Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nimekwama Katikati ya Tamaduni Tofauti—Nifanyeje?

Nimekwama Katikati ya Tamaduni Tofauti—Nifanyeje?

SURA YA 22

Nimekwama Katikati ya Tamaduni Tofauti—Nifanyeje?

Baba au mama yako ni mhamiaji?

□ Ndiyo □ Hapana

Lugha inayozungumzwa shuleni na utamaduni wa wanafunzi wenzako ni tofauti na nyumbani kwenu?

□ Ndiyo □ Hapana

“Sisi ni Waitaliano, na Waitaliano ni waongeaji na wachangamfu sana. Sasa tunaishi Uingereza. Waingereza wanaonekana wanyamavu na wenye sheria nyingi. Nahisi kama mkosa kabila, si Mwingereza, si Mwitaliano.”—Giosuè, Uingereza.

“Shuleni mwalimu aliniambia nimtazame anapozungumza. Lakini ninapomtazama Baba anapozungumza, anasema kukodolea watu macho ni kukosa adabu. Nilihisi nimechanganyikiwa.” —Patrick, aliyezaliwa nchini Ufaransa na wazazi wahamiaji kutoka Algeria.

WAZAZI wako walipohama, mambo hayakuwa rahisi. Ghafula walijikuta katikati ya watu ambao lugha, utamaduni, na mavazi yao yalikuwa tofauti kabisa. Walionekana wageni popote walipokuwa. Kwa sababu hiyo, huenda walidharauliwa na kubaguliwa.

Imekuwa hivyo kwako pia? Yaliyoorodheshwa hapa chini ni baadhi ya matatizo ambayo vijana wengine walio katika hali hiyo wamekabili. Tia alama ya ✔ kando ya tatizo unaloona kuwa gumu sana kushughulika nalo.

Kuchekwa. Noor alikuwa msichana mdogo familia yao ilipohamia Amerika Kaskazini kutoka Jordan. “Tulikuwa tukivalia kwa njia tofauti, kwa hiyo watu walikuwa wakitucheka,” anasema. “Isitoshe, hatukuwa tukielewa utani wa Wamarekani.”

Mkosa-kabila. “Nilizaliwa Ujerumani,” asema msichana anayeitwa Nadia. “Kwa kuwa wazazi wangu ni Waitaliano, nilikuwa nikizungumza Kijerumani kwa matamshi ya Kiitaliano, nao watoto shuleni walikuwa wakiniita ‘mgeni mshamba.’ Lakini ninapoenda Italia, najikuta nikizungumza Kiitaliano kwa matamshi ya Kijerumani. Kwa hiyo, najiona kuwa mkosa-kabila. Popote ninapoenda, mimi ni mgeni.”

Tamaduni tofauti nyumbani. Ana alikuwa na umri wa miaka minane familia yao ilipohamia Uingereza. Anasema: “Ilikuwa rahisi kwangu na kwa ndugu yangu kuzoea maisha ya London. Lakini haikuwa rahisi kwa wazazi wangu, ambao kwa miaka mingi waliishi Madeira, kisiwa kidogo cha Ureno.”

Voeun alikuwa na umri wa miaka mitatu familia yao ilipohamia Australia kutoka Kambodia. “Bado wazazi wangu hawajazoea utamaduni na mazingira mapya,” anasema. “Mara nyingi Baba anakasirika kwa sababu simwelewi.”

Kizuizi cha lugha nyumbani. Ian alikuwa na umri wa miaka minane familia yao ilipohamia New York kutoka Ekuado. Baada ya kuishi Marekani kwa miaka sita, anasema: “Sasa nazungumza Kiingereza vizuri kuliko Kihispania. Walimu shuleni huzungumza Kiingereza, rafiki zangu huzungumza Kiingereza, nami huzungumza Kiingereza na ndugu yangu. Hivyo, Kiingereza kinazidi kuchukua mahali pa Kihispania.”

Lee, aliyezaliwa Australia na wazazi kutoka Kambodia, anasema: “Ninapozungumza na wazazi wangu na kutaka kuwaeleza mambo waziwazi, ninashindwa kuzungumza lugha yao vizuri.”

