Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 18

Yesu Aongezeka Naye Yohana Apungua

Yesu Aongezeka Naye Yohana Apungua

MATHAYO 4:12 MARKO 6:17-20 LUKA 3:19, 20 YOHANA 3:22–4:3

  • WANAFUNZI WA YESU WABATIZA WATU

  • YOHANA MBATIZAJI AFUNGWA GEREZANI

Baada ya kusherehekea Pasaka katika majira ya kuchipua ya mwaka wa 30 W.K., Yesu na wanafunzi wake wanaondoka Yerusalemu. Hata hivyo, hawarudi moja kwa moja nyumbani kwao huko Galilaya. Wanaenda katika eneo la Yudea, ambako wanabatiza watu wengi. Yohana Mbatizaji amekuwa akifanya kazi kama hiyo kwa karibu mwaka mmoja, na baadhi ya wanafunzi wake bado wako pamoja naye, labda katika bonde la Mto Yordani.

Yesu hambatizi mtu yeyote—wanafunzi wake wanabatiza watu chini ya mwelekezo wake. Katika kipindi hiki cha huduma ya Yesu, Yesu na Yohana wanawafundisha Wayahudi ambao wanatubu dhambi walizotenda dhidi ya agano la Sheria ya Mungu.—Matendo 19:4.

Lakini wanafunzi wa Yohana wanaona wivu, wanamlalamikia kumhusu Yesu: “Mtu [Yesu] aliyekuwa pamoja nawe . . . anabatiza na watu wote wanaenda kwake.” (Yohana 3:26) Lakini Yohana hana wivu. Anashangilia mafanikio ya Yesu na anataka wanafunzi wake washangilie pia. Yohana anawakumbusha: “Ninyi wenyewe mlishuhudia kwamba nilisema, ‘Mimi si Kristo, bali, nimetumwa nimtangulie.’” Anatoa mfano kuhusu jambo hilo ili wote waelewe: “Yule aliye na bibi harusi ndiye bwana harusi. Hata hivyo, rafiki ya bwana harusi, anaposimama na kumsikia, anashangilia sana kwa sababu ya sauti ya bwana harusi. Kwa hiyo shangwe yangu imekamilishwa.”—Yohana 3:28, 29.

Kama rafiki ya bwana harusi, Yohana alishangilia miezi kadhaa iliyopita alipowatambulisha wanafunzi wake kwa Yesu. Baadhi yao walimfuata Yesu na baada ya muda wangetiwa mafuta kwa roho takatifu. Yohana anataka pia wanafunzi wake wa sasa wamfuate Yesu. Kwa kweli, kusudi la Yohana ni kutayarisha njia kwa ajili ya huduma ya Yesu. Yohana anaeleza hivi: “Huyo lazima aendelee kuongezeka, lakini mimi lazima niendelee kupungua.”—Yohana 3:30.

Yohana mwingine, ambaye hapo awali alianza kumfuata Yesu, baadaye aliandika hivi kuhusu alikotoka Yesu na jukumu lake muhimu katika kuwaokoa wanadamu: “Yule anayetoka juu yuko juu ya watu wote. . . . Baba anampenda Mwana naye amekabidhi vitu vyote mkononi mwake. Yule anayemwamini Mwana ana uzima wa milele; yule asiyemtii Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu hukaa juu yake.” (Yohana 3:31, 35, 36) Huo ni ukweli muhimu ambao watu wanapaswa kujua!

Muda mfupi baada ya Yohana Mbatizaji kusema kwamba jukumu na kazi yake lazima ipungue, anakamatwa na Mfalme Herode. Herode amemchukua Herodia, mke wa Filipo ndugu yake wa kambo, na kumwoa. Yohana anapofunua hadharani kitendo hicho cha uzinzi, Herode anaagiza Yohana afungwe gerezani. Anaposikia kwamba Yohana amekamatwa, Yesu anaondoka Yudea pamoja na wanafunzi wake na ‘kwenda Galilaya.’—Mathayo 4:12; Marko 1:14.