walianzisha miradi ya utafiti iliyogharimu pesa nyingi, wakitumia mbinu walizodhani zingeharakisha mageuzi. Kumekuwa na matokeo gani baada ya utafiti huo ambao umechukua zaidi ya miaka 40? “Licha ya gharama kubwa,” asema mtafiti Peter von Sengbusch, “majaribio ya kutumia unururishaji [ili kubadili chembe za urithi] kutokeza aina mbalimbali zinazoweza kuzaana, yaliambulia patupu.”21 Pia, Lönnig alisema: “Kufikia miaka ya 1980, matumaini na msisimko uliokuwapo miongoni mwa wanasayansi yalikuwa yamegonga mwamba ulimwenguni pote. Utafiti kuhusu uzalishaji wa kudukiza ukiwa kitengo tofauti cha utafiti ulitupiliwa mbali katika nchi za Magharibi. Karibu mimea na wanyama wote waliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi . . . walikufa au walikuwa dhaifu kuliko wale wenye chembe za asili.” *

Hata hivyo, data ambazo kufikia sasa zimekusanywa kwa miaka 100 hivi ya kutafiti mabadiliko ya chembe za urithi kwa ujumla, na hasa miaka 70 ya uzalishaji wa mimea na wanyama kwa kubadili chembe za urithi, zimewawezesha wanasayansi kukata kauli mbalimbali kuhusu uwezo wa kutokeza jamii mpya kwa kubadili chembe hizo. Baada ya kuchunguza matokeo ya utafiti huo, Lönnig alikata kauli hii: “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa. Kauli hiyo inapatana na majaribio na matokeo ya utafiti ambayo yamefanywa katika karne ya 20 na pia inapatana na sheria za welekeo.”

Hivyo basi, je, mabadiliko ya chembe za urithi yanaweza kubadili spishi moja iwe kiumbe kingine kipya kabisa? Matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba haiwezekani. Kutokana na utafiti mbalimbali ambao amefanya, Lönnig amekata kauli kwamba “spishi zinazotambulika waziwazi zina mipaka ambayo haiwezi kufutiliwa mbali wala kukiukwa na mabadiliko yoyote katika chembe za urithi yanayotokea bila mpangilio wowote.”22

Fikiria kinachomaanishwa na uthibitisho huo. Ikiwa wanasayansi stadi wameshindwa kutokeza spishi mpya kwa kudukiza mabadiliko na kuteua chembe bora za urithi, itawezekanaje basi mchakato usiotegemea akili yoyote ufaulu kufanya hivyo? Ikiwa utafiti unaonyesha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadilisha spishi za awali na kutokeza spishi mpya kabisa, basi, yale mageuzi makubwa yatawezekanaje?

Dhana ya 2. Uteuzi wa kiasili ulitokeza spishi mpya. Darwin aliamini kwamba ule aliourejelea kuwa uteuzi wa kiasili ungetegemeza viumbe bora zaidi, ilhali viumbe dhaifu hatimaye vingekufa na kutoweka. Wanamageuzi wa kisasa wanafundisha kwamba kadiri spishi zilivyoenea na kutapakaa, ndivyo uteuzi wa kiasili ulivyoteua viumbe ambavyo chembe zao za urithi zilibadilika na kujipatanisha zaidi na mazingira yao mapya. Kwa hiyo, wanamageuzi wanadai kwamba spishi hizo zilizotapakaa hatimaye zilitokeza spishi mpya kabisa.

Ukweli wa mambo. Kama tulivyoona, kuna uthibitisho wa kutosha unaoonyesha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kamwe kutokeza aina mpya kabisa za mimea na wanyama. Hata hivyo, wanamageuzi wana uthibitisho gani wa kuunga mkono dai lao kwamba uteuzi wa kiasili huchagua chembe bora za urithi zilizobadilika ili kutokeza spishi mpya? Broshua iliyochapishwa mnamo 1999 na Shirika la Kitaifa la Sayansi (NAS) nchini Marekani ilirejelea “spishi 13 za shore waliochunguzwa na Darwin katika Visiwa vya Galápagos, ambao leo wanaitwa shore wa Darwin.”23

Katika miaka ya 1970, watafiti kadhaa wakiongozwa na Peter R. na B. Rosemary Grant wa Chuo Kikuu cha Princeton, walianza kuwachunguza shore hao nao wakagundua kwamba baada ya mwaka mzima wa ukame katika visiwa hivyo, kulikuwa na shore wengi zaidi wenye midomo mirefu kuliko wale wenye midomo mifupi. Kwa kuwa mojawapo ya njia za msingi za kuainisha spishi 13 za shore ni kuchunguza ukubwa na umbo la midomo yao, matokeo ya uchunguzi huo yalionwa kuwa muhimu sana. Broshua hiyo ya NAS yaendelea kusema: “Akina Grant wamekadiria kwamba ukame ukitokea mara moja kila baada ya miaka 10 katika visiwa hivyo, baada ya miaka 200 hivi tu, spishi mpya ya shore itatokea.”24

Hata hivyo, broshua hiyo ya NAS inakosa kutaja kwamba katika miaka iliyofuata miaka ya ukame, kulikuwa na shore wengi zaidi wenye midomo mifupi. Watafiti hao waligundua kwamba jinsi hali ya hewa ilivyokuwa ikibadilika kisiwani, mwaka mmoja kulikuwa na shore wengi zaidi wenye midomo mirefu, lakini baadaye kukawa na shore wengi zaidi wenye midomo mifupi. Pia waligundua kwamba baadhi ya “spishi” hizo tofauti za shore zilizalishana kwa mtambuka na kutokeza vizazi vilivyostahimili vizuri zaidi kuliko vizazi vya awali. Walikata kauli kwamba ikiwa ndege hao wangeendelea kuzalishana kwa njia hiyo, “spishi” hizo mbili hatimaye zingeungana na kuwa spishi moja.25

Shore wa Darwin wanathibitisha jambo moja tu, kwamba wanaweza kuzoeleana na mazingira mageni

Basi je, kwa kweli uteuzi wa kiasili hutokeza spishi mpya kabisa? Makumi ya miaka iliyopita, mtaalamu wa biolojia ya mageuzi George Christopher Williams alianza kutilia shaka ikiwa uteuzi wa kiasili unaweza kufanya hivyo.26 Mwaka wa 1999, mtaalamu wa nadharia ya mageuzi Jeffrey H. Schwartz aliandika kwamba uteuzi wa kiasili unaweza kusaidia spishi mbalimbali kubadilika kulingana na jinsi hali zinavyobadilika, lakini hautokezi chochote kipya.27

Kwa kweli, shore wa Darwin hawajabadilika na kuwa “kitu chochote kipya.” Bado wao ni shore. Na uhakika wa kwamba shore hao wanazalishana kwa mtambuka unafanya mbinu za wanamageuzi fulani za kuainisha spishi zitiliwe shaka. Isitoshe, utafiti kuhusu ndege hao umefichua kwamba hata taasisi za kisayansi zenye kuheshimika zinaweza kuripoti matokeo ya utafiti mbalimbali zikiegemea upande mmoja.

Dhana ya 3. Rekodi ya visukuku (mabaki ya viumbe na vitu vya kale) inathibitisha mabadiliko ya mageuzi makubwa. Broshua ya NAS iliyotajwa awali humfanya msomaji aamini kwamba visukuku ambavyo wanasayansi wamepata vinathibitisha kabisa kwamba mageuzi makubwa yalitokea. Inasema: “Visukuku vya hatua nyingi mbalimbali za mageuzi kati ya samaki na amfibia, kati ya amfibia na reptilia, kati ya reptilia na mamalia, na katika mamalia wa hali ya juu, vimegunduliwa hivi kwamba mara nyingi ni vigumu kuainisha kikamili wakati ambapo spishi moja inabadilika na kuwa spishi nyingine.”28

Ukweli wa mambo. Taarifa hiyo inayosemwa kwa usadikisho katika broshua hiyo ya NAS inashangaza sana. Kwa nini? Niles Eldredge, anayeshikilia sana fundisho la mageuzi, anasema kwamba rekodi ya visukuku haionyeshi kwamba kuna mabadiliko yanayotokea hatua kwa hatua, bali kwamba katika vipindi virefu vya wakati “ni mabadiliko madogo sana au hata hakuna mabadiliko yanayotokea katika spishi zilizo nyingi.” *29

Kulingana na rekodi ya visukuku, vikundi vyote vikuu vya wanyama vilitokea ghafula navyo havijabadilika

Kufikia leo, wanasayansi ulimwenguni pote wamechimbua na kurekodi visukuku vikubwa milioni 200 na mabilioni ya visukuku vidogo. Watafiti wengi wanakiri kwamba rekodi hiyo kubwa ya visukuku inaonyesha kwamba vikundi vyote vikuu vya wanyama vilitokea ghafula navyo havijabadilika sana, huku spishi nyingi zikitoweka ghafula jinsi tu zilivyotokea.

Mageuzi—Fundisho Linalohitaji “Imani”

Kwa nini wanamageuzi wengi mashuhuri hudai kwamba yale yanayoitwa mageuzi makubwa ni jambo hakika? Richard Lewontin, mtu mashuhuri anayeamini mageuzi aliandika waziwazi kwamba wanasayansi wengi hukubali kwa urahisi madai ya kisayansi ambayo hayajathibitishwa kwa sababu ya “agano ambalo tayari limefanywa, agano la uyakinifu.” * Wanasayansi wengi hukataa hata kufikiria uwezekano wa kuwa kuna Mbuni mwenye akili kwa sababu, kama Lewontin alivyoandika, “hatuwezi kumruhusu Mungu akanyage mlangoni petu.”30

Kuhusiana na hilo, mwanasosiolojia Rodney Stark ananukuliwa katika jarida Scientific American akisema: “Wazo la kwamba ukitaka kuwa mwanasayansi lazima uepushe akili yako na minyororo ya dini limekuwa likipigiwa debe kwa zaidi ya miaka 200.” Pia anataja kwamba katika vyuo vikuu vya utafiti, “watu wenye maelekeo ya kidini hufyata midomo yao.”31

Ikiwa unaamini fundisho la mageuzi makubwa kuwa la kweli, lazima uamini kwamba wanasayansi waagnosti au waatheisti hawawezi kamwe kuruhusu maoni yao yaathiri kauli zao wanapofanya utafiti. Lazima uamini kwamba vitu vyote vyenye uhai vilitokana na mabadiliko ya chembe za urithi na uteuzi wa kiasili, ijapokuwa utafiti ambao umefanywa kwa karne moja unaonyesha kwamba mabadiliko ya chembe hayajabadili hata spishi moja inayojulikana wazi iwe kitu kingine kipya kabisa. Lazima uamini kuwa viumbe vyote viligeuka polepole kutoka kwa kiumbe kimoja, ijapokuwa rekodi ya visukuku inaonyesha kwamba aina kuu za mimea na wanyama zilitokea ghafula na hazijabadilika na kuwa aina nyingine, hata baada ya muda mrefu sana kupita. Je, unafikiri imani kama hiyo inategemea ukweli wa mambo au dhana tu? Kwa kweli, ili kuamini mageuzi mtu anahitaji “imani.”

^ fu. 3 Mabadiliko katika mbwa wanaozalishwa mara nyingi hutokana na kasoro katika utendaji wa chembe za urithi. Kwa mfano, mbwa anayeitwa dachshund ana umbo dogo kwa sababu gegedu zake zimedumaa.

^ fu. 6 Ingawa neno “spishi” linatumiwa mara nyingi katika sehemu hii, kumbuka kwamba neno hilo halipatikani katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo. Kitabu hicho kinatumia neno “aina” ambalo lina maana pana zaidi. Mara nyingi kile ambacho wanasayansi hukiita spishi mpya ni tofauti ndogo-ndogo katika “aina” zinazozungumziwa katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo.

^ fu. 8 Utafiti unaonyesha kwamba uteseli, tando, na maumbile mengine ya chembe hutimiza fungu muhimu katika kutokeza umbo na utendaji wa kiumbe.

^ fu. 9 Lönnig anaamini kwamba uhai ulitokana na uumbaji. Maelezo yake katika broshua hii ni maoni yake mwenyewe wala hayawakilishi maoni ya taasisi ya Max Planck Institute for Plant Breeding Research.

^ fu. 10 Katika majaribio mengi ya kubadili chembe za urithi, idadi ya viumbe wapya ilizidi kupungua huku aina zilezile za mimea na wanyama zikitokezwa. Isitoshe, chini ya asilimia 1 ya mimea iliyotokezwa kwa kubadili chembe za urithi ndiyo iliyoteuliwa kwa ajili ya utafiti zaidi, na chini ya asilimia 1 ya mimea hiyo iliyoteuliwa ndiyo iliyofaa kwa matumizi ya kibiashara. Hata hivyo, hakuna hata spishi moja mpya kabisa iliyotokezwa. Matokeo ya utafiti uliohusisha wanyama yalikuwa duni hata kuliko yale ya mimea hivi kwamba majaribio hayo yalitupiliwa mbali.

^ fu. 21 Hata mifano michache kutoka katika rekodi ya visukuku ambayo watafiti wanarejelea kuwa uthibitisho wa mageuzi inaweza kuzua ubishi. Ona ukurasa wa 22 hadi 29 wa broshua, Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai, iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

^ fu. 24 Katika muktadha huu, “uyakinifu” ni nadharia ya kwamba vitu vyote ulimwenguni, kutia ndani uhai wote, vilitokea bila nguvu zozote zisizo za kawaida kuingilia kati hata kidogo.