Noor, aliyetajwa mapema, anasema: “Baba yangu alijaribu sana kusisitiza tuzungumze lugha yake tunapokuwa nyumbani, lakini hatukutaka kuongea Kiarabu. Tuliona kujifunza Kiarabu kuwa mzigo usio wa lazima. Rafiki zetu walikuwa wakizungumza Kiingereza. Vipindi vyote vya televisheni tulivyotazama vilikuwa vya Kiingereza. Kiarabu kina kazi gani?”

Unaweza Kufanya Nini?

Kama masimulizi hayo yanavyoonyesha, kuna wengi wenye matatizo kama yako. Badala ya kujaribu kushughulika na hali hizo, huenda ukaamua kutupilia mbali utamaduni wenu na kuzoeleana na mazingira yako mapya. Hata hivyo, huenda kufanya hivyo kukawaudhi wazazi wako nawe utamauke. Badala yake, kwa nini usijifunze kuyashughulikia matatizo hayo na ujaribu kunufaika kutokana nayo? Fikiria madokezo yafuatayo:

Jinsi ya kushughulika na dhihaka. Hata ufanye nini, huwezi kupendwa na kila mtu. Nyakati zote watu wanaofurahia kuwadhihaki wengine hawatakosa sababu ya kufanya hivyo. (Methali 18:24) Kwa hiyo, usipoteze wakati ukijaribu kubadili maoni yao yenye ubaguzi. “Mtu mwenye madharau hapendi kuonywa,” akasema Mfalme Sulemani. (Methali 15:12, Biblia Habari Njema) Maneno ya ubaguzi hufunua kupungukiwa kwa mwenye kuyasema, wala si anayesemwa.

Jinsi ya kushughulikia hali ya kuwa “mkosa-kabila.” Ni kawaida kutaka kuwa sehemu ya kikundi fulani, kama vile familia au utamaduni. Hata hivyo, ni kosa kufikiri kwamba thamani yako inategemea utamaduni au malezi. Huenda watu wakakupima kulingana na mambo hayo, lakini Mungu hafanyi hivyo. “Mungu hana ubaguzi,” akasema mtume Petro. “Katika kila taifa mtu ambaye anamwogopa na kutenda uadilifu anakubalika kwake.” (Matendo 10:34, 35) Ukijitahidi kumpendeza Yehova Mungu, atakuona kuwa sehemu ya familia yake. (Isaya 43:10; Marko 10:29, 30) Hakuna “kabila” bora kuliko hilo!

Jinsi ya kushughulika na tofauti za kitamaduni nyumbani. Karibu katika kila familia, wazazi na watoto huwa na maoni yanayotofautiana. Katika hali zako, huenda tofauti hizo zikaonekana kuwa kubwa hata zaidi—wazazi wanataka uishi kulingana na desturi za nchi mliyotoka, nawe unataka kuishi kulingana na desturi za makao yenu mapya. Hata hivyo, ikiwa unataka mambo yakuendee vema katika maisha yako, lazima ‘umheshimu baba yako na mama yako.’—Waefeso 6:2, 3.

Badala ya kukataa desturi za wazazi wako kwa sababu hazikufai, jaribu kutambua kinachofanya wazazi wako waheshimu desturi hizo. (Methali 2:10, 11) Jiulize maswali yafuatayo: ‘Je, desturi hizo zinapingana na kanuni za Biblia? Ikiwa sivyo, ni nini hasa kuhusu desturi hizo ambacho sipendi? Ni kwa njia gani ninaweza kuzungumza na wazazi wangu kwa heshima na kuwaeleza maoni yangu?’ (Matendo 5:29) Bila shaka, itakuwa rahisi zaidi kuwaheshimu wazazi wako—kuelewa maoni yao na kueleza hisia zako—ikiwa unajua kuzungumza lugha yao vizuri.

Jinsi ya kushinda tofauti za lugha nyumbani. Familia kadhaa zimeona kwamba ikiwa watazungumza lugha ya mama peke yake wanapokuwa nyumbani, watoto watajifunza lugha zote mbili. Mnaweza kujaribu hilo nyumbani kwenu. Pia, unaweza kuwaomba wazazi wako wakusaidie kujifunza kuandika lugha yenu. Stelios, aliyelelewa Ujerumani lakini lugha yake ni Kigiriki, anasema: “Wazazi wangu walizoea kusoma andiko la Biblia pamoja nami kila siku. Walikuwa wakisoma kwa sauti, nami ninaandika. Sasa ninaweza kusoma na kuandika Kigiriki na Kijerumani.”

Kuna faida gani nyingine? “Nilijifunza lugha ya wazazi wangu kwa sababu nilitaka kuwa na uhusiano wa karibu pamoja nao kihisia, na hasa kiroho,” asema Giosuè, aliyetajwa awali. “Kujifunza lugha yao kumenisaidia kuwaelewa. Nao pia wananielewa.”

Daraja, Si Kizuizi

Unauonaje utamaduni wenu? Kuwa kizuizi kinachokutenga na wengine au kama daraja linalokuunganisha nao? Vijana wengi Wakristo wamegundua kwamba wana sababu nyingine ya kutaka kuziba pengo lililopo kati ya tamaduni. Wangependa kuwaambia wahamiaji wengine kuhusu habari njema za Ufalme wa Mungu. (Mathayo 24:14; 28:19, 20) “Kuweza kueleza Maandiko katika lugha mbili ni pendeleo!” asema Salomão, aliyehamia London akiwa na umri wa miaka mitano. “Nilikuwa karibu kusahau lugha yangu ya mama, lakini sasa kwa kuwa niko katika kutaniko la Kireno, ninaweza kuzungumza kwa ufasaha Kiingereza na Kireno.”

Noor, aliyetajwa mapema, aliona kuna uhitaji wa wahubiri wanaoweza kuzungumza Kiarabu. Anasema: “Sasa ninajifunza lugha hiyo, na kuanza kufufua mambo niliyokuwa nimesahau. Mtazamo wangu umebadilika. Sasa ninataka kurekebishwa ninapozungumza Kiarabu. Ninataka kujifunza.”

Bila shaka, ikiwa unaelewa tamaduni mbili na unaweza kuzungumza lugha mbili au zaidi, una faida kwelikweli. Kujua tamaduni mbili kunakusaidia kuelewa hisia za watu na kujibu maswali yao kuhusu Mungu. (Methali 15:23) Preeti aliyezaliwa nchini Uingereza, na ambaye wazazi wake ni Wahindi, anasema, “Kwa kuwa ninaelewa tamaduni mbili, sina wasiwasi ninapokuwa katika huduma. Ninawaelewa watu wa tamaduni zote mbili, yaani naelewa imani na mitazamo yao.”

Unaweza kuona hali zako kuwa baraka badala ya kuziona kuwa kizuizi? Kumbuka, Yehova anakupenda jinsi ulivyo, bali si kwa sababu ya nchi ambayo wewe na familia yenu mnatoka. Kama vijana walionukuliwa hapa, unaweza kutumia ujuzi ulio nao kuwasaidia wengine wanaozungumza lugha yenu wajifunze kumhusu Yehova, Mungu wetu mwenye upendo asiye na ubaguzi? Ukifanya hivyo, utapata furaha ya kweli!—Matendo 20:35.

ANDIKO MUHIMU

“Mungu hana ubaguzi.”—Matendo 10:34.

PENDEKEZO

Ikiwa vijana wenzako wanakudhihaki kwa sababu ya malezi yako, usivunjwe moyo na dhihaka zao badala yake cheka pamoja nao. Acha waseme, mwishowe watachoka.

JE, WAJUA . . . ?

Ukijifunza vizuri lugha mbili, unaweza kuongeza uwezekano wako wa kupata kazi.

HATUA ZA KUCHUKUA!

Ili kuelewa vizuri zaidi lugha ya wazazi wangu, nita ․․․․․

Mambo ambayo ningependa kuuliza mzazi (wazazi) wangu kuhusu habari hii ni ․․․․․

UNA MAONI GANI?

● Kujua malezi na utamaduni wa wazazi wako kutakusaidia jinsi gani kujielewa vizuri zaidi?

● Unapojilinganisha na vijana waliolelewa katika utamaduni mmoja, ni mambo gani unayoweza kufurahia ambayo wao hawana?

[Blabu katika ukurasa wa 160]

“Ninakuwa na furaha ninapowasaidia wengine. Ninaweza kuwaeleza maandiko ya Biblia watu wanaozungumza Kirusi, Kifaransa, au Kimoldova.”—Oleg

[Picha katika ukurasa wa 161]

Unaweza kuamua kuona utamaduni wenu kuwa daraja linalokuunganisha na wengine