Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SWALI LA 1

Uhai Ulianzaje?

Uhai Ulianzaje?

Ulipokuwa mtoto mdogo, uliwauliza wazazi wako, “Watoto hutoka wapi?” Ikiwa uliwauliza, walikujibu namna gani? Ikitegemea umri wako na utu wao, huenda wazazi wako walilipuuza swali hilo au walikujibu tu kijuu-juu tena kwa aibu. Au labda walikuambia hadithi fulani iliyobuniwa ambayo baadaye uligundua ni ya uwongo. Bila shaka, ili kumtayarisha mtoto kwa ajili ya maisha ya utu-uzima na ndoa, atahitaji pia kufundishwa jinsi wanadamu wanavyozaana.

Kama vile tu wazazi hushindwa kuzungumzia mahali watoto wanakotoka, wanasayansi fulani hushindwa kuzungumzia swali lililo muhimu zaidi—Uhai ulitoka wapi? Kupata jibu lenye kusadikisha kuhusu swali hilo kunaweza kumsaidia mtu kuwa na mtazamo unaofaa kuelekea uhai. Hivyo basi, uhai ulianzaje?

Chembe ya yai lililotungishwa la mwanadamu, ikiwa imekuzwa mara 800

Wanasayansi wengi husema nini? Wengi wanaoamini mageuzi watakuambia kwamba uhai ulianza mabilioni ya miaka iliyopita kwenye ukingo wa kidimbwi cha kale kilichojaa maji wakati wa kupwa au katika sehemu za chini ya bahari. Wao huhisi kwamba katika maeneo yasiyojulikana kama hayo, kemikali zilijikusanya na kuwa vitu vinavyofanana na mapovu, vikafanyiza molekuli tata, na kuanza kujigawanya-gawanya. Wanaamini kwamba uhai wote duniani ulijitokeza wenyewe tu kutokana na chembe “sahili,” moja au zaidi.

Wanasayansi wengine wanaoheshimika ambao pia wanaunga mkono mageuzi hawakubaliani na wazo hilo. Wanakisia kwamba chembe za kwanza au angalau sehemu zake kuu zilikuja duniani kutoka anga la nje. Kwa nini? Kwa sababu, licha ya jitihada zao nyingi, wanasayansi hawajaweza kuthibitisha kwamba uhai unaweza kutokea ghafula kutokana na molekuli zinazodhaniwa zilitokeza uhai. Katika mwaka wa 2008, Alexandre Meinesz, Profesa wa Biolojia, alizungumzia utata huo. Alisema kwamba kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, “hakuna uthibitisho wowote uliopatikana kupitia majaribio yaliyofanywa unaounga mkono nadharia ya kwamba uhai ulitokea ghafula Duniani kutokana na molekuli fulani, wala hakuna maendeleo ya kisayansi yanayoweza kuthibitisha hilo.”1

Uthibitisho unafunua nini? Jibu la swali, Watoto hutoka wapi? limethibitishwa na haliwezi kupingwa. Sikuzote uhai hutokana na uhai ambao tayari upo. Hata hivyo, tukirudi nyuma miaka mingi iliyopita, inawezekana kwamba sheria hiyo ya msingi ilivunjwa? Inawezekana kweli kwamba uhai ulijitokeza wenyewe kutokana na kemikali zisizo hai? Kuna uwezekano wowote kwamba jambo hilo linaweza kutokea?

Watafiti wamegundua kwamba ili chembe iendelee kuwa hai, angalau aina tatu tofauti za molekuli tata lazima zifanye kazi pamoja—DNA au deoksiribonyukilia asidi, RNA (ribonucleic acid), na protini. Leo, ni wanasayansi wachache wanaoweza kudai kwamba chembe kamili iliyo hai ilijitokeza yenyewe kutokana na mchanganyiko wa kemikali zisizo hai. Hata hivyo, kuna uwezekano gani kwamba RNA au protini zinaweza kujitokeza zenyewe? *

Stanley Miller, 1953

Wanasayansi wengi huhisi kwamba huenda uhai ulijitokeza wenyewe kwa sababu ya jaribio fulani lililofanywa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1953. Mwaka huo, Stanley L. Miller aliweza kutengeneza asidi-amino, kemikali za msingi zinazofanyiza protini, kwa kupitisha nguvu za umeme ndani ya mchanganyiko wa gesi zilizodhaniwa kuwa zingewakilisha anga la dunia. Tangu wakati huo, asidi-amino zimepatikana pia katika vimondo. Ugunduzi huo unamaanisha kwamba kemikali za msingi za uhai zinaweza kujitokeza tu zenyewe?

Robert Shapiro, aliyekuwa profesa wa kemia katika Chuo Kikuu cha New York, asema: “Baadhi ya waandikaji wameamini kwamba kemikali zote za msingi za uhai zinaweza kutengenezwa kwa urahisi kwa kutumia majaribio kama yale ya Miller na kwamba zinapatikana katika vimondo. Hata hivyo sivyo ilivyo.”2 *

Fikiria molekuli ya RNA. Imefanyizwa na molekuli ndogo zinazoitwa nukliotidi. Nukliotidi ni aina tofauti ya molekuli na ni tata zaidi kidogo kuliko asidi-amino. Shapiro anasema kwamba “hakuna nukliotidi za aina yoyote zinazoripotiwa kuwa zilitokana na majaribio yanayohusisha umeme wala katika uchunguzi wa vimondo.”3 Pia anasema kwamba uwezekano wa molekuli kujifanyiza bila mpangilio maalum na kujikusanya kutoka kwa kemikali nyingi za msingi “ni mdogo sana hivi kwamba hata kama ungetokea mahali popote katika ulimwengu unaoonekana, lingeonwa bahati njema.”4

RNA 1 inahitajika ili kutengeneza protini 2, hata hivyo, protini zinahusika katika utengenezaji wa RNA. Inawezekana kweli kwamba yoyote ya molekuli hizo ilijitokeza yenyewe? Ribosomu 3 itazungumziwa katika sehemu ya 2.

Namna gani molekuli za protini? Zinaweza kufanyizwa kutokana na asidi-amino 50 hivi au maelfu kadhaa ya amino-asidi zilizokusanywa pamoja katika mpangilio hususa wa hali ya juu. Protini ya wastani katika chembe yoyote ina amino-asidi 200. Hata katika chembe hizo kuna maelfu ya aina tofauti-tofauti za protini. Uwezekano wa kwamba protini moja tu iliyo na amino-asidi 100 pekee ingeweza kujifanyiza kwa njia isiyo na mpangilio maalum duniani, umekadiriwa kuwa mara moja tu hivi baada ya kufanya majaribio hayo mara milioni bilioni.

Ikiwa kutengeneza molekuli tata katika maabara kunahitaji mwanasayansi mwenye ujuzi, je, inawezekana kwamba molekuli tata zaidi zilizo katika chembe zilijitokeza zenyewe?

Mtafiti Hubert P. Yockey, anayeunga mkono fundisho la mageuzi ana maelezo zaidi. Anasema: “Haiwezekani kwamba chanzo cha uhai ni ‘protini tu.’”5 RNA inahitajika kutengeneza protini, hata hivyo, protini zinahusika katika utengenezaji wa RNA. Namna gani ikiwa, licha ya uwezekano huo mdogo sana, protini na molekuli ya RNA zingetokea mahali pamoja wakati uleule? Kuna uwezekano wowote kwamba zinaweza kufanyiza uhai unaoweza kutokeza chembe ambazo zinaweza kuzaana na kuendeleza uhai? “Yaelekea uwezekano wa jambo hilo kujitokeza lenyewe (kukiwa na mchanganyiko usio na mpangilio maalum wa protini na RNA) ni mdogo sana,” asema Dkt. Carol Cleland *, mshiriki wa NASA (National Aeronautics and Space Administration’s Astrobiology Institute). “Hata hivyo,” aendelea, “yaelekea watafiti wengi wanafikiri kwamba ikiwa wataelewa jinsi protini na RNA zinavyojifanyiza kupitia njia za asili, basi kwa njia fulani haitakuwa vigumu kuelewa jinsi kemikali hizo zinavyoshirikiana.” Kuhusu nadharia za leo zinazoeleza jinsi huenda kemikali hizo za msingi zilivyojitokeza zenyewe, anasema: “Hakuna yoyote kati ya nadharia hizo inayoeleza kwa usahihi jinsi jambo hilo lilivyotukia.”6

Ikiwa mtu mwenye akili anahitajiwa kubuni roboti isiyo na uhai na kuiwezesha kutenda, je, mtu mwenye akili nyingi zaidi hahitajiwi ili kuumba chembe iliyo hai na hata zaidi mwanadamu?

Kwa nini ukweli huu ni muhimu? Wazia changamoto inayowakabili watafiti ambao huamini kwamba uhai ulijitokeza wenyewe. Wamepata amino-asidi fulani ambazo zinapatikana pia katika chembe zilizo hai. Kupitia majaribio yaliyofanywa kwa ustadi mkubwa, wametengeneza molekuli tata zaidi katika maabara zao. Hatimaye, wanatarajia kutengeneza sehemu zote zinazohitajiwa ili kuunda chembe “sahili.” Hali yao inaweza kulinganishwa na ya mwanasayansi anayechukua vitu vya asili na kuvigeuza kuwa chuma, plastiki, silikoni, na waya; kisha anatengeneza roboti. Halafu anairatibu roboti hiyo ili iweze kutengeneza roboti nyingine zinazofanana nayo. Kwa kufanya hivyo, anathibitisha nini? Kwamba mtu mwenye akili anaweza kutengeneza mashini yenye kuvutia.

Vivyo hivyo, ikiwa wanasayansi watawahi kutengeneza chembe, watakuwa wametimiza jambo lenye kustaajabisha kwelikweli—hata hivyo, je, watakuwa wakithibitisha kwamba chembe hiyo inaweza kujitokeza yenyewe bila mwelekezo wowote? Kinyume cha hilo, watakuwa wanathibitisha jambo lililo tofauti kabisa, sivyo?

Una maoni gani? Uthibitisho wote wa kisayansi kufikia sasa unaonyesha kwamba uhai unaweza kutokezwa tu na uhai ambao tayari upo. Kuamini kwamba hata chembe “sahili” iliyo hai ilijitokeza yenyewe kutokana na kemikali zisizo na uhai, kunahitaji imani kubwa isiyo na msingi.

Ukiwa na ukweli huo, uko tayari kuwa na imani kama hiyo? Kabla ya kujibu swali hilo, chunguza kwa makini jinsi ambavyo chembe zimetengenezwa. Kufanya hivyo kutakusaidia kuamua ikiwa nadharia ambazo wanasayansi fulani wamefundisha kuhusu chanzo cha uhai ni za kweli, au ni kama hadithi za kubuniwa ambazo wazazi fulani huwaambia watoto wao kuhusu mahali ambapo watoto hutoka.

^ fu. 8 Uwezekano wa DNA kujifanyiza yenyewe utazungumziwa katika sehemu ya 3, “Maagizo Yalitoka Wapi?

^ fu. 10 Profesa Shapiro haamini kwamba uhai ulitokana na Muumba. Anaamini kuwa uhai ulijitokeza wenyewe kwa njia fulani ambayo bado haijaeleweka. Mwaka wa 2009 wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza, waliripoti kwamba wametengeneza nukliotidi katika maabara yao. Hata hivyo, Shapiro anasema kwamba viambato vyao “bila shaka havifikii viwango vyangu vinavyokubalika vya kutengeneza RNA.”

^ fu. 13 Dkt. Cleland haamini masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji. Anaamini kwamba uhai ulijitokeza wenyewe katika njia fulani ambayo bado haijaeleweka vizuri.