Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 48

Afanya Miujiza, Lakini Akataliwa Hata Huko Nazareti

Afanya Miujiza, Lakini Akataliwa Hata Huko Nazareti

MATHAYO 9:27-34; 13:54-58 MARKO 6:1-6

  • YESU AWAPONYA VIPOFU NA MABUBU

  • WATU WA NAZARETI WAMKATAA

Yesu amekuwa na siku yenye shughuli nyingi. Baada ya kusafiri baharini kutoka eneo la Dekapoli, alimponya mwanamke aliyekuwa na mtiririko wa damu na kumfufua binti ya Yairo. Lakini bado siku haijaisha. Yesu anapoondoka nyumbani kwa Yairo, watu wawili ambao ni vipofu wanamfuata, wakisema kwa sauti: “Tuhurumie, Mwana wa Daudi.”—Mathayo 9:27.

Wanapomwita Yesu “Mwana wa Daudi” wanaume hao wanaonyesha kwamba wanaamini Yesu ndiye mrithi wa kiti cha ufalme cha Daudi na basi ndiye Masihi. Inaonekana Yesu anapuuza vilio vyao, labda ili kuona kama watasisitiza, nao wanasisitiza. Yesu anapoingia ndani ya nyumba, wale wanaume wawili wanamfuata. Yesu anawauliza: “Je, mna imani kwamba ninaweza kufanya hivyo?” Wanamjibu wakiwa na uhakika: “Ndiyo Bwana.” Ndipo Yesu anagusa macho yao na kusema: “Na itendeke kwenu kulingana na imani yenu.”—Mathayo 9:28, 29.

Ghafla wanaanza kuona! Kama Yesu alivyowaambia watu wengine hapo awali, anawaagiza watu hao wasitangaze jambo alilofanya. Lakini wakiwa na shangwe sana, baadaye wanazungumza kumhusu Yesu kila mahali.

Wanaume hao wawili wanapoondoka, watu wanamleta mtu ambaye hawezi kuzungumza kwa sababu ana roho mwovu. Yesu anamfukuza roho huyo mwovu, na papo hapo yule mtu anaanza kuzungumza. Umati unashangazwa na jambo hilo na kusema: “Jambo kama hili halijawahi kuonekana katika Israeli.” Mafarisayo wako hapo pia. Hawawezi kupinga miujiza hiyo, basi wanarudia shutuma zao kuhusu chanzo cha kazi za Yesu: “Anawafukuza roho waovu kwa nguvu za mtawala wa roho waovu.”—Mathayo 9:33, 34.

Muda mfupi baadaye, Yesu anarudi kwenye mji wake wa nyumbani, Nazareti, akiwa pamoja na wanafunzi wake. Karibu mwaka mmoja uliopita, alifundisha huko katika sinagogi. Mwanzoni watu walishangazwa na mambo aliyosema, lakini baadaye wakakasirishwa na mafundisho yake na wakajaribu kumuua. Sasa Yesu anajaribu tena kuwasaidia majirani wake wa zamani.

Siku ya Sabato, anarudi kwenye sinagogi ili kufundisha. Wengi wanashangaa, hata wanauliza: “Mtu huyu alipata wapi hekima hii na matendo haya yenye nguvu? Wanasema: “Je, huyu si mwana wa yule seremala? Je, mama yake haitwi Maria, na ndugu zake Yakobo, Yosefu, Simoni, na Yuda? Na dada zake, je, wote hawako pamoja nasi? Basi, alipata wapi mambo haya yote?”—Mathayo 13: 54-56.

Watu wanafikiri kwamba Yesu ni mtu wa kawaida tu katika eneo hilo. Wanawaza hivi, ‘Tulimwona akikua, basi anawezaje kuwa Masihi?’ Kwa hiyo, licha ya uthibitisho wote—kutia ndani hekima ya Yesu na kazi zake zenye nguvu—wanamkataa. Kwa kuwa wanamfahamu, hata watu wake wa ukoo wanakwazika kwa sababu yake, na hivyo Yesu anasema: “Nabii anaheshimiwa kila mahali isipokuwa katika eneo lake la nyumbani na katika nyumba yake mwenyewe.”—Mathayo 13:57.

Kwa kweli, Yesu anashangazwa na ukosefu wao wa imani. Kwa hiyo, hafanyi miujiza yoyote huko “isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya.”—Marko 6:5, 6.