Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 5

Yesu Alizaliwa Wapi na Wakati Gani?

Yesu Alizaliwa Wapi na Wakati Gani?

LUKA 2:1-20

  • YESU AZALIWA HUKO BETHLEHEMU

  • WACHUNGAJI WAMTEMBELEA MTOTO YESU

Kaisari Augusto, maliki wa Milki ya Roma, ameagiza kwamba kila mtu anapaswa kuandikishwa. Basi Yosefu na Maria wanapaswa kusafiri hadi jiji alikozaliwa Yosefu, jiji la Bethlehemu, upande wa kusini wa Yerusalemu.

Watu wengi wamekuja Bethlehemu ili kuandikishwa. Sehemu pekee ya kukaa ambayo Yosefu na Maria wanapata ni katika zizi, ambako punda na wanyama wengine huwekwa. Yesu anazaliwa hapo. Maria anamfunga kwa vitambaa na kumlaza katika hori, mahali ambapo chakula cha wanyama huwekwa.

Lazima iwe kwamba Mungu alihakikisha Kaisari Augusto anaagiza watu waandikishwe. Kwa nini? Kwa sababu hilo lilifanya iwezekane kwa Yesu kuzaliwa huko Bethlehemu, jiji alikozaliwa Mfalme Daudi, babu yake. Maandiko yalikuwa yametabiri zamani kwamba Mtawala aliyeahidiwa angezaliwa katika jiji hilo.—Mika 5:2.

Huu ni usiku muhimu sana! Katika viwanja vya malisho, mwangaza mkubwa unaangaza kuzunguka kikundi cha wachungaji. Ni utukufu wa Yehova! Mmoja wa malaika wa Mungu anawaambia wachungaji: “Msiogope, kwa maana tazama! ninawatangazia habari njema ya shangwe kubwa ambayo watu wote watakuwa nayo. Kwa sababu leo katika jiji la Daudi, amezaliwa mwokozi ambaye ni Kristo, Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu: Mtamkuta mtoto aliyefungwa kwa vitambaa akiwa amelala katika hori.” Ghafla, malaika wengi zaidi wanatokea na kusema: “Utukufu kwa Mungu katika vilele vilivyo juu, na amani duniani kwa watu wenye nia njema.”—Luka 2:10-14.

Baada ya malaika kuondoka, wachungaji wanaambiana: “Twendeni Bethlehemu tukaone jambo hili ambalo Yehova ametujulisha.” (Luka 2:15) Wanaondoka haraka na kumpata mtoto mchanga Yesu mahali ambapo malaika alisema wangempata. Wachungaji wanaposimulia mambo waliyoambiwa na malaika, wale wote wanaosikiliza wanashangaa! Maria anathamini sana maneno hayo naye anakata kauli moyoni mwake.

Watu wengi leo wanaamini kwamba Yesu alizaliwa Desemba 25. Lakini katika eneo la Bethlehemu, Desemba ni kipindi cha mvua na baridi. Pindi nyingine, hata kunakuwa na theluji. Wakati kama huo wa mwaka, wachungaji hawangekuwa nje malishoni usiku pamoja na wanyama wao. Pia, haiwezekani kwamba maliki Mroma angewaagiza watu ambao tayari walikuwa na mwelekeo wa kumwasi wasafiri kwa siku nyingi katika majira ya baridi kali ili waandikishwe. Inaonekana kwamba Yesu alizaliwa Oktoba